`
TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 » Sunnah  

FADHILA ZA SWAWM

Imeandikwa na: Ukht Muznah  Faraj

Ndugu yangu katika imaan:

Sifa njema zote Anastahiki Allah (s.w.t.) Mola wa viumbe wote Mwingi wa Rehma na Mwingi wa Kusamehe na rehma na amani zimfikie kipenzi Chake Allah Mtume wetu Muhammad (S.A.W.) Jamaa na sahaba wake wote.

Amma Baad:

Ndugu yangu muislamu ama kwahakika umetufikia mwezi ulio mtukufu na wenye fadhila kubwa na mavuno kwa wenye mazingatiyo kwa hayo nao ni mwezi wa Ramadhan ambao Allah Ameufaradhisha kwa Waislam kwa kauli yake Jalla Wa 'Alaa Alipo sema:

"Enyi mlioamini mmefaradhishiwa (mmelazimishwa) kufunga (Saumu mwezi wa ramadhani) kama walivyofaradhishiwa kabla yenu ili mpate kumcha Allah. Qur'an 2-183

 

Na hili la kumcha Allah ndio lengo kabwa la ibada hii ya funga kwani ni ibada ya siri baina yako na Mola wako.  Na wengi wanaliona gumu jambo hili la kufunga wakati linafadhila kubwa kabisa wengi wanapitwa na fadhila za kufunga kwa kupenda kula na kunywa.  Majuto yatawajia pale watakapo kutana na Mola wao hali hawana kitu.

Na nisiku maalum, siku chache katika mwaka mzima zilizowekwa watu hawamuonei  haya Mwenyeezi Mungu wanakula mchana bila ya udhuru wowote wa kisheria.  Allah Anatwambia katika kitabu chake kitukufu:

"Siku chache tu (kufunga huko) Na atakaekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine. Qur'an 2-184

Amaa kwahakika tumeona umuhimu na wajibu wa kufunga. hivyo basi napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwafahamisha ndugu zangu katika imaan fadhila za kufunga namuomba Allah Aniwezeshe.

Miongoni mwa fadhila hizo ni:

1- Hakika ya funga inamuokoa mtu kutokana na moto

 kama ilvyopokewa na Imam Ahmad katika hadithi sahihi.

Kutoka kwa Jaabir (r.a) hakika ya Mtume (s.a.w) amesema: " saumu nikinga itamukoa mja kutokana na moto" (siku ya qiyama)

(imepokewa na tabraniy kutoka kwa othman bin abil aass)

Na katika hadithi iliopokewa na muttafaqun alayhi 

Kutoka kwa Abiy Saidi lkhudhriyy (r.a) hakika Mtume (s.a.w.) amesema: " Mwenye kufunga siku kwa ajili ya Allah Mwenyeez Mungu Atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa umbali wa miaka sabini"

Ndugu yangu muislam ikiwa unafunga siku moja Allah Atakuokoa na moto wa jahannam je, Ukifunga ramadhani yote! hakika hii ni fadhila kubwa.

Na fadhila hizi zinaingia katika funga za lazima yaani fardhi na Sunnah. 

2- Saumu ni kinga kutokana na matamanio:

Imekuja katika hadithi.

Kutoka kwa Ibni Masoud (r.a) amesema Mtume (s.a.w.) "Enyi kundi la vijana miongoni mwenu atakaekuwa na uwezo wa kuowa basi na aowe (kufanya hivyo) kutampelekea kuinamisha macho yake na kuhifadhi tupu yake. Ikiwa hana uwezo wa kuowa basi na afunge kwani hiyo ni kinga kwake" (hadithun muttafaqun alayhi)

Hakika vijana wengi wanashtakia kutokana na matamanio khasa katika zama zetu hizi za wanawake wanavyotembea wazi katika masoko kwenye magazeti wanajitoa katika matangazo katika televisheni hii ndio sababu kubwa inayo leta athari ya uchafu na ufisadi mkubwa katika ardhi.  Allah Atuhifadhi! Na kwa sababu hiyo Mtume (s.a.w.) akawanasihi vijana ikiwa mtu hana uwezo wa kuowa basi na afunge.

3- Hakika saumu ni njia ya kumpelekea mtu peponi:

Kutoka kwa Abiy Umamah (r.a) amesema kumwambia Mtume (s.a.w.) "Ewe Mtume wa Allah Niamrishe mimi jambo litakalonifaa mbele ya Allah. "akasema Mtume (s.a.w.) Ni juu yako kufunga kwa hakika hakuna mfano wake" (sunanu nnisaai)

Akabainisha alayhi ssalatu wassalam hakuna kitu kitakachomkurubisha mja kwa Allah, na kumuweka mbali na adhabu kama kufunga. Bali ametupa khabari Mtume (s.a.w.) katika pepo kuna mlango khassah wa wenye kufunga.

Kutoka kwa Sahal bin Sa'ad (r.a) hakika Mtume (s.a.w.) amesema "Hakika katika pepo kuna mlango unaitwa Rayyaan, wataingia humo siku ya qiyama wenye kufunga tu. hatoingia yeyote mwingine, utasema wako wapi wenye kufunga?  Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwingine, wakisha kuingia utafugwa, basi hatoingia mwengine" (imepokewa na Bukhar)

Na umepewa jina hilo inanasibiana na sifa ya saumu ambayo inampata mtu kiu kutokana na athari ya kufunga.  Mara nyingi mtu anapofunga  hatamani chakula kama anavyotamani maji.

4- Hakika ya funga itamuombea mtu siku ya qiyama:

Kutoka kwa Abdullahi bin Amru bin Aassi (r.a) amesema Mtume (s.a.w.) " Funga na Qur'an zitamuombea mja siku ya qiyama, itasema funga ewe mola amejizuilia kutokana na chakula chake na matamanio yake wakati wa mchana, basi namuombea msamaha, na itasema Qur'an, amejizuilia kutokana na usingizi wake wakati wa usiku ninamuombea msamaha. akasema wamesamehewa. (imepokewa na Ahmad na Haakim biisnadis sahihi)

5- Hakika ya saumu ni kafara na msamaha kutokana na madhambi:

Kwahakika mema huondosha maovu na saumu ni katika jambo jema sana. Na Amesema Allah (s.w.) "Hakika ya mema huyaondosha maovu"

Qur'an 11-114.

Na katika hadithi iliyopokewa na maimamu sita.

Kutoka kwa Hudhayfah (r.a.) amesema Mtume (s.a.w.) " Fitna ya mtu kwa mkewake (watu wake) mali yake na jirani yake itamfidiya kutokana na sala, funga na sadaqa"

Mara nyingi kunakua na upungufu ima katika haki za mkeo kwa njia ya maneno au kuudhi na upungufu mdogodogo na katika makosa ya haki za jirani iwe kwa matendo au qauli na katika kuitakasa mali.  Vyote hivyo hutakaswa na sala, funga na sadaqa.  Iwapo mtu atajilazimisha na haya basi atasamehewa madhambi yake madogo.

Na kutoka kwa Abiy Hurayrah (r.a.) hakika Mtume (s.a.w.) amesema "Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na akatarajia malipo atasamehewa madhambi yake aliyoyatanguliza"

Imaani ni kumuamini Allah na funga ukamkusudia Allah Aliyetukuka na ukataraji malipo ambayo Allah Ameyatolea ahadi kwa wenye kufunga.   Kwani kuna baadhi ya watu bado wanamshirikisha Mwenyeezi Mungu katika ibada Zake,  wafunga, wasali kwa ajili ya majini, ni makosa makubwa sana.

Na katika hadithi nyingine:

Kutoka kwa  Abiy Harayrah (r.a) amesema Mtume (s.a.w.)  " Sala tano, na Ijumaa mpaka Ijumaa, na Ramadhani mpaka Ramadhani, zitamfidia hizo baina yake madamu atakua ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa" (imepokewa na muslim)

Kufunga mwezi wa Ramadhani ni sababu ya kusamehewa madhambi ambayo umeyatanguliza katika kipindi cha mwaka mzima uliopita lakini basi imewekewa sharti nikwamba ujiepushe na madhambi makubwa kwani madhambi makubwa hayafutiki mpaka ulete tawbah na hili wamekubaliana wanavyuoni wote.  Na vilevile Allah Amesema katika kitabu chake kitukufu:

Ikiwa mtajiepusha na (madhambi) Makubwa yaliyo katazwa Atakufutieni (Mwenyeez Mungu) maovu yenu na Atakuingizeni katika maingizo matukufu.

Qur'an 4-31.

6- Hakika ya saumu ni sababu ya kupata furaha ya nyumba mbili:

Kama ilivyokuja katika hadithi iliyopokewa na muttafuqun alayhi.

Kutoka kwa Abiy Hurayrah (r.a) Amesema Mtume (s.a.w.) "Mwenye kufunga ana furaha mbili; furaha ya kwanza anapofungua na furaha ya pili atakapokutana na Mola wake".

Amma kwa hakika  katika furaha ya kwanza ni pale Allah Alipotuhalalishia wakati wa jioni kula na kunywa kwani ni vitu ambavyo tunavipenda kwa hivyo tukamuabudu Mwenyeezi Mungu kwa kujizuilia kula, kunywa na matamanio wakati wa mchana.

Amma furaha ya pili nipale Allah alipo tuwafiqisha kuitimiza saumu hadi jioni kwani mara nyingine unakua taabani mpaka ikifika jioni unamshukuru Allah Alhumdulillahi nimeifikisha saumu hadi jioni na nimeikamilisha ibada.

 

7- Hakika ya harufu ya mdomo wa mwenye kufunga mbele ya Allah ni nzuri kuliko harufu ya miski: 

Harufu ya mdomo ambayo inatoka ni kutokana na kutokula chakula.  Nayo ni harufu iwachukizayo watu lakini mbele ya Allah Anaipenda. Hadithi iliyopokelewa na muttafuqun alayhi:

Amesema Mtume (s.a.w.) "Naapa kwa yule ambae nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake; harufu ya mdomo wa mfungaji ni nzuri mbele ya Allah kuliko harufu ya miski".

Kwa dalili hii inafaa mtu kupiga msuaki wakati jua limeshachomoza bali ni jambo linalo pendeza sana katika kila hali unaweza ukasafisha mdomo wako kwa kupiga msuaki wakati wa sala, wakati wa udhu, wakati unapo amka kutoka usingizini na pindi unapoona mdomo wako umebadilika ladha unapiga msuaki maadamu utachunga kitu kisipenye katika koo ambacho itabatilisha saumu yako. Isiwe kwamba Allah anapenda harufu hiyo basi ikawa hupigi msuaki.  Hiyo harufu hata ukipiga msuaki Amesema Allah Anaipenda sana na itakuja kutokana na kutopita kitu tumboni.

 

Ninamuomba Mwenyeez Mungu aniwafiqishe mimi na ndugu zangu katika imaani ajalie yawe na manufaa na faida kwa wasomaji

INSHAALLAH.