|
Mwenyezi
Mungu amemleta Mtume wake Muhammad (SAW) akiwa kama ni mletaji
habari njema na muonyaji ambaye hakuacha jambo lolote la kheri
isipokuwa ametujulisha nalo na kutuhimiza kulikimbilia, na
hakuacha jambo lolote la shari isipokuwa ametutahadharisha nalo.
Na kwa vile
umma huu ni umma wa mwisho, basi Mtume huyu mtukufu (SAW)
ametuletea kutoka kwa Mola wake dalili za kutosha zilizo wazi
zenye kutujulisha juu ya kukaribia kwa Siku ya Kiama na yeye
akatubainishia kwa ulimi wake tena kwa ufasaha kabisa juu ya
baadhi ya yatakayotokea katika mwisho wa zama na akatuhakikishia
kuwa yote hayo lazima yatatokea, haya yote yakiwa ni dalili juu
ya ukweli wa utume wake (SAW) utakayowafanya watu wajitayarishe
vizuri na Siku hiyo, siku ambayo mtu hatovuna isipokuwa kile
alichochuma, na hatokuwa na wakumlaumu isipokuwa nafsi yake.
Mwenyezi
Mungu anasema;
“Isije
ikasema nafsi (asije akasema mtu); “Eee majuto yangu kwa yale
niliyopunguza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa
miongoni mwa wanaoyafanyia mzaha (mambo ya dini)”.
Au ikasema;
“Kama Mwenyezi Mungu angeniongoa bila shaka ningekuwa miongoni
mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu”.
Au ikasema
ionapo adhabu; “Kama ningepata marejeo (ya kurejea tena duniani)
ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema”.
(Ataambiwa)’
“Kwa yakini! Bila shaka zilikujia Aya (dalili) zangu
ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni mwa wanaotakabari”.
Az Zumar –
56-59
Katika
kuzijuwa dalili hizo kisha kuziona zikitendeka hapa duniani
kunampatia mtu faida nyinigi sana zikiwemo zifuatazo;
·
Kuwa
na uhakika juu ya ukweli wa utume wake Muhammad (SAW).
·
Kujitayarisha vizuri na Siku ya Kiama. Kwani mtu kwa mfano
anapopewa habari juu ya meli inayokaribia kuwasili bandarini,
huingoja meli hiyo huku akiwa na wasi wasi mwingi, lakini
anapoisika sauti ya selo ya meli hiyo anakuwa na uhakika usio na
shaka kuwa meli sasa imekaribia kweli kuwasili.
Mfano huu
ni sawa na mtu aliyejulishwa juu ya dalili ya kukaribia kwa Siku
ya Kiama, kisha akaziona dalili hizo zikitendeka mbele ya macho
yake kama zilivyoelezwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Mtu
huyo anakuwa na uhakika usio na shaka wa kuwepo kwa siku ya
Kiama.
·
Kwa
ajili hiyo, kuzijuwa na kuziona dalili za kukaribia kwa Siku ya
Kiama kunaongeza pia yakini juu ya ukweli wa kukaribia kwa Siku
hiyo.
·
Kunamsaidia mtu kutoyumbishwa na masaibu, mitihani na machafuko
yanayotekea kila siku, kwani akirudi katika mafundisho ya Mtume
wa Mwenyezi Mungu (SAW) ataona kuwa yoote hayo yamekwishatajwa
kuwa yatakuja kutokea.
·
Kunamsaidia mtu aliyejisahau akawa anaikimbilia dunia,
anapoziona dalili hizo zikitokea kikweli humkumbusha mtu huyo
akawa anaifanyia kazi akhera yake badala ya kuikimbilia dunia.
Kutokana na
haya na mengi mengineyo, Mwenyezi Mungu akamfunulia Mtume wake
(SAW) baadhi ya dalili ya yale yatakayotokea kabla ya kuja kwa
Siku ya Kiama.
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa anapozungumza juu ya dalili za
kukaribia kwa Siku ya Kiama, mashavu yake yanageuka kuwa mekundu
huku akiipaza sauti yake juu kwa ghadhabu mfano wa amri jeshi
mwenye kulipa amri jeshi lake.
Alikuwa pia
akisema;
“Nimeletwa
baina yangu na Kiama kiasi kama hiki”, huku akiashiria kwa
kidole chake cha shahada na cha pili yake.
Zipo dalili
zinazoitwa ‘dalili ndogo’ na zipo pia ‘dalili kubwa’ za Siku ya
Kiama. Nyingi katika dalili ndogo zimekwisha tokea na kuonekana,
jambo lililowafanya Waislamu waongezeke imani na kumsadiki zaidi
Mtume wao (SAW), na zitakapoanza kuonekana dalili kubwa, basi
zitatunga na kufuatana moja baada ya nyingine mpaka Kiama
kitakaposimama. Lakini sisi tutazitaja hapa baadhi chache sana
za ‘dalili ndogo’ tu.
FITAN
Neno
‘Fitan’ ambalo ni wingi wa (plural ya) Fitna, maana yake ni
Mitihani. Lakini neno hili linaongezeka maana yake kila
linapozidi kutumika, kwani neno hili linaweza kumaanisha misiba,
madhambi, kufru, mauaji, kuchomwa moto nk.
Neno
‘Fitan’ pia linamaanisha vita vya wenyewe kwa wenyewe (civil
war)
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) ametujulisha juu ya Fitna nyingi sana
zitakazotokea baada yake zikiwa kama ni dalili ya kukaribia kwa
Siku ya Kiama. Fitna zitakazomfanya mtu asiweze kutambua ipi
haki na ipi batil. Fitna zitakazozitetemesha nyoyo na
kuiyumbisha imani hata mtu anaweza akaamka asubuhi akiwa ni
Muislamu na jioni yake akageuka kuwa kafiri, au anaweza kuamka
asubuhi akiwa kafiri na jioni yake akawa Muislamu.
Kila
inapotokea fitna, mtu hudhani kuwa hii ndiyo itakayoangamiza,
kisha humalizika na kutokea nyingine kubwa kuliko ile. Na hali
itaendelea hivyo mpaka kitakaposimama Kiama.
Anasema Abu
Musa Al Ashary (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Kinapokaribia Kiama zitatokea Fitna nyingi mfano wa vipande vya
usiku wenye kiza kizito, mtu ataamka ndani yake akiwa Muislamu
na jioni yake anakuwa kafiri, au anakuwa wakati wa jioni
Muislamu na asubuhi anakuwa kafiri. Aliyekaa katika mtihani huo
anakuwa bora kuliko aliyesimama na aliyesimama anakuwa bora
kuliko mwenye kutembea taratibu na mwenye kutembea anakuwa bora
kuliko anayekwenda mwendo wa kukazana”.
Imam Ahmed
na Ibni Majah na Al Hakim na wengineo.
Imetolewa
na Muslim pia kutoka kwa Abu Huraira (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (SAW) amesema;
“Kimbilieni
kufanya amali njema kabla ya kuja kwa Fitna mfano wa vipande vya
usiku wenye kiza kizito, mtu ndani yake anaamka akiwa Muislamu
na jioni yake anakuwa kafiri, au jioni anakuwa kafiri na asubuhi
anakuwa Muislamu. Mtu ndani ya fitna hizo anaiuza dini yake kwa
thamani ndogo ya dunia.”
Muslim
Na maana ya
neno ‘vipande vya usiku wenye kiza kizito’, ni ule ubaya wa
Fitna hizo utakaomfanya mtu achanganyikiwe asiweze kutambua
baina ya haki na batil.
Kutoka kwa
Ummu Salamah (RA) amesema kuwa usiku mmoja Mtume wa Mwenyezi
Mungu (SAW) aliamka akiwa na hofu nyingi huku akisema;
“Subhana
llah! Hazina ngapi aloteremsha Mwenyezi Mungu, na mitihani
mingapi aloteremsha Mwenyezi Mungu? Nani atakayewaamsha
waliolala vyumbani mwao (akimaanisha wake zake) huenda mtu akawa
amevaa duniani akenda uchi akhera”.
Maulamaa
wamelitafsiri neno ‘amevaa duniani akenda uchi akhera’, tafsiri
nyingi sana zikiwemo zifuatazo;
·
Mtu
tajiri mwenye nguo nyingi hapa duniani lakini hana amali njema
za kumsitiri huko akhera.
·
Wengine wakasema kuwa maana yake ni mtu mwenye kuvaa nguo
zisizomsitiri hapa duniani na huko akhera hatokuwa na cha
kumsitiri.
KUVUNJWA
KWA MLANGO
Nitaanza
kwa kutaja baadhi ya hadithi alizozungumzia ndani yake Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) fitna za mwanzo katika Uislamu, fitna
zilizotokea miaka michache baada ya kufariki kwake, mara baada
ya kuuliwa kwa Khalifa wa pili wa Waislamu Omar bin Khattab
(RA).
Katika
Bukhari na Muslim na Attirmidhiy kutoka kwa Hudhaifa (RA)
amesema kuwa Omar bin Khattab (RA) aliuliza siku moja;
“Yupi kati
yenu aliyehifadhi kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) juu ya
Fitna?”
Hudhaifa
akasema;
“Mimi
nimehifadhi kama alivyosema”.
Omar (RA)
akamwambia;
“Tuhadithie, kwani wewe ni jasiri”.
Hudhaifa
(RA) akasema;
“Fitna ya
mtu katika ahli yake (watu wa nyumba yake) na mali yake na
jirani zake zinaondoka kwa kusali na kutoa sadaka na kwa
kuamrisha mema na kukataza mabaya”.
Omar
akasema;
“La, mimi
sikusudii (fitna) hizi, bali zile zinazorusha mawimbi (makubwa)
kama mawimbi ya bahari’.
Akasema;
“Ewe Amiri
wa Waislamu! Wewe umeepukana nazo fitna hizo, kwani baina yako
na baina yake (fitna hizo) upo mlango uliofungwa”.
Omar
akauliza;
“Mlango huo
utafunguliwa au utavunjwa?”
Akasema;
“La, bali
utavunjwa”.
Omar (RA)
akasema;
“Kwa hivyo
hautofungika tena….”
Na katika
riwaya nyingine akasema;
“Kwa hivyo
hautofungika mpaka Siku ya Kiama?”
Wakamuuliza
(waliokuwa wakimsikiliza Hudhaifa baada ya kufa kwa Omar);
“Aliujuwa?”
Na katika
riwaya nyingine;
“Omar
alikuwa akiujuwa mlango huo?”
Hudhaifa
(RA) akawaambia;
“Naam kama
(anavyojuwa kuwa) usiku wa leo unakuja kabla ya usiku wa
kesho).”
Masruq bin
Al Ajda-a alipomuuliza Hudhaifa(RA);
“Nani
mlango huo”.
Akasema;
“(Mlango
huo ni) Omar.”
Kisha
Hudhaifa (RA) akawaambia;
“Mimi
nilimuhadithia Omar hadithi (hii) kama nilivyomsikia Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) bila makosa.”
Ikawa kama
alivyotujulisha Msemakweli Muhammad (SAW), kwani mlango huo
ulivunjwa mara baada ya kuuliwa Khalifa wa pili wa Waislamu Omar
bin Khattab (RA) na kuanzia hapo fitna zikafunguka na kuenea na
kukithiri, na fitna ya mwanzo ilikuwa kuuliwa kwa Khalifa wa
tatu wa Kiislamu Mwenye Nuru mbili Othman bin Affan (RA).
KUULIWA KWA
OTHMAN (RA)
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) aliwahi kumbashiria Othman bin Affan (RA)
kuwa atakumbwa na mtihani mkubwa.
Kisa
chenyewe ni kama ifuatavyo;
Katika
hadithii iliyosimuliwa na Bukhari, anasema Abu Musa Al Ash
ary(RA) kuwa siku moja alimuona Mtume(SAW) akielekea katika
kisima kilichozungushiwa ukuta.
Abu Musa Al
Asha-ary anasema;
“Nikasema;
Leo mimi nitakuwa mlinzi wa Mtume(SAW). Nikamuona Mtume(SAW)
akielekea kisimani, akakidhi haja yake kisha akakaa juu ya
kisima huku akining’iniza miguu yake.
Akaja
Abubakar akataka ruhusa ya kuingia ndani, nikamwambia; “Hapo
hapo ulipo, ngoja kwanza usiingie mpaka nikakuombee ruhusa kwa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)”.
Nikamwendea
Mtume(SAW) na kumwambia;
“Abubakar
anataka ruhusa ya kuingia”,
Akanambia;
“Mruhusu
aingie, na mbashirie Pepo”.
Nikafanya
hivyo, akaingia na kukaa juu ya kisima kuliani kwa Mtume(SAW) na
kuining’iniza miguu yake kama alivyofanya Mtume(SAW).
Mlango
ukagongwa tena. Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu.
Nikauliza;
“Nani?”
“Omar bin
Khattab”,
Nikamwambia;
“Hapo hapo
ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu
(SAW)”.
Mtume(SAW)
akanambia;
“Mruhusu
aingie, na mbashirie Pepo”.
Nikafanya
hivyo, na Omar naye akaingia na kukaa juu ya kisima kushotoni
kwa Mtume(SAW) na kuining’iniza miguu yake kama walivyofanya
wenzake.
Haujapita
muda mlango ukagongwa tena; Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu.
“Nani?”
“Othman bin
Affan”.
Nikamwambia; “Hapo hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe
Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)”.
Nilipomjulisha, Mtume (SAW) akanyamaza muda kidogo, kisha
akanambia;
“Mruhusu
aingie na mbashirie Pepo baada ya kupambana na mtihani mkubwa”.
Nilipomwambia hivyo, Othman akasema;
“Allahu l
Mustaan”, (na katika riwaya nyingine alisema ; “Tutakuwa na
subira Inshaallah”), kisha akaingia, lakini Othman hakupata pa
kukaa, akenda upande wa pili akakaa akiwa amekabiliana nao.
Anasema Abi
Musa(RA);
“Nikahisi
kama hivi ndivyo makaburi yao yatakavyokuwa, na nikatamani ndugu
yangu naye aje”.
Bukhari
Ingawaje
Omar bin Khattab (RA) aliuliwa kama alivyouliwa Othman (RA),
lakini Omar aliyeuliwa na kafiri anayeabudu moto wakati
akisalisha Sala ya Alfajiri hakupata misukosuko kama aliyopata
Othman (RA) kabla ya kuuliwa kwake.
Baada ya
kuuliwa Othman (RA) fitna zikawa nyingi, khitilafu zikaongezeka,
hata Masahaba (RA) walishiriki katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe.
MNAYAONA
NINAYOYAONA MIMI?
Siku moja
alipokuwa akisimamia ujenzi wa ngome katika mji wa Madina Mtume
wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliyekuwa akiyajuwa yote hayo kuwa
yatatokea, aliwauliza Masahaba wake;
“Mnaona
ninayoyaona?”
Masahaba
(RA) wakasema;
“Hatuoni
(kitu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) akasema;
“Mimi naona
mapigano mengi yakitokea baina ya nyumba zenu, wingi wa
nyumba
kubwa kubwa (zinazowakusanya watu wengi ndani yake).”
FITNA
ZITOKAZO UPANDE WA MASHARIKI
Fitna
nyingi zilizowakumba Waislamu zilitokea upande wa Mashariki ya
dunia, na fitna ya mwanzo iliyoleta mfarakano baina ya Waislamu
ilitokea upande huo wa Mashariki, jambo ambalo bila shaka
lilimfurahisha sana shetani.
Na haya
yanakubaliana na maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)
aliyetujulisha kuwa huko ndiko kwenye pembe ya Shetani.
Kutoka kwa
Ibni Omar (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)
amesema huku akiashiria upande wa Mashariki;
“Fitna ipo
huku, Fitna ipo huku, kutakapotokeza pembe ya shetani”.
Bukhari na
Muslim
Habari hizi
alizotujulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) zilianza kuonekana
tokea mwanzo wakati yalipotokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
jambo ambalo bila shaka yoyote lilimfurahisha sana shetani.
Anasema
Sheikh Yusuf bin Abdullah Al Wabil kuwa;
“Kutoka
upande wa mashariki Fitna nyingi sana zilitokea, kwani huko
ndiko yalipoanza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya
Waislamu, kutoka huko umekuja ukadiani, ukoministi. Tataar pia
wametokea huko katika karne ya saba ya Hijri wakaangamiza na
kueneza shari kubwa sana”.
“Hadi hii
leo”, anaendela kusema Sheikh Yusuf; “Fitna zinaendelea kutujia
kutokea upande huo wa Mashariki ya dunia na hata Yajuju wa
Majuju watatokea upande huo huo”.
KUPOTEA KWA
AMANA
Kutoka kwa
Abu Hurairah (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Uaminifu
utakapoondoka basi isubirini saa (kingojeeni Kiama)”.
Akaulizwa;
“Vipi
unapotea (uaminifu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”
Akasema;
“Mambo
yakiegemezwa kwa wasiostahiki, basi isubirini saa”.
Bukhari –
Kitabul Riqaaq
Mtume (SAW)
akatubainishia pia kuwa uaminifu utatoweka katika nyoyo na
kubaki athari yake tu.
Imepokelewa
kutoka kwa Hudhaifa (RA) kuwa amesema;
“Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) amenihadithia mambo mawili, na mojawapo
katika hayo nimekwishaliona likitokea na ninalisubiri la pili
(nilione pia). Amenihadithia kuwa uaminifu utatoweka.
Amenihadithia kuwa amana (ilipoteremshwa), iliteremshwa ndani ya
mizizi ya nyoyo za watu, kisha iilipoteremshwa Qurani wakaijuwa
zaidi, kisha wakaijuwa (vizuri zaidi) kupitia katika Sunnah
(Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)).
Kisha
akatuhadithia juu ya kunyanyuliwa (kupotea) kwa amana akasema;
“Mtu
analala usingizi huku amana inafutwa moyoni mwake na kubaki
athari yake tu, mfano wa doa lisilokuwa na rangi. Kisha analala
usingizi (mwingine) na amana inafutwa (‘tena’ - yaani hilo doa
lililobaki) kisha itabaki amana mfano wa alama (ya ngozi
iliyokunjika) inayobaki mkononi baada ya mtu kunyanyua kitu”.
(inayotoweka baada ya kupita muda mdogo).(au) maumivu yanayobaki
mguuni baada ya kukanyaga kijinga kidogo cha moto (pakafanya
lenge lenge kisha likakauka)”.
Kisha Mtume
(SAW) akasema;
“Kisha watu
watakuwa wanafanya biashara na hapana hata mmoja katika yao
atakayekuwa muaminifu, itafika hadi kusemwa; “Katika watu wa
kabila Fulaanii yupo mtu moja muaminifu. Na hata itafika hadi
watu watakuwa wakimsifia mtu huku wakisema; ‘Mwanamume kweli
huyu, mkarimu kweli huyu, ana akili kweli huyu’, (atapewa sifa
zote hizo) wakati mtu huyo hata imani (wala uaminifu) hata yenye
uzito wa hardali ”.
Hudhaifa
(RA) akaendela kusema;
“Nimekwishaiona zama ambayo ndani yake uaminifu baina ya watu
ulikuwepo. Na sikuwa nikijali ninafanya biashara na nani (kwa
sababu watu wote waaminifu), akiwa mtu huyo ni Muislamu basi
Uislamu wake utamfanya asiipoteze amana yake. Na kama mtu huyo
ni Mkristo au Myahudi, basi atakuwa anafanya kama anavyotakiwa
(kutonidhulumu haki yangu). Ama wakati huu wa leo, Uaminifu
umeondoka, na khiyana imedhihiri na sitofanya biashara isipokuwa
na Fulani au Fulani (tu)”.
Yaani
alikuwa akifanya biashara na baadhi ya watu wachache tu alokuwa
akiwaamini.
Hudhaifa
(RA) aliishi muda baada ya kuuliwa kwa Othman bin Affan (RA).
Bukhari na
Muslim
Anasema
Sheikh Yusuf Al Wabil aliyeandika kitabu cha ‘Ashraat al Saa-a’
kuwa;
“Miongoni
mwa dalili za kupotea kwa Amana ni kule kupewa ufalme, uongozi
au uhakimu watu wasiokuwa waadilifu wala waaminifu, kwani
viongozi wanapotengenea, raia nao hutengenea. Ama huko juu
kukiharibika, basi chini nako kutaharibika pia.
Na Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) amekwishatujulisha kuwa utafika wakati wa
hadaa, mambo yatakapokwenda kinyume. Wakati huo, muongo ndiye
atakayesadikiwa na mkweli atakadhibishwa, na muaminifu ataitwa
haini na haini ndiye atakayeaminiwa”.
Kubebeshwa
mzigo wa uongozi watu wasioijali dini yao, ni dalili ya watu
kutojali maamrisho ya dini yao, na dalili ya upungufu wa
maulamaa na kuongezeka kwa ujinga, na hizi pia ni katika dalili
za kukaribia kwa Kiama alizozitaja Mtume wa Mwenyezi Mungu
(SAW).
Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Katika
dalili za kukaribia kwa Kiama ni kupotea kwa elimu na kuongezeka
ujinga.’
Bukhari
KUSHINDANA
NA KUJISIFIA KATIKA KUIPAMBA MISIKITI
Imepokelewa
kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Katika
dalili za kukaribia kwa Kiama; ni watu kushindana na kujisifia
katika kuipamba misikiti”.
Annasai
Anasema
Bukhari;
“Amesema
Anas (RA) kuwa; ‘Watu wataipamba lakini hawendi kusali ndani
yake isipokuwa wachache”.
Omar bin
Khattab (RA) alikataza watu kuipamba sana misikiti kwa sababu
mapambo yanawababaisha watu ndani ya Sala zao, na alipokuwa
akisimamia utengenezaji wa msikiti wa Mtume (SAW) alikuwa
akiwaambia wajenzi;
“Wakingeni
watu na mvua na msitie rangi nyekundu wala manjano mkawababaisha
watu”.
Bukhari
“Mwenyezi
Mungu amrehemu Omar bin Khattab (RA)”, anasema Sheikh Yusuf
Wabil, “kwani watu hawakutoshelezeka na kuwakinga watu na mvua
wala hawakutoshelezeka na rangi za manjano na nyekundu, bali
misikiti siku hizi inapambwa na kujazwa nakhshi mfano wa nguo
inavyonakshiwa”.
MAUAJI
Kutoka kwa
Abu Hurairah (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)
amesema;
“Kiama
hakitosimama mpaka ‘Haraj’ ikithiri”.
Wakamuuliza;
“Ni nini
hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?’
Akasema;
“Mauaji,
mauaji!.”
Muslim
Na katika
riwaya nyingine iliyosimuliwa na Abu Musa (RA) kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Kabla ya
Kiama kusimama kutatokea ‘Haraj’.”
Wakamuuliza;
“Ni nini
hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”
Akasema;
“Mauaji”.
Wakamuuliza;
“Kuliko
tunavyouwa? Tunauwa (vitani) katika mwaka mmoja zaidi ya elfu
sabini?”
Akasema;
“Si kama
kuuwa kwenu washirikina, bali huko ni kuuwana nyinyi wenyewe kwa
wenyewe.”
Wakasema;
“Tutakuwa
na akili zetu siku hiyo?”
Akasema;
“Zitaondolewa akili za wengi wa watu wa zama hizo. Watakuwa na
wafuasi wengi kama vumbi, wengi wao watadhani kuwa wameshika
chochote (katika haki), lakini (ukweli ni kuwa) hawana
chochote”.
Imam Ahmed
– Ibni Majah
Kutoka kwa
Abu Hurairah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Naapa kwa
Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, haitotoweka dunia
mpaka iwajie watu siku ambayo ndani yake muuaji hatojuwa kwa
ajili gani ameuwa na wala aliyeuliwa kwa ajili gani ameuliwa.”
Akaulizwa;
“Yatakuwaje
hayo?”
Akasema;
“Al Haraj!
aliyeuwa na aliyeuliwa (wataingia) Motoni.”
Haya yote
yashatokea kweli katika zama zilizopita na tuanayaona yakitokea
katika zama zetu hizi pia, hasa baada ya kuvumbuliwa kwa silaha
zinazoangamiza.
Na katika
hadithi sahihi iliyomo katika Mustadrak ya Al Hakim, Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Umma wangu
ni umma utakaohurumiwa, hawatokuwa na adhabu huko Akhera, kwani
adhabu zao ni za dunia, mauaji na mashaka na mitetemeko”.
MTU
ATATAMANI KUFA
Imepokelewa
kuwa Abu Hurairah (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu
(SAW) amesema;
“Hakitosimama Kiama mpaka mtu atakapopita penye kaburi la mtu
akasema;
“Yareti
mimi ndiye ningelikuwa mahali pake”.
Bukhari
Na kutoka
kwa Abu Hurairah pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Naapa kwa
yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, dunia haitotoweka
mpaka mtu atakapopita penye kaburi akasimama na kusema; ‘Yareti
ningelikuwa mimi ndani ya kaburi hili’. Si kwa ajili ya dini,
bali kwa ajili ya mitihani.”
Bukhari
Amesema
Ibni Masaud (RA);
“Utakupitikieni wakati, mtu akiyakuta mauti yanauzwa, basi
atayanunua”.
Wanasema
maulamaa kuwa mambo kama haya si lazima yatokee katika kila
nchi, lakini yanaweza kutokea katika zama mbali mbali kutokana
na mitihani mizito mbali mbali, na mtu anapokumbwa na mitihani
hiyo atakapopita makaburini atahisi kama kwamba yule aliyelala
ndani mle ndiye aliyestarehe, ama yeye anajiona yumo katika
adhabu, misukosuko mashaka na mitihani mikubwa isiyomalizika.
KUPIGANA NA
WARUMI (WAKRISTO)
Kutoka kwa
Auf bin Malik Al Ashjaiy (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (SAW) amesema;
“Hesabu
mambo sita, lazima yatatokea kabla ya kusimama Kiama”,
(miongoni
mwa mambo sita hayo akasema; “Kisha vita vitasimamishwa baina
yenu na watu wa manjano (Wakristo), kisha watakufanyieni khiana,
watakujieni chini ya bendera themanini, chini ya kila bendera
(watu) elfu kumi na mbili.”
Bukhari
Siku moja
alikuja mtu kwa Abdillahi bin Masaud (RA) akamwambia;
“Ewe
Abdallah! Kiama kitasimama (karibu sana)”.
Abdillahi
bin Masaud (RA) aliyekuwa amekaa akiwa ameegemea, akakaa vizuri
kisha akamwambia;
“Hakika ya
Kiama hakitosimama mpaka kwanza mirathi isigawiwe na ngawira
isifurahiwe”.
Kisha
akasema huku akiashiria upande wa Sham (upande wa Mashariki);
“Maadui
watajikusanya kuwapiga vita Waislam, na Waislam watajikusanya
kwa ajili ya kupambana nao”.
Nikamuuliza;
“Warumi?
(Wakristo?)”
Akasema;
“Ndiyo, na
katika vita hivyo wengi watartaddi, na Waislamu watatayarisha
jeshi litakalokuwa tayari kufa lisilokubali kurudi nyuma bila
ushindi, watapigana vita mpaka usiku utakapoingia, kisha
watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao, kisha
jeshi litaangamia, kisha Waislamu watatanguliza jeshi (lingine)
litakalokuwa tayari kufa, watapigana vita mpaka wakati wa jioni,
kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao,
kisha litaangamia jeshi. Itakapoingia siku ya nne, Waislamu
waliobaki watakuja kuwasaidia, na Mwenyezi Mungu atawajaalia
ushindi uwe upande wao, watapigana vita visivyopata kuonekana
namna yake, hata ndege akipita juu yao, basi ataanguka akiwa
amekufa”.
Muslim
KUJA KWA
QAHTANIY
Imepokelewa
kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Hakitosimama Kiama mpaka kwanza aje mtu kutoka kabila la
Qahtaniy (kabila la watu wa Yemen), atawaongoza watu kwa bakora
(yaani atawaongoza na wataongoka vizuri na wote watampenda)”.
Imam Ahmed
– Bukhari na Muslim
MUHAMMAD
FARAJ SALEM AL SAIY
|