TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 »  Sira  
ALIVYOUSIMAMIA UJUMBE NA KUUFIKISHA KWA WATU

    Mtume (SAW) ameifanya kazi yake kwa ukamilifu

na ameufikisha ujumbe kwa watu  kama alivyotakiwa.

Wakati mwingine alikuwa akiwaendea watu maalum au huwaalika watu chakula, na mara nyengine hujitolea kuyaendea makabila mbali mbali huku akiwa na subira juu ya yale yanayomkuta, na kabila moja baada ya moja humkatalia. Wakati mwingine huwaita watu ili akutane nao au huwaendea pale walipo, na mara nyingine huwatuma walinganiaji katika sahaba zake, na  mara nyingine hutuma wajumbe kwa wafalme na ma gavana, mara nyingine hupigana Jihadi dhidi ya wale wanaowazuia watu kuilingania njia ya MwenyeziMungu.

Makafiri walipambana na uenezi huu pamoja na waenezaji kwa kila namna ya ukatili, nguvu na udhia.

Maqureish wakati mwingine walikuwa wakiwafanyia mzaha Mtume (SAW) na sahaba zake (RA), kisha ghafla wanawavamia baadhi ya Waislamu na kuwaunguza kwa moto, kuwauwa au kuwaadhibisha. Waliwapiga pande Waislamu na kuwazunguka wakiwemo katika nyumba za Abu Talib kwa muda wa miaka mitatu, hata iliwabidi Waislamu wale ngozi na miti. Udhia ukazidi na Masahaba wa Mtume(SAW) ikawabidi wahame na kukimbilia  Uhabeshi (Ethiopia) mara mbili, kisha wakahamia Madina.

Maqureish wakafanya njama ili wamuuwe Mtume wa MwenyeziMungu(SAW), lakini MwenyeziMugu akamwamrisha ahame ili aokoke  na hila zao.

Alikuwa akiwaelezea watu yote aliyotakiwa na MwenyeziMungu ayaeleze. Alitujulisha hata yale yaliyo na makatazo kwake yeye binafsi kutoka kwa MwenyeziMungu:

Mfano wa kauli ya MwenyeziMungu:

"Alikunja (Mtume ) paji na akageuza uso.

Kwa sababu alimjia kipofu.

Na nini kilichokujulisha (ya kuwa huyo Sahaba pofu hahitaji mawaidha mapya?)  Labda yeye atatakasika (kwa kusikia mawaidha mapya).

Au atakumbuka (aliyoyasahau). Ukukmbusho huo upate kumfaa.

Ama ajionaye hana haja (ya dini).

Wewe ndie unayemshughulikia?

Na si juu yako kama hakutakasika.

lakini anayekukimbilia.

Naye anaogopa.

Wewe unampuuza (Usifanye hivyo)".

(Abasa -1-10).

Aliambiwa haya kwa sababu Mtume(SAW) alipokuwa akiwalingania baadhi ya viongozi wa makafiri alijiwa na kipofu Mwislamu aitwae Ibn Ummi Maktoum akimuuliza masuali, na Mtume (SAW) alichukizwa kwa kuulizwa masuali wakati alipokuwa akijaribu kuwasilimisha wakubwa wa makabila ambao wangelisilimu wao pamoja na wafuasi wao ingepatikana kheri kwa Waislamu.

Mtume (SAW) hakumfanyia lolote la zaidi kipofu huyo isipokuwa alikunja uso wake tu. Na Ibn Ummi Maktoum kwa vile ni kipofu, hawezi kuuona uso wa Mtume (SAW) ulokunjwa na kwa hivyo hakuudhika.

Lakini MwenyeziMungu akamteremshia Mtume(SAW) makatazo, na akayafikisha makatazo hayo kama yalivyoteremshwa.

Lengo la Mtume (SAW) katika maisha yake yote lilikuwa ni kuyafikisha yale aliyoamrishwa na Mola wake bila ya kujali ukubwa wa taabu au vikwazo atakavyopambana navyo.

Katika Hijja yake ya mwisho (Hijjatul Wadaa) aliwauliza Waislamu;

"Je! nimefikisha?"

Wakashuhudia kuwa amewafikishia kikamilifu dini ya MwenyeziMungu;

Kisha akasema:-

"MwenyeziMungu shuhudia".

Hakika ya hali yake ilivyokuwa katika kila nyanja ya maisha yake inashuhudia kuwa sifa kama hizi hawezi kuwa za mtu wa aina nyingine isipokuwa ni sifa za Mtume wa MwenyeziMungu (SAW) na mjumbe Wake.