|
ASSALAMU ALAYKUM!
Ndugu yangu katika imaan:
Sifa njema
zote Anastahiki Allah Mola wa viumbe vyote na Swalah na
salamu zimfikie Mtume wetu na kipenzi chetu Muhammad
(s.a.w.) na aali zake na sahaba zake wote.
Ama kwa hakika katika
mwezi wa Ramadhaan kuna fadhila nyingi ambazo mimi
nitazitaja kwa uchache namuomba Allah Aniwafiqishe 'asaa
yawe na manufaa katika duniya na akhera Insha-Allahu
Aamiin.
1) NI MWEZI WA QUR'AN:
Kama Alivyosema Mwenyeezi
Mungu Mtukufu katika kitabu Chake:
"Mwezi wa
Ramadhani ni mwezi ambao imeteremshwa Qur'an ili iwe uongozi
kwa watu na hoja na upambanuzi (Baina ya haki na batil)
Qur'an 2:185
Na imekua makusudio yake
nikuteremshwa Qur'an kutoka katika Lauhim-Mahfudh ilaa samai
dduniya (Kutoka Lawhim-Mahfuudh mpaka mbingu ya kwanza).
Vilevile kama ilivyo
pokewa na ibni 'Abbaas kuwa makusudiyo yake kwa hakika
kuteremshiwa Mtume (s.a.w.) Qur'an mwanzo ni katika mwezi wa
Ramadhani na vilevile Qur'an mwanzo wa kateremka ni usiku wa
Laylatul Qadir na Laylatul Qadir iko katika mwezi wa
Ramadhaan.
Hivyo basi ni juu yetu
kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana kusoma
Qur'an. Walikua Salaf Swaalih (Wema Waliotangulia)
wakikilinda kitabu cha Allah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi
yaliyokuwemo kwa mazingatiyo. Pia Tunaambiwa kuwa Sayyidnaa
Jibriil (a.s.) akimfundisha Mtume (s.a.w.) Qur'an katika
mwezi wa Ramadhaan, na alikuwa 'Uthmaan bin 'Afaan (r.a.)
kila siku akisoma Qur'an yote yaani anakhitimisha mara moja
kwa siku, kwa maana, msahafu mzima anausoma kwa siku moja.
Na walikuwa baadhi yao katika wema wakisoma Qur'an yote kwa
siku tatu, wengine kwa wiki moja na wengine kwa siku kumi.
Walikuwa wakisoma Qur'an ndani ya Swalah na nje ya Swalah.
Mwenyeezi Mungu
Atuwafiqishe mimi na wewe tuisome Qur'an na kwa mazingatiyo
khassa katika mwezi huu tufanye juhudi sana ili tuweze
kupata fadhila za mwezi huu mtukufu.
2) NI
MWEZI WA SUBIRA:
Subira
ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mcha Mungu na
mnyenyekevu kwa Allah. Na katika kufunga kunatakiwa subira
pale mtu anapo jizuilia kutokana na kutokula, kunywa,
matamanio na mengineyo. na imekua saumu ni nusu ya subira na
subira malipo yake ni pepo kama alivyosema Mwenyeezi Mungu
mtukufu:
"Kwa hakika
(Mwenyeezi Mungu) Atawapa wenye kusubiri malipo bila ya
hisabu"
Qur'an 39:10:
3) MILANGO
YA MOTO INAFUNGWA, MILANGO YA PEPO INAFUNGULIWA NA MASHETANI
WANAFUNGWA:
Kama ilivyokuja katika
hadithi iliyopokelewa na Maimamu wawili:
Mtume
(s.a.w.) amesema, "Pindi inapo kuja Ramadhaan inafunguliwa
milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na
masheytwaani wanafungwa kwa Minyororo"
(imesimuliwa
na Al-Bukhaariy na Muslim)
Kwa
hakika utaona katika mwezi huu watu wengi
wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu wanajaa misikitini
kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwasababu mashettaani
wamefungwa na sheytaani juu ya uasi wake lakini anauogopa
mwezi wa Ramadhaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio
mana wengi nyoyo zina badilika wanaswali na kujitahidi
kufanya kheri. Lakini ikimalizika Ramadhaan tu basi Swalah
imekwisha kama vile Allah yupo Ramadhaan tu. Huu ni msiba
ndugu zangu waislamu Allah Asitujaalie katika hao.
4) LAYLATUL
QADR:
Katika mwezi huu kuna siku
ya Laylatul Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama
Alivyosema Mwenyeezi Mungu:
" Huo ni usiku
wa hishima ni bora kuliko miezi elfu.
Huteremka Malaika na roho
(za viumbe watakatifu) katika (usiku) huo
kwa idhini ya
Mola kwa kila jambo.
Ni amani (usiku) huo mpaka
mapambazuko ya alfajiri"
Qur'an
97:3-5
Imehisabiwa
mtu atakapo fanya ibada katika usiku huo mmoja nikama
amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila
kubwa kabisa. Na katika Muwat'aa Imamu Maalik kwa isnadi
iliyotumwa amesema.
Mtume
(s.a.w.) ameona umri wa umma za mwanzo ni mrefu, na umri wa
umati wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul
Qadr uwe ni bora kuliko miezi
elfu.
(Muwattah1/321(Muhammad Fuad 'Abdul Baaqy)
Hakuna
siku tukufu na kubwa kama siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta
usiku huu katika kumi la mwisho kufanya ibada ili tupate
fadhila hizo. Ninamuomba Allah atuwezeshe kwa hilo AMIIN.
5) DUA NI ZENYE KUKUBALIWA:
Katika hadithi iliyopokewa
na imam Ahmad:
Kutoka kwa
Jaabir (r.a) kwa isnadi iliyo nzuri.
Mtume
(s.a.w.) Amesema "kila Muislamu dua zake ni zenye kukubaliwa
atapo muomba katika mwezi wa Ramadhaan"
Na imepokewa katika
hadithi kuwa du'aa ya mwenye kufunga pia ni yenye
kukubaliwa. Basi mtu ajipinde katika kumuelekea Allah
kumuomba mambo ya kheri ya dunia na akhera aombe pepo ya
Jannaatul Firdaus na alete maombi mengine Insha Allah
Mwenyeezi Mungu Atayapokea maombi yetu AMIIN.
Lamwisho ambalo nitakua
nimekamilisha maudhui yangu:
HAKIKA MWEZI HUU NI MWEZI WA KUTOA:
Na alikua Mtume (s.a.w.)
akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhaan.
Imepokewa na
tirmidh kutoka kwa Anas (r.a.)
Kasema Mtume (s.a.w.) "Bora ya kutoa sadaqa ni kutoa katika
mwezi wa Ramadhaan"
Na imepokewa
na Zaid bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia
'Umar bin Khattwaab (r.a.) anasema, "ametuamrisha Mtume
(s.a.w.) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo
nimemtangulia Abu Bakkar nimekwenda na nusu ya mali,
akasema Mtume (s.a.w.) kunambia umewabakishia nini watu
wako? nikasema nusu kama hii, na akaja Abu Bakkar na kila
mali yake Mtume (s.a.w.) akamuuliza umewabakishia nini watu
wako? Akasema nimewabakishia Mwenyeezi Mungu na Mtume wake.
Nikasema huyu Abu Bakkar hapitiki na kitu chochote abadan"
Kuonyesha wema
waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini
tofauti kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika
mambo ya kidunia.
Insha Allah Atujalie mema
tuyafuate na mabaya tuyawache na tushindane katika kila
kheri ili tuwe ni wenye kufuzu na kupata daraja ya juu ya
Pepo.
ALLAHUMMA AAMIIN.
|