TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 » Ramadhaan  

BAADA YA RAMADHAAN

SWAWM ZA SUNNAH NA UMUHIMU WAKE

Muhammad Baawazir

Ndugu Waislam, wakati tunaelekea kukaribia kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhaan, ambao umejaa fadhila nyingi na kheri zisizopatikana katika miezi kumi na moja iliyobaki,  kuna umuhimu mkubwa wa kuendeleza zoezi hili la Funga baada ya mwezi huu mtukufu hususan, na kwa mwaka mzima kwa ujumla Insha-Allah.

Swawm kwa ujumla na Swawm za Sunnah haswa ni jambo kubwa sana la kiibada. Na ni bora sana ieleweke ndugu zangu, kuwa Swawm si Ibada ifanyikayo katika mwezi wa Ramadhaan pekee, bali ni jambo ambalo linalofanyika mwaka mzima katika nyakati mbalimbali kama tutakavyoona katika makala haya.

Kama ilivyo katika Ibada ya Swalah, kuna Swalah za Sunnah au Rawaatib au Nawaafil, ambazo ndizo zitakazokuwa viraka siku ya kiyama wakati zile Swalah za Fardh zitakapopelea katika Mizani. Nazo Swawm za kujitolea au za Sunnah, ndizo zitakazomuongezea mja thawabu na ujira pamoja na ile Swawm yake ya Fardh ambayo ni Ramadhaan.

Hapa chini tutaziorodhesha Swawm za SUNNAH ambazo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   kazipendekeza kwetu tuzitekeleze:

1. SWAWM YA SIKU SITA ZA MWEZI WA SHAWWAAL

Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhaan na siku ya ‘Iyd ul Fitr. Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   anasema:

 ))  من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر))

   رواه مسلم و الترمذي و  ابن ماجه , أبو داود و أحمد.

((Atakayefunga mwezi wa Ramadhaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima)). Imepokewa na Maimaam Muslim, At Tirmidhy, Ibn Maajah, Abu Dawuud na Ahmad.

Maulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300+60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.

Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu.

2. SWAWM YA SIKU YA ‘ARAFAH (Kwa wale wasiokwenda kuhiji)

Imesimuliwa na Abu Qutaadah kuwa Mtume صلى الله عليه  

 صلى الله عليه وآله وسلم   alisema:

عنْ أَبي قتَادةَ رضِي اللَّه عَنْهُ ، قالَ : سئِل رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم

: عَنْ صَوْمِ يوْمِ عَرَفَةَ ؟ قال :(( … يكفِّرُ السَّنَةَ المَاضِيةَ وَالبَاقِيَةَ (( رواه مسلمٌ .

Imetoka kwa Abu Qataadah رضِي اللَّه عَنْهُ kwamba Aliulizwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhusu Swawm ya 'Arafah akasema ((Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka uliopo)) Muslim

3. SWAWM YA SIKU TATU KATIKA KILA MWEZI ’AYAAMUL BIYDH’

Imesimuliwa na Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  alisema:

))"من صام ثلاثة أيام من كل شهر فذلك صوم الدهر فأنزل الله عز وجل تصديق ذلك في كتابه { من جاء بالحسنة فله عشر أمثالها } فاليوم بعشرة أيام))  رواه الترمذي  قال الشيخ الألباني : صحيح

((Yeyote atakayefunga kila mwezi siku tatu,ni sawa amefunga mwaka mzima, kisha Mwenyeezi Mungu akashusha Aya ithibitishayo maneno ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  isemayo: {{Atakayetenda jambo zuri basi malipo yake ni mara kumi mfano wake}}. Siku moja kwa malipo ya siku kumi!)) Imepokewa At Tirmidhy na kasema Sheikh Albaniy kuwa ni Sahihi.

Ukiitazama hadithi hii, utakuta makusudio yaliyotajwa kuwa malipo ya Funga hiyo ya siku tatu za kila mwezi, ni sawa na ya mwaka mzima, ni kuwa, ukipiga hesabu ya hizo siku tatu za kila mwezi, mara miezi kumi na mbili ya mwaka, ni sawa na siku 36. Na siku hizo 36 mara 10 ambazo ndizo malipo ya kila siku kwa mara kumi, basi utapata jumla ya siku 360 ambazo ni takriban idadi ya mwaka mzima wa Kiislam. Fadhila zilizoje na Ujira mrahisi kiasi gani wa kuuchuma ndugu watukufu!

Masiku haya matatu huitwa Masiku Meupe ‘‘Ayaam ul Biydh’’,kwa ushahidi (mashiko) yafuatayo:

Abu Dharr Al Ghifaari anasimulia kuwa Mtume 

 صلى الله عليه وآله وسلم alimwambia:

)) "يا أبا ذر إذا صمت من الشهر ثلاثة أيام فصم ثلاث عشرة وأربع عشرة

 وخمس عشرة)) رواه الترمذي   قال الشيخ الألباني : حسن صحيح  

((Ee Abu Dharr! Endapo utafunga siku tatu za kila mwezi, basi funga siku ya 13, ya 14, na ya 15)) Hizi huitwa ‘Ayaam ul Biydh’ [Masiku Meupe]. Imepokewa na At Tirmidhy na kasema Sheikh Albaaniy kuwa ni Sahihi..

         4.     SWAWM YA JUMATATU NA ALKHAMIYS

عن أبي هريرة  رضي الله عنه قال: كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصوم

الإثنين والخميس وعندما سئل قال: (( تُعْرَضُ الْأَعْمَالُ يَوْمَ ‏ ‏الِاثْنَيْنِ وَالْخَمِيسِ فَأُحِبُّ

 أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ }))  رواه الترمذي وقال حديث حسن

Abu Hurayrah رضي الله عنه anasimulia kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga Jumatatu na Alkhamiys. Alipoulizwa sababu ya Swawm katika siku hizo, akajibu: ((Matendo ya Wanaadam huwekwa mbele ya Mwenyeezi Mungu kila siku ya Jumatatu na Alkhamiy, nami napenda matendo yangu yawekwe mbele ya Allaah nikiwa nimefunga)). Imepokewa At-Tirmidhy na kasema Hadiyth Hassan

    5.     SWAWM YA SIKU YA TASU’AA NA ‘ASHURAA

Hizi ni Swawm za siku ya tisa na ya kumi ya mwezi wa Muharram (Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislam). Hizi ni Swawm kwa kumbukumbu na kumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa kumuokoa Nabii Muusa a.s. pamoja na watu wake, kutokana na Firauni na jeshi lake!

6.     SWAWM NYINGINEZO

Swawm katika mwezi wa Muharram zina fadhila nyingi kama Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    alivyomweleza Abu Hurayrah.. Pia Swawm katika mwezi wa Sha’aban, ambapo Bi ‘Aishah رضي الله عنها anasema kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akikithirisha sana kufunga.

 

NIA

Swawm kama amali zingine, ni lazima kuwepo na Nia ndani yake. Nia katika Swawm za Sunnah ni tofauti na Nia katika Swawm ya mwezi wa Ramadhaan, Mwezi wa Ramadhaan Mtu anatakiwa anuie kabla ya alfajiri. Lakini katika Swawm za Sunnah, Nia Mtu anaweza kunuia wakati wowote, hata mchana wa Swawm maadam hajala au hajafanya  chochote kiharibishacho Swawm toka alfajiri. Ushahidi wa jambo hili ni maelezo ya

 Bi ‘Aishah  رضي الله عنها aliposimulia kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwajia siku moja na kuwaauliza je, mna chakula chochote hapa nyumbani? Tukasema:Hakuna!! Akawaambia kuwa: Basi Nafunga!! Na siku nyingine alikuja akiwa amefunga (Swawm ya Sunnah), na sisi tulikuwa tumepewa zawadi ya ‘Hais’ (aina ya chakula alichokuwa akikipenda), nikamwambia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa tuna ‘Hais’ tumezawadiwa hapa, nimekubakishia je, unataka? Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : ‘Kisogeze hapa, ingawa nilikuwa nimeamka na Nia ya kufunga lakini nitafungua na kukila’. Kisha akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : ‘Mfano wa Swawm ya kujitolea (SUNNAH) ni sawa na Mtu ana pesa zake, kisha akawa na khiari ya  kuzitoa Sadaka au kutozitoa” Imepokewa na Imaam Ibn Maajah.

 

MUHIMU: Ni bora watu wafahamu kuwa Nia pahala pake ni moyoni, na si kutamka, ukishapitisha uamuzi wa kufunga, basi hiyo yatosha na sio kukariri maneno au kutafuta mtu akufundishe namna ya kuitamka Nia kiarabu au vinginevyo!!

 

WA ALLAHU A’ALAM