|
Sifa njema ni za Allah,
Bwana wa Ulimwengu, na rehma na amani zimshukie Mtume wetu
Muhammad na aali zake na sahaba zake.
“'Iyd” ni neno la kiarabu linalomaanisha
jambo la kitabia au ada, lenye kurudi na kujirejea.
'Iyd au
sikukuu ni alama au nembo inayopatikana katika kila taifa,
ikiwa ni pamoja na mataifa yale yaliyotajwa katika vitabu
vitukufu na yale ya waabudiao masanamu, pamoja na wengineo,
kwa sababu kusherehekea sikukuu ni jambo la kimaumbile
katika maumbile ya mwanaadamu. Watu wote wanapenda kuwa na
matukio maalumu ya kufanya sherehe, ambapo wanaweza
kukukusanyika pamoja na kuonyesha furaha zao.
Sikukuu za mataifa ya makafiri zinaweza
kufungamanishwa na mambo ya kidunia, kama kuanza kwa mwaka,
kuanza kwa msimu wa kilimo, kubadilika kwa hali ya hewa,
kuanzishwa kwa dola, kutawazwa kwa kiongozi, n.k. Zinaweza
pia kufungamanishwa na matukio ya kidini, kama ambavyo
nyingi ya sikukuu zinazowahusu Mayahudi na Wakiristo tu,
mfano Alkhamisi ambayo wanadai kuwa meza maalum
iliteremshwa kwa Yesu, Krismas, Mwaka Mpya, Siku ya
kushukuriana, na sikukuu ambazo watu hupeana zawadi.
Hizi husherehekewa katika nchi zote za Ulaya na Amerika ya
Kaskazini hivi sasa, na katika nchi nyengine ambazo ukristo
una nguvu, hata kama nchi yenyewe si ya kikiristo kiuhalisi.
Baadhi ya wanaoitwa Waislam huweza kujiunga katika sikukuu
hizi, kwa sababu ya ujinga au unafiki.
Magians nao pia wana sikukuu zao, kama
Mahrajaan, Namrudh n.k.
Ma-baatini (Miongoni mwa Mashia)
wana sikukuu zao pia, kama ‘Eid al-Ghadeer”, ambapo wanadai
kuwa Mtume (SAW) amempa ukhalifa ‘Ali (RA) na maimamu kumi
na moja baada yake.
Waislamu
wanatambulika kwa sikukuu zao.
Maneno ya Mtume (SAW)
"Kila Umma una sikukuu yake
na hii ni sikukuu yenu" yanaonyesha
kuwa Eid hizi mbili ni maalumu kwa Waislamu tu, na kuwa
hairuhusiwi kwa Muislam kuwaiga makafiri na washirikina nao
katika jambo lolote ambalo ni maalumu ndani ya
sherehe zao, iwapo kama ni chakula, nguo, kuwasha moto au
matendo ya ibada.
Watoto wa Kiislam wasiruhusiwe kucheza
katika sikukuu hizo za kikafiri, au kujipamba, au kujumuika
na makafiri katika matukio hayo. Sikukuu zote za kikafiri au
zilizozushwa ni haraam, mfano kama sherehe za Siku ya Uhuru,
maadhimisho ya mapinduzi, miti ya sherehe za sikukuu au
kutawazwa kwa kiongozi, siku za kuzaliwa, Sikukuu ya
Wafanyakazi, Sikukuu ya Nile, Shimm al-Naseem (sikukuu ya
majira ya baridi ya Wamisri), siku ya walimu, na Maulidi ya
Mtume (Kuzaliwa kwa Mtume ).
Waislam hawana sikukuu ukiacha ile ya Eid
al-Fitr na Eid al-Adh’haa, kwa sababu ya hadiith iliyotolewa
na Anas (RA) amesema: "Mjumbe wa
Allah (SAW) alikuja Madiynah na watu walikuwa na siku mbili
wakicheza na kufurahi. Akauliza, "Ni siku gani hizi mbili?"
Wakasema, "Tulikuwa tukicheza na kufurahi katika siku hizi
zama za ujaahiliyya" (zama za ujinga kabla ya Uislamu).
Mtume (SAW) akasema, "Allaah Amekupeni siku bora kuliko
hizo, nazo ni siku ya 'Eid Al-Adhaa na siku ya 'Eid Al
Fitr". (sunan Abi Dawuud 1134)
Yafuatayo ni maelezo kuhusu sheria na adabu
za Eid mbili kwa mujibu wa Sharia ya Kiislam:
AHKAAM
AL-'IYD (Sheria katika 'Iyd)
Kufunga
Ni haram kufunga katika siku za Eid kutokana
na hadiith ya Abu Sa’iyd al-Khudri (RA), amesema kuwa Mtume
(SAW) amekataza kufunga katika siku ya Fitr na katika siku
ya Kuchinja (Adh’haa). (Imeripotiwa na Muslim, 827)
Sheria katika Sala
za 'Iyd
Baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa Sala ya
Eid ni waajib, huu ni mtizamo wa wanavyuoni wa Kihanafi na
Shaykh al-Islam Ibn Taymiyah (RA). Wanasema kuwa Mtume (SAW)
alikuwa akisali sala zote za Eid na hakuacha kufanya hivyo
hata mara moja. Wamechukua ushahidi katika aya (yenye
tafsiri),
"Basi
sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi"
Al-Kawthar: 2
Yaani Sala ya Eid na kuchinja baada yake,
ambayo ni amri, na kwa ukweli kuwa Mtume (SAW) aliwaamrisha
wanawake watolewe kuhudhuria sala ya Eid, na kwamba mwanamke
aliyekuwa hana jilbaab aazime kutoka kwa ndugu yake
Baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa sala ya
Eid ni Fardh Kifaaya (fardhi yenye kutosheleza). Huu ni
mtizamo wa Kihambali. Kundi la tatu linasema kuwa sala ya
Eid ni sunnah iliyokokotezwa. Huu ni mtizamo wa Kimaalik na
Kishaafi. Wanachukua ushahidi ya hadiith ya Bedui inayosema
kuwa Allaah (SWT) Hakufaradhisha sala yoyote kwa waja Wake
zaidi ya zile sala tano. Kwa hiyo Waislam wafanye hima
kuhudhuria sala ya Eid, hususan kwa kuwa maoni ya kuwa ni
wajiib yameegemea katika ushahidi wenye nguvu. Neema,
baraka na malipo makubwa yanapatikana kwa kuhudhuria sala za
Eid, na kwa ukweli kuwa mtu atakuwa anafuata mwendo wa Mtume
(SAW) kwa kufanya hivyo, basi inatosha kuwa ni changamoto.
Mambo ya lazima na
wakati wa Sala ya 'Iyd
Baadhi ya
wanavyuoni wa Kihambali wanasema kuwa sharti za Sala ya Eid
ni iqaamah lazima isomwe na ni lazima isaliwe kwa jamaa.
Baadhi yao wamesema kuwa sharti za sala ya Eid ni sawa na
zile za sala ya Ijumaa, isipokuwa katika khutba, ambapo
kuihudhuria si lazima. Wengi miongoni mwa wanavyuoni
wanasema wakati wa sala ya Eid unaanza pale jua
linapochomoza kwa masafa ya urefu wa mshale, kwa
linavyoonekana kwa macho matupu, na unaendelea mpaka jua
linapokaribia kuwa sawa sawa
Maelezo ya Sala ya
'Iyd
‘Umar (RA)
amesema: “ Sala ya Eid Fitri na al-Adh’haa ni rakaa mbili
zilizotimia, sio fupi fupi. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya
Mtume, na muongo ni mwenye kulaaniwa.”
Abu Sa’iyd
amesema: “Mtume (SAW) amekuwa akija
katika pahala pa kusalia katika siku za Fitr na al-Adh’ha,
na jambo la mwanzo analofanya ni kusali”.
Takbiira
inarejewa mara saba katika rakaa ya mwanzo na mara tano
katika rakaa ya pili, Qur’an inasomwa baada yake katika kila
rakaa.
Imeripotiwa kutoka kwa A’ishah:
Takbira ya al-Fitri na al-Adh’haa ni mara saba katika rakaa
ya mwanzo na mara tano katika rakaa ya pili, mbali na
Takbiira ya rukuu .
(imeripotiwa na Abu Dawuud; imesahihishwa na jumla
ya isnaad)
Iwapo mtu
amejiunga na sala amemuwahi imaam wakati wa Takbira hizi za
ziada, ni juu yake kusema “Allaahu Akbar” pamoja na imaam,
na halazimiki kuzilipa Takbira ambazo zimempita, kwa sababu
(takbira hizo) ni sunna, sio waajib.
Kuhusu nini kinatakiwa kisemwe baina ya Takbiira,
Hammaad ibn Salamah ameripoti kutoka kwa Ibraahiim kuwa
"Waliid ibn ‘Uqbah aliingia
msikitini wakati Ibn Mas’uud, Hudhayfah na Abu Muusa wapo
hapo, na akasema, “Eid ipo hapa, nini natakiwa kufanya?” Ibn
Mas’uud akasema: “Sema ‘Allaahu Akbar’, msifu na mshukuru
Allaah, msalie Mtume (SAW) na omba du’a, kisha sema ‘Allaahu
Akbar’, msifu na mshukuru Allaah, msalie Mtume (SAW)….n.k.’
(Imeripotiwa na at-Tabaraani. Ni hadithi sahihi
iliyonukuliwa katika al-Irwaa’ na kwengineko).
Kusoma Qur’aan
katika Sala za 'Iyd
Imependekezwa (mustahabb) kuwa katika Sala
za Eid, imaam asome surat Qaaf (sura ya 50) na surat
al-Qamar (sura ya 54), kama ilivyoripotiwa katika Sahiih
Muslim kuwa
‘Umar ibn Al-Khattwaab alimuuliza
Abu Waaqid al-Laythi, “Nini Mjumbe wa Allaah (SAW) alikuwa
akisoma katika [Eid] al-Adh’haa na al-Fitr?” Akasema,
“Alikuwa akisoma Qaaf, Wal-Qur’aan al-majiid [Qaaf 50:1] na
Iqtarabat as-saa’ah wa’nshaqq al-qamar [al-Qamar 54:1].
Ripoti nyingi zinaonyesha kuwa Mtume (SAW)
alikuwa akisoma Suurat al A’laa [87] na Suurat al-Ghaashiyah
{88], kama ambavyo alivyokuwa akizisoma katika sala ya
Ijumaa. Al-Nu’maan ibn Bishr amesema:
"Mtume (SAW) alikuwa
akisoma katika 'Eid mbili na siku ya Ijumaa Sabbih Isma
Rabbikal-a'laa (Al-A'alaa 87:1) na Hal Ataaka
Hadiythul-Ghaashiyah (Al-Ghaashiyah 88:1)"
Sahiyh Muslim 878
Samura (RA) amesema
"Mtume (SAW) alikuwa akisoma
katika Eid mbili Sabbih Isma Rabbikal-a'alaa (Al-a'alaa
87:1) na Hal Ataaka Hadiythul-Ghaashiyah (Al-Ghaashiyah
88:1) Imesimuliwa na Ahmad na wengine ni Sahiyh [
Al-Irwaa 3/116]
Sala inasaliwa
kabla ya khutbah
Moja ya sheria za Eid ni kuwa sala ni lazima
iwe kabla ya khutbah, kama ilivyoripotiwa katika Musnad
Ahmad kutoka katika hadiith ya Ibn ‘Abbaas, ambaye
ameshuhudia kwamba
Mtume (SAW) alisali kabla ya khutba
siku ya Eid kisha akatoa khutba (Musnad Ahmad 1905.
Hadiythi hii pia iko katika Sahihi mbili)
Yeyote anayetaka
kuondoka wakati wa khutbah ameruhusiwa kufanya hivyo
‘Abd- Allaah ibn al-Saab amesema:
"Nilihudhuria 'Eid pamoja na Mtume
(SAW) na alipomaliza alisema, tutatoa khutba, kwa hiyo
anayetaka kukaa (na kusikiliza) khutba basi akae na
anayetaka kuondoka basi aondoke (Irwaa al Ghaliyl
3/96)
Sala isicheleweshwe kwa muda mrefu:
‘Abd-Allaah ibn Bishr, sahaba wa Mtume
(SAW), alitoka pamoja na watu siku ya Fitr au al-Adh’haa, na
akaonyesha kutopendezwa kwa kuwa imaam alikuja akiwa
amechelewa sana. Akasema " Wakati
wa Mtume (SAW) tungelikuwa tumeshamaliza wakati wa sasa" na
huo ulikuwa wakati wa Tasbiyh (Imesimuliwa na na
Bukhaari).
Sala
za sunna, pahala pa Sala (ya 'Iyd)
Hakuna sala za
sunna ambazo zinasaliwa kabla au baada ya sala ya Eid, kama
alivyoripoti Ibn ‘Abbaas kuwa
"Mtume (SAW) alikuwa akitoka katika siku ya Eid na akasali
rakaa mbili, bila ya chochote (sala yoyote) kabla au baada
yake". Hali hii ni iwapo sala itasaliwa pahala pa
kusaliwa au sehemu ya wazi. Hata hivyo, iwapo watu watasali
Eid msikitini, basi watatakiwa wasali rakaa mbili za Tahiyat
al-Masjid (sala ya kiamkizi cha msikiti) kabla hawajakaa
kitako.
Iwapo watu hawatokuwa na habari ya 'Iyd mpaka siku ya pili
Abu ‘Umayr ibn
Anas ameripoti kutoka kwa ami yake miongoni mwa Ansaar kuwa
alisema:
"Kulikuwa na mawingu
na hatukuweza kuuona mwezi wa
Shawwaal, kwa hiyo tukaanza sikukwa kufunga, kisha ukaja
msafara mwisho wa siku na wakamwabia Mtume (SAW) kuwa
wameona mwezi wa Shawwaal siku moja kabla, akawaambia watu
waache kufunga na wakaenda kuswali Eid siku ya pili"
Imeripotiwa na watano, ni Sahiyhi; Al-Irwaa' 3/102
Iwapo mtu
amekosa sala ya Eid, mtazamo ulio sahihi kuliko yote ni kuwa
anaweza kuilipa kwa kusali rakaa mbili.
Kuhudhuria kwa
Wanawake katika Sala za 'Iyd
Hafsah amesema:
"Tulikuwa tukiwazuwia wasichana wenye hedhi kuhudhuria Sala
za Eid. Kisha akaja mwanamke kukaa katika ngome ya Banu
Khalaf na akatumambia kuhusu dada yake. Mume wa dada yake
alihudhuria vita kumi na mbili pamoja na Mtume (na
akasema) , Dada yangu alikuwa naye katika vita sita.
Akasema tulikuwa tukiwatendea walioumia na tukiwashughulikia
wagonjwa. Dada yangu alimuuliza Mtume kama kuna ubaya
wowote kutokwenda kusali Eid ikiwa hana jilbaab. Akasema
"mwache rafiki yake ampe moja wa jilbaab lake ili aweze
kushuhudia baraka za Eid na aone kujumuika kwa Waislamu"
Umm 'Atiya alipokuja nilimuuliza umemiskia Mtume (SAW)
akisema hivyo? " Akasema "Baba yangu achinjwe kwa ajili
yake" Na alikuwa hamtaji ila baada ya kusema "baba yangu
achinjwe kwa ajili yake" . "Nimemsikia akisema kuwa
wasichana na wale wanaotawishwa au wasichana waliotawishwa
na wanawake wenye hedhi ili washuhudie baraka za Eid na
kujumuika kwa waumini. Lakini wale wenye hedhi wakae mbali
na sehemu ya kusali" (Sahiyh Al Bukhaari)
Vijana wa kike (‘awaatik, mmoja ‘aatiq) ni
wale waliokwisha vunja ungo au wako karibu na kufanya hivyo,
au wamefikia umri wa kuolewa, au walio na thamani
katika familia zao, au wasiofanyishwa kazi zisizo na
heshima. Inaonekana kuwa wamekuwa wakizuiwa vijana hawa
kutoka nje kwa sababu ya uovu uliojitokeza baada ya
kizazi cha kwanza cha Uislam; lakini Sahaabah
hawakukubaliana na hilo na wakaona kuwa sheria ya wakati wao
lazima ibaki kama ilivyokuwa wakati wa Mtume (SAW).
“Jilbaab lake”- ametakiwa kuazima baadhi ya
nguo ambazo hakuwa akizihitajia.
“Wanaotengwa/Wanaotawishwa”- ambao
wanaowekewa paazia kipembeni mwa nyumba ambamo wari hukaa
nyuma yake.
“Wanawake walio katika hedhi”- huyyadh,
mmoja haa’idh– hii inaweza kurejea kwa vijana wa kike
waliofikia umri wa kukua, au wanawake waliomo katika siku
zao na wasio tohara.
“Wanawake walio katika hedhi wanatakiwa
wajitenge na sala – pahala penyewe” – Ibn al-Munayyir
amesema: "Sababu ya kujitenga na
sehemu ya kuswali ni kuwa wakisimama pamoja na wanawake
wanaosali japokuwa hawasali, itaonekana kuwa hawana heshima
na sala au hawajali kwa hiyo ni bora kwao kuepuka kufanya
hivyo"
Imesemekana kuwa sababu ya kutakiwa wanawake
walio katika hedhi kujitenga na sehemu ya kusalia ni
tahadhari, kuwa wanawake wasije karibu ya wanaume bila ya
sababu iwapo wao hawasali, au wasiwaudhi wengine kwa damu au
harufu yake.
Hadiith hii
inamtaka kila mmoja kuhudhuria sala ya Eid, na kushirikiana
baina yao katika wema na ucha Mungu. Wanawake walio katika
hedhi wasiachwe nyuma katika kumtaja Allaah au sehemu njema
kama mikusanyiko yenye madhumuni ya kutafuta elimu na
kumtaja Allaah – ukiachia misikitini. Hadithi hii pia
inaonyesha kuwa wanawake wasitoke nje bila ya jilbaab.
Hadithi hii
inatuambia kuwa sio sawa kwa vijana wa kike na wanawake
wanaotawishwa kutoka nje bila ya sababu inayokubalika.
Inasema kuwa imependekezwa (mustahabb) kwa wanawake kuvaa
jilbaab, na kuwa imeruhusiwa kuazimana nguo. Pia imeonyesha
kuwa sala ya Eid ni wajibu.
Ibn Abi Shaybah
pia ameeleza kuwa Ibn ‘Umar alikuwa akenda nae yeyote
anaeweza kwenda nae katika wanawake wa nyumbani kwake katika
sala za Eid.
Hadithi ya Umm
‘Atiyah pia inaeleza sababu ya sheria hii, ni kuwa ili
wanawake waweze kushuhudia baraka ya Eid, waone mkusanyiko
wa Waislam, na wapate nao baraka na utukufu wa siku hii.
At-Tirmidhi
(Mwenyeezi Mungu Amrehemu) alisema katina Sunan yake, baada
ya kutaja Hadiyth ya Umm 'Atiya, "baadhi ya 'ulamaa
wamechukulia Hadiythi hii na kuwaruhusu wanawake waende
katika Sala za Eid na wengineo hawakupendezewa. Imeripotiwa
kuwa 'Abdullah Ibn Al Mubaarak alisema, 'Sipendi wanawake
waende katika Sala za Eid siku hizi. Na mwanamke
akishikilia kwenda basi mumewe amwachilie kwenda lakini
anapokwenda avae nguo zake kukuuu kabisa na asijipambe.
Na akishikilia kujipamba basi asitoke nje. Na hali hii
mume anayo haki kumzuwia kutoka nje.
Imeripotiwa kuwa bibi 'Aishah (RA)
alisema, "Kama Mtume (SAW) angeliona hali za wanawake
walivyo hivi sasa angeliwazuwia kwenda misikitini
kama vile wanawake wa Bani
Israaiyl walivyozuiliwa" Imeripotiwa kwamba Sufyaan
Al Thawriy hakupendezewa wanawake kwenda kuswali Swalah za
Eid. (At-Tirmidhiy 495)
Umm ‘Atiyah
ametoa fatwa yake katika hadithi iliyotajwa hapo juu, muda
baada ya kufa Mtume (SAW) kufariki, na haikuripotiwa kuwa
yeyote miongoni mwa Masahaba amepingana na fatwa hii. Maneno
ya ‘Aa’ishah,
“Iwapo Mtume (SAW) angeona
yanayofanyika kwa wanawake, angewazuilia kwenda misikitini”,
hayapingi hii fatwa (alimradi tu wanawake wanatimiza
masharti ya Kiislamu ya kutoka kwao nje)
Ni vizuri zaidi iwapo ruhusa itatolewa kwa wale
wanawake wasiotoka kwa ajili ya kuwaangalia wanaume au
kuangaliwa wao, ambao kuhudhuria kwao hakutopelekea uovu
wowote na wasiokwenda kusongamana na wanaume mitaani au
msikitini (yaani wanawake ambao kutoka kwao hakutosababisha
fitna au kishawishi kwake au kwa wanaume).
Wanaume
wawakague wanawake wao wanapotoka nje kwa ajili ya sala
kuhakikisha kuwa hijabu zao ziko kamili, kwa sababu wao ndio
“wachungaji” wenye jukumu kwa “machunga” wao. Wanawake
wanatakiwa watoke wakiwa katika nguo zisizovutia, wasiwe
wamejipamba au kujitia manukato. Wanawake walio katika hedhi
wasiingie msikitini au sehemu ya kusalia; wanaweza kungojea
ndani ya gari, kwa mfano, ambapo wanaweza kusikia khutbah.
ADAAB ZA 'IYD
Kukoga
Moja ya heshima za Eid ni kukoga kabla ya
kwenda katika sala. Imeripotiwa katika ripoti sahihi katika
al-Muwatta’ na kwengineko kuwa ‘Abd-Allaah ibn ‘Umar alikuwa
akikoga siku ya al-Fitr kabla ya kuja pahala pa kusalia.
(al-Muwatta’428)
Imeripotiwa kuwa Sa'iyd
ibn Jubayr alisema "Mambo matatu ni Sunnah siku ya Eid;
kwenda kwa miguu katika uwanja wa kusali (Mswallah),
kukoga, na kula kabla ya kutoka nje" . Hivi ndivyo
alivyosema Sa'id ibn Jubayr na labda amejifunza haya kutoka
kwa baadhi ya maswahaaba.
An-Nawawi (RA) ametaja kuwa wanavyuoni
wamekubaliana kuwa imependekezwa (mustahaab) kukoga kabla ya
sala ya Eid.
Sababu ya kuwa ni mustahaab kukoga kabla ya
sala ya Ijumaa na mikusanyiko mengine pia inahusika katika
suala la Eid vilevile.
Kula kabla ya kutoka
Mtu asitoke kwenda pahala pa kusalia Eid
al-Fitr kabla ya kula tende, kwa sababu ya hadiith
iliyosimuliwa na al-Bukhari kutoka kwa Anas ibn Maalik
ambaye amesema:
"Mtume (SAW) alikuwa hatoki
asubuhi ya Eid Al Fitr mpaka ale tende na alikuwa kila kwa
hesabu ya witri. (odd)
(al-Bukhaari,
953)
Imependekezwa (mustahaab) kula kabla ya
kutoka kwa sababu hii inahakikisha kuwa hatukuruhusiwa
kufunga katika siku hiyo, na ni onyesho kuwa saumu sasa
imemalizika. Inb Hajar (RA) ameeleza kuwa hii ni kwa ajili
ya kuwakinga watu kuendeleza saumu na pia inamaanisha utii
kwa Allaah (SWT).(Fath, 2/446).
Iwapo mtu hatakuwa na tende, anaweza
kufutari kwa chochote kilichoruhusiwa. Kwa upande mwengine,
katika Eid al-Adh’haa, imependekezwa mtu asile mpaka baada
ya sala, ambapo mtu anatakiwa kula nyama ya mnyama mmojawapo
aliyechinjwa (kwa ajili ya siku hii).
Takbira (Allaahu
Akbar) katika siku ya 'Iyd
Hii ni moja ya sunnah kubwa kabisa ya siku
hii, kwa sababu ya maneno ya Allaah (yenye tafsiri):
"......Mwenyezi Mungu
anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito,
na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa
amekuongoeni ili mpate kushukuru"
al-Baqarah 2:185].
Ad-Daaraqutni na wengine wameripoti kuwa
wakati Ibn ‘Umar alipokuwa akitoka katika Eid al-Fitr na
al-Adh’haa, huwa anajitahidi kutoa Takbiir mpaka anapofika
pahala pa kusalia, kisha kuendelea na Takbiir mpaka aje
imaam.
Tendo la kutoa Takbiira kutoka nyumbani hadi
pahala pa kusalia, na mpaka imaam aingie, ni maarufu
miongoni mwa salaf na limeripotiwa na waandishi wengi kama
Ibn Abi Shaybah, ‘Abd al-Razzaaq na al-Firyaabi katika
kitabu chake Ahkaam al-‘Eidayn kutoka katika kundi la salaf.
Moja ya mfano wake ni ripoti kuwa Naafi’ ibn Jubayr alikuwa
akitoa Takbiira na alikuwa akishangaa kwa nini watu
hawafanyi hivyo. Alikuwa akiwaambia watu, "Kwa nini hamfanyi
Takbiir? Ibn Shihaab Al Zuhri kasema, "Watu walikuwa
wakifanya takbiir kuanzia wakati wanapotoka majumbani mwao
hadi anapoingia imaam".
Wakati wa kutoa Takbiira katika Eid al-Fitr
unaanza usiku wa kuamkia Eid mpaka wakati imaam anapofika
kuongoza sala.
Maneno ya Takbiira
Ibn Abi Shaybah ameripoti katika al-Musannaf
kuwa Ibn Mas’uud (RA) alikuwa akitamka takbira katika siku
za Tashriiq kama ifuatavyo:
“Allaahu akbar, Allaahu
akbar, laa ilaaha ill-Allaah, wa Allaahu akbar, Allaahu
akbar wa Lillaahi’l-hamd (Allaah ni Mkubwa kabisa
….hakuna Mungu isipokuwa Allaah, Allaah ni Mkubwa kabisa, na
sifa zote njema ni za Allaah)’. Ibn Abi Shaybah aliripoti
haya mahala pengine katika isnaad hiyo hiyo, lakini ikiwa na
pamoja na maneno “Allaahu Akbar” ikirejewa mara tatu.
Al-Muhaamili pia ameripoti kuwa Ibn Mas’uud
alikuwa akisema :
“Allaahu akbar kabiiran, Allaahu
akbar kabiiran, Allaahu Akbar wa ajall, Allaahu Akbar wa
Lillaahi’l-hamd
(Allaah ni Mkumbwa kabisa, Allaah ni Mkubwa kabisa, Allaah
ni Mkubwa kabisa, Allaah ni Mkubwa kabisa na Mtukufu, na
sifa zote njema ni za Allaah)”. (al-Irwaa’, 3/126).
Kupongezana
Watu wanaweza kupeana pongezi na salaam
njema za Eid, bila ya kujali aina ya maneno. Mfano wanaweza
wakaambizana, “Taqabbal Allaah
Minnaa Wa Minkum
(Allaah azikubali [ saumu na ibada] zetu na zenu” au “Eid
mubarak” na mfano wa hayo katika salaam zilizoruhusiwa.
Tendo la
kupeana salamu limekuwa maarufu wakati wa Masahaaba na
wanavyuoni kama Imaam Ahmad na wengine wameruhusu hilo. Kuna
ripoti zinazoonyesha imeruhusiwa kuwapongeza watu katika
matukio maalum. Masahaaba walikuwa wakipongezana wakati
linapotokea jambo zuri, mfano pale Allaah alipokubali toba
ya mtu n.k.
Hakuna shaka
kuwa kumpongeza mtu kwa namna hii ni moja kati ya namna ya
heshima zaidi katika tabia njema na ni moja kati ya muamala
mzuri sana wa jamii ya Waislam.
Kuvaa vizuri zaidi siku ya 'Iyd
'Abdullah ibn 'Umar (RA) amesema,
'Umar alichagua jubbah (nguo refu inayovaliwa juu ya kanzu)
ambayo ilitengenezwa kwa hariri na ilikuwa ikiuzwa kwa bei
ya takhfifu sokoni, aliileta kwa Mtume (SAW) na akasema,
"ewe Mtume nunua hii na uvae kwa ajili ya Eid na
watakapokuja wageni" Mtume (SAW) akasema "Hizi ni nguo za
yule ambaye hana sehemu akhera
(imeripotiwa na Al-Bukhaari 948)
Mtume (SAW) alikubaliana na mawazo ya ‘Umar
ya mtu kuvaa vizuri zaidi, lakini alikataa na kupingana na
mawazo ya kununua jubbah hilo kwa sababu lilikuwa
limetengenezwa kwa hariri.
Al-Bayhaqi ameripoti kuwa Ibn Umar alikuwa
akivaa nguo zake nzuri siku ya Eid, kwa hivyo wanaume
wanatakiwa wavae nguo nzuri zaidi walizokuwa nazo wanapotoka
kwa ajili ya Eid.
Kwa upande mwengine, wanawake, wajiepushe na
mapambo wanapotoka kwa ajili ya Eid, kwa sababu wao
wamekatazwa kuonyesha mapambo yao mbele ya wanaume wasio
mahrim zao. Mwanamke anayetaka kutoka ameharamishiwa kujitia
manukato au kujionyesha kwa njia ya kushawishi mbele ya
wanaume, kwa sababu yeye ametoka kwa ajili ya ibada tu. Je,
unafikiria kuwa ni sahihi kwa mwanamke muumini kumuasi Yule
Ambae yeye (mwanamke) anatoka kwenda kumuabudu, na kwenda
kinyume na amri Zake kwa kuvaa
nguo za kuvutia zenye kumbana na za rangi
zinazong’ara au kujitia manukano n.k?
Sheria katika
kusikiliza khutba za 'Iyd
Ibn Qudaamah (RA) amesema katika kitabu
chake cha al-Kaafi (p.234):
Imaam anapotoa salaam (mwisho wa Swalah)
atoe khutba sehemu mbili kama khutba ya Ijumaa kwa sababu
Mtume (SAW) alifanya hivyo. Khutba ya Eid ni tofauti na
khutba ya Ijumaa kwa mambo manne, jambo la nne ambali ni
Sunnah na sio fardhi kusikiliza kwa sababu imeripotiwa
kwamba 'Abdulla bin Al-Saa'ib alisema,
"Nilihudhuria Eid na Mtume
(SAW) na alipomaliza kuswali, alisema "tutatoa khutba sasa
kwa hiyo anayependa kukaa (na kusikiliza) akae na yeyote
anayetaka kuondoka basi na aondoke".
Katika al-Sharh al-Mumti’ ‘ala Zaad
al-Mustanfi’ cha Ibn ‘Uthahymiin, 5/192, kinasema:
“Maneno [ya Ibn Qudaamah], ‘kama khutbah
mbili za Ijumaa’ inamaanisha kuwa anatakiwa atoe khutbah
mbili, hata kama kuna kutokubaliana katika jambo hili, kama
ambavyo tumetaja hapo juu. Khutba ya Eid, imeegemea katika
sheria zilizo sawa na za Ijumaa, hata katika nukta ya
kuzumgumza wakati wa khutba hiyo ni haraam, lakini sio
wajibu kuhudhuria, hali ya kuwa kuhudhuria khutba ya Ijumaa
ni wajibu, kwa sababu Allaah (SWT) Amesema
(maana ya maneno hayo):
"Enyi mlio amini!
Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri
ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara"
Al-Jumu'aa :9
Kuhudhuria khutba ya Eid sio wajibu, na mtu
anaruhusiwa kuondoka, bali iwapo atabakia, ni lazima
asizungumze na yeyote. Hivi ndivyo muandishi alivyokusudia
aliposema ‘kama khutba mbili za Ijumaa’. “
Mmoja wa wanavyuoni amesema: “Si wajibu
kusikiliza khutba za Eid, kwa sababu kama ingelikuwa ni
wajibu kuzihudhuria na kuzisikiliza basi ingekuwa ni haraam
kuondoka. Lakini kwa kuwa imeruhusiwa kuondoka, basi si
wajibu kusikiliza”.
Hata hivyo, iwapo mazungumzo yatawakera wale
wanaosikiliza, ni haraam kuzungumza kwa sababu ya kero hizo,
sio kwa sababu ya kutokusikiliza. Kwa msingi huu, iwapo mtu
atakuwa na kitabu wakati imaam anakhutubia, basi ameruhusiwa
kukisoma, kwa sababu kufanya hivyo hakutomkera yeyote.
Lakini kwa mujibu wa madh’hab anayofuata muandishi huyu, ni
wajibu kusikiliza khutba hiyo iwapo utakuwepo (hapo pahala
pa kusalia).
Mtu kutoka kwa
njia moja na kurudi kwa kutumia njia nyengine
Jabir ibn ‘Abd-Allah
(RA) ameripoti kuwa Mtume (SAW) alikuwa akibadilisha njia
siku ya Eid. (imeripotiwa na
al-Bukhari, 986)
Imeripotiwa kuwa Mtume (SAW) alikuwa akitoka
kwa miguu, na alikuwa akisali bila ya adhana wala iqaamah,
kisha hurudi kwa kutumia njia nyengine tofauti. Inasemekana
kuwa njia hizi mbili zitamtolea ushahidi siku ya Kiyama, kwa
sababu siku hiyo ardhi itasema juu ya kila kitu
kilichofanywa juu yake, zuri na baya. Vile vile inasemekana
kuwa imefanywa hivi ili kuonyesha alama na utamaduni
wa Kiislam katika njia zote mbili; kutoa ukumbusho wa
Allah; kuwavunja moyo wanafiki na Mayahudi na
kuwaogopesha kwa wingi wa watu walio pamoja nae; kutimiza
mahitaji wa watu kwa kuwapa fatwa, kuwasomesha na kuwawekea
mifano ya kuifuata; kuwapa sadaka wale wanaohitajia; au
kuwatembelea jamaa zake na kukuza mahusiano yao.
Tahadhari juu ya kufanya maovu
1. Baadhi ya watu wanadhani kuwa Uislam
unatuambia kukesha na kusali usiku wa Eid, kwa kunakili
hadithi ya uongo inayosema "Yeyote atakayekesha usiku wa Eid
moyo wake hautokufa siku ya kufa moyo wake" Hadithi hii
imeripotiwa katika isnaad mbili moja ambayo ni dhaifu na ya
pili ni dhaifu sana.
Uislam hautuambii kuutenga usiku wa Eid
kwa kukesha na kusali; hata hivyo, iwapo mtu ana tabia ya
kuamka na kusali usiku (qiyaam), hakuna ubaya wa kufanya
hivyo katika usiku wa Eid pia.
2.
Mchanganyiko wa wanawake na
wanaume katika maeneo ya sala, mitaani, n.k. Inasikitisha
kuwa haya yanatokea sio misikitini tu, bali hata katika
sehemu tukufu zaidi, al-Masjid al-Haram [Makkah]. Wanawake
wengi, Allaah Awaongoze wanatoka wakiwa hawajajisitiri,
wamejipamba na kujitia manukato, wanaonyesha mapambo
yao, wakati kuna mkusanyiko mkubwa katika msikiti huo.
Hatari ya hali hii iko wazi kabisa. Kwa hiyo wale wahusika
ni lazima wapange sala za Eid vizuri, kwa kuweka milango
tofauti na njia tofauti kwa wanawake na wawacheleweshe
wanaume kutoka mpaka wanawake wawe wameshatoka.
3.
Baadhi ya watu wanajikusanya
siku ya Eid kwa ajili ya kuimba na kufanya aina nyengine za
….burudani, na hii haikuruhusiwa.
4.
Baadhi ya watu wanashereheka
katika Eid kwa sababu Ramadhani imemalizika na kuwa
hawahitajiki tena kufunga. Haya ni makosa, waumini
wanasherehekea Eid kwa sababu Allaah Amewasaidia wao
kumaliza mwezi wa saumu, sio kwa sababu ya kumalizika kwa
saumu ambayo watu wengine wanaichukulia kuwa ni mzigo.
Tunamuomba Allaah
azikubali ibada zetu na toba zetu. Allaah Ampe rehma Mtume
wetu Muhammad.
|