|
بسم الله الرحمن الرحيم
الحمد لله رب العالمين و الصلا ة و السلا
م علي نبينا محمد وعلى آله وصحبه, و بعد:
UTANGULIZI.
Baada ya
kumshukuru Allah [s.w.t.] na kumtakia rehma na amani Mtume
[s.a.w.] pamoja na Ali zake na Maswahaba zake wote.
Basi kwa
hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu
(s.w.t) amejaalia
kwa waja wake miongo [misimu] ya kuzidisha ndani yake
matendo mema na Mwenyezi Mungu (s.w.t)
huzidisha
pia malipo ya matendo
hayo kwa waja
wake , na miongoni mwa miongo hiyo ni huu mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Basi katika
makala hii nitaelezea kwa ufupi juu ya funga na yale
yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na hukumu, fadhila na
adabu zake.
Ninamuomba
Allah [s.w.t.] awanufaishe
waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na
aturuzuku
ikh-laswi [kutaka radhi zake pekee] katika matendo yetu yote, amiiin.
Na kwake
pekee ndio kwenye mafanikio ya dunia na akhera.
Ndugu yenu
katika imani:
IBRAHIM
A.H.GHULAAM.
22 RAJABU
1426H,
SANA`A
YEMEN.
MAANA YA FUNGA
Neno swaumu
ambalo ni funga katika lugha ya kiswahili,
kilugha lina maana ya kujizuilia . Ama katika sheria funga
[swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu [s.w.t.] kwa kujizuilia
na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia kudhihiri alfajiri
[ya pili] mpaka kuchwa [kuzama] kwa jua na kwa kunuilia
kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu [s.w.t.].
HISTORIA YA
FUNGA
Kwa hakika
funga si ibada ngeni, bali ni ibada iliyofaradhishwa kwa
umati zilizotangulia na pia kufaradhishwa katika umati huu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{{Enyi
mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu] kama
walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate
kumcha Mungu}} (2:183).
Ama katika
umati huu wa Muhammad [s.a.w.] funga ilifaradhishwa katika
mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya hijrah (2H).
HUKUMU YA FUNGA.
Funga ya
mwezi wa Ramadhani ni nguzo katika nguzo za Uislamu, nayo ni
wajibu kwa dalili ya kitabu (Qur-an), Sunnah na
Ijmai
(makubaliano) ya wanavyuoni wote wa Kiislamu.
1:
Amesema Allah [s.w.t.]: {{Enyi
mlioamini mmelazimishwa
kufunga (saumu)
kama
walivyolazimishwa waliokuwa kabla
yenu ili mpate kumcha mungu. Siku chache tu ( kufunga
huko)...(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa
Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qurani
ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na
upambanuzi (wa baina ya haki na batili) Atakae kuwa
katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani)afunge.
…}(2:183-185) .
2: Na
imepokewa hadithi kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar (r.a)
amesema : Nimemsikia Mtume (s.a.w.) akisema: “Umejengwa
Uislamu juu ya nguzo tano; kushuhudia ya kwamba hakuna Mola
anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (s.w.t) na
kwamba hakika ya Muhammad (s.a.w) ni mtume wa Allah(s.w.t)
na usimamishaji Swalah na utoaji zakah na kuhiji katika
nyumba (tukufu) ya alkaaba na funga ya ramadhani. (Al
Bukhariy na
Muslim).
Na kuna
hadithi nyingine
nyingi
zinazojulisha wajibu huo, na wanavyuoni wote wamewafikiana
juu ya uwajibu huo.
INAE MUWAJIBIKIA
FUNGA YA RAMADHANI.
Funga ya
Ramadhani inamuwajibikia kila Muislamu, baleghe, mwenye
akili, alie katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye siha (afya-
asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga (kama
hedhi na nifasi kwa wanawake).
*Na
inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao
wanapofikia umri wa miaka saba(7) na kuwalazimisha hadi
ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi(10), na hili
inabidi pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.
NYUDHURU ZA
KUFUNGA
Nyudhuru za
kuacha kufunga zinatofautiana na kila udhuru una hukumu yake,
na hapa nitazielezea
nyudhuru hizo kwa ufupi.
1- Hedhi (damu
ya mwezi) na nifasi (damu ya uzazi), huu ni udhuru ambao
unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa haramu
kwake funga na iwapo atafunga haitosihi
(haitokubaliwa)
funga yake, na ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.
2- Maradhi au
Safari. Na mwenye udhuru wa maradhi (yanayotibika kwa
kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga na
itawawajibikia kulipa. Amesema Allah (s.w.t.):{{Atakaye kuwa
katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye
kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku
alizoacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu
anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito..
.}} (2:185). Na
kama maradhi yatazidi au kumletea madhara iwapo atafunga
basi itakuwa lazima kwake kutokufunga.
*Ama safari
ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake kutokufunga wanachuoni
wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au kwa
mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa
takiribani kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa
msafiri anayesafiri kwa chombo cha aina yoyote
atakachosafiria,ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito
wowote.
3- Vizee (vikongwe)
na wenye maradhi sugu (yasiotarajiwa kupoa). Na haya mawili
iwapo yana msababishia madhara basi ni katika udhuru na
ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa
kumlisha masikini kibaba (mudi) cha chakula
(ambacho ni sawa na na
uzito wa gramu 600g takiribani)au
chakula
kinacho
mshibisha masikini mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.
4- Waja
wazito na wanyonyeshaji.
Nao ni katika
wenye ruhusa ya kutokufunga, na inawabidi kulipa siku
walizoshindwa kufunga kwa sababu ya udhuru huo.
5:Iliemzidia
njaa au kiu na akahofia kuangamia, huu pia ni katika udhuru
wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni kwamba:
yule
mwenye kuhofia kuangamia inakuwa kwake ni wajibu kufungua,
na itamuwajibikia kulipa kama mgonjwa.
NGUZO ZA FUNGA
1- Nia nayo
ni kukusudia kufunga usiku wa kuamkia funga, kwa funga ya
faradhi.
2- Kujizuilia
na vyenye kufunguza (kufuturisha).
3- Muda wa
kufunga (mchana kuanzia alfajiri mpaka kutwa (kuzama) kwa
jua).
UNAVYOTHIBITI
KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI
1- Kwa
kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa shaabani.
2- Kwa
kuonekana mwezi mwandamo siku ya 29 ya mwezi wa Shaabani,
imepokewa hadithi na Abu Hurayrah (r.a.) kwamba Mtume (s.a.w.)
amesema: {Fungeni kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na
fungueni kwa kuonekana kwake}
(Al Bukhariy na Muslim).
*Na mwezi wa
kuingia Ramadhani inatosha kuonekana na Muislamu mmoja
mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima
uonekane na Waislamu waadilifu wawili au zaidi.
YANAYO BATILISHA
(KUHARIBU) FUNGA
1- Kula au
kunywa kwa kukusudia.
2- Kila
kinachoingia tumboni au kooni kwa kukusudia.
3- Kukutana
kimwili (kuingiliana) kati ya mume na mke.
4- Kujitoa
manii (mbegu za uzazi) au kusababisha kutokwa na manii (kwa
kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana au kupigana mabusu nakadhalika).
5-
Kujitapisha kwa makusudi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu
Hurayrah (r.a.) amesema: amesema Mtume (s.a.w):
{...na
mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa.}
(wameipokea
maimamu watano).
6- Kutokwa na
damu ya mwezi (hedhi) au damu ya uzazi (nifasi).
*Wakati wowote
yanapomtokea mwanamke mawili hayo funga yake ya siku hio
itakuwa imeharibika na itamlazimikia kuilipa siku hio baada
ya mwezi wa Ramadhani.
YASIO FUNGUZA
1- Kula au
kunywa kwa kusahau.Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah
amesema, amesema Mtume (s.a.w): {Mwenye kusahau nae amefunga,
basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake….}
( Al Bukhariy na
Muslim ).
2- Kusukutua
au kupandisha maji puani wakati wa udhu (bila ya
kubalighisha).
3- Kuoga au
kujiburudisha kwa kujimwagia maji katika kiwiliwili (hasa
katika maeneo yenye joto kali).
4- Kuonja
chakula kwa mpishi (kwa sharti ya kutokumeza alichokionja).
5- Kutokwa na
mbegu za uzazi (manii)katika usingizi (ndoto) au bila ya
kukusudia.
6- Kuamka na
janaba.Imepokewa hadithi kutoka kwa Mamama `Aishah na Ummu
Salamah (r.a) kwamba Mtume (s.a.w) alikuwa akiamka na janaba
kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na
kufunga (Al Bukhariy na Muslim).
7- Kupiga
mswaki (wakati wowote).
8- Kuchoma
sindano ya kawaida ya tiba.
9- Kung`oa
jino na mfano wake.
10- Mwanamke
kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au nifasi.
ADABU ZA FUNGA
BAADHI
YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI
1- Kula daku.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas ibn Maalik (r.a) amesema:
amesema Mtume (s.a.w): {Kuleni
daku kwani hakika chakula cha daku kina baraka ndani yake}
(Al Bukhariy na Muslim).
*Na
inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.
2-Kuharakisha
kufutari (mara tu likizama jua). Imepokewa hadithi kutoka
kwa Sahl ibn Saad (r.a),
Hakika
Mjumbe wa Mungu (s.a.w) amesema: {Watu watakuwa bado wapo
katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari}.( Al
Bukhariy na Muslim).
*Na inasuniwa
(kuanza) kufutari kwa tende au maji. Imepokewa
hadithi
kutoka kwa
Salmaan ibn`Aamir
(r.a) kutoka kwa Mtume (s.a.w.)amesema: {Anapofutari mmoja
wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi
na afutari kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho)
( Wameipokea
Maimamu watano).
*Na pia
inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati
wa kufutari,kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufutari
ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu
(s.w.t).
BAADHI YANAYOTAKIWA AYAKITHIRISHE
MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI
1- Kisimamo
cha usiku (Swalah ya tarawehe), amesema Mtume (s.a.w): {Mwenye
kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani (thabiti)
na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (s.w.t.)
husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake}. (Al
Bukhariy na Muslim).
*Na inafaa
kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu
watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia), amesema
Mtume (s.a.w): {Msivizuilie vijakazi vya Mwenyezi Mungu (wanawake)
(kuhudhuria ibada) katika misikiti ya Mungu}.(Al
Bukhariy na
Muslim).
Na
haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika
usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu
za kimsingi zinazo
kubalika kisheria, amesema Mtume(s.a.w): {wakiwaombeni
ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni}.
(Muslim).
2- Kuzidisha
kusoma Quran.
Mwezi wa
Ramadhani ni mwezi wa Quran na ndio mwezi ulioteremshwa
ndani yake Quran, Amesema Allah(s.w.t.):{{Hakika
tumeiteremsha (Qurani) katika laylatul-Qadr (usiku wenye
heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani).}} (97:1). Na
{{(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao
imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani…}} (2:185).
3- Sadaka.
Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi fadhila na
thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Amesema Ibn ‘Abbaas
(r.a): Alikuwa Mtume (s.a.w.) mkarimu (mtoaji) na alikuwa
mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhani wakati anapokutana
na Jibriyl (a.s.) (Al Bukhariy na Muslim).
*Na katika
sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni
kuwafuturisha waliofunga, amesema Mtume (s.a.w): {Mwenye
kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya
aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu
chochote}. (Ahmad na Annasaiy).
4- Kufanya
Umrah, amesema Mtume (s.a.w): {Umrah katika mwezi wa
Ramadhani una malipo sawa na Hijjah}. (Muslim).
5- Itikafu (nako
ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha
na ibada mbalimbali), inasuniwa kufanya itikafu
na
hasa katika
kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi
kutoka kwa Ibn ‘Umar (r.a) amesema: Alikuwa Mtume(s.a.w.)
akifanya itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa
Ramadhani.(Al Bukhariy na Muslim).
6- Kuutafuta
usiku wa cheo (laylatul-qadr), na zaidi katika kumi la
mwisho la Ramadhani, imepokewa hadithi kutoka kwa Mama
‘Aishah (r.a) amesema: Amesema Mtume (s.a.w): {Utafuteni
usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho za
Ramadhani} (Al
Bukhariy na Muslim)
Na amepokea
Abu Hurayrah (r.a) kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema: {Mwenye
kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani
thabiti na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (s.w.t)
husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo)}. (AlBukhariy
na Muslim).
7- Toba. Nako
ni kurudi kwa Allah (s.w.t) kutokana na makosa aliyoyatenda
mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia
kutokuyarudia tena makosa hayo).
*Tukumbuke
ya kwamba Mwanaadamu si mkamilifu daima yupo katika hatari
ya kufanya makosa, sawa makosa hayo ikiwa ni makosa
ambayo
ameyahisi au hakuyahisi wakati wa kuyafanya kwake, toba ndio
njia ya kujikosha na madhambi ya makosa hayo,na kipindi cha
mwezi wa Ramadhani ni fursa muhimu ya kutubia.
*
Ikiwa
katika makosa yake kuna haki za wanaadamu inamlazimu kuzirejesha
kwa wenyewe
haki hizo.
FADHILA ZA FUNGA
Zimepokewa
Hadithi nyingi sana zinazoelezea fadhila
za
funga ya Ramadhani, miongoni mwa hadithi hizo ni hadithi
zifuatazo:
1- Amesema
Mtume(s.a.w): {Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na
kutarajia malipo (toka kwa Allah (s.w.t)) husamehewa
madhambi aliyoyatanguliza}.
(Al Bukhariy na Muslim).
2- Na amesema
Mtume (s.a.w): {amesema Allah (s.w.t): Kila amali ya
mwanaadamu (aifanyayo) ni yake,
wema (mmoja)
hulipwa kwa mfano wake mara kumi mpaka mara mia saba,
isipokuwa funga, hakika ya funga ni Yangu mimi, na Mimi
najua namna gani Nimlipe kwa funga hiyo, ameacha matamanio
yake na chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu,
mfungaji ana furaha mbili, furaha wakati wa kufutari kwake
na furaha nyengine pale atapokukutana na Mola wake. Harufu
yakinywa cha mfungaji inapendeza zaidi kwa Mwenyezi
Mungu
kuliko harufu ya miski}. (Al
Bukhariy na Muslim).
YANAYOPASWA
KUJIEPUSHA NAYO MFUNGAJI.
1- Tabia
chafu na maneno maovu, kama kusengenya, kusema uongo, na
kadhalika.
2- Kuzidisha
usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu
fursa ya kufanya ibada zaidi.
3- Kupoteza
wakati mwingi katika michezo na maongezi yasiyo na faida, na
kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada mbali mbali.
4- Kuacha
kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa
kwa jua.
5- Kufanya
israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari.
6- Kufutari
kwa vyakula vyenye harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu
thaumu,vitunguu maji, doriani, na kadhalika kwa kuhofia
kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika kwa Swalah.
7-
Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na unyenyekevu.
YANAYOTAKIWA KWA
KUMALIZIKA RAMADHANI.
1- Kutoa
zakatul-fitri,nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamume,
mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).*Watoto
wadogo,Watumwa na pia Wanawake waliochini ya usimamizi wa
Wanaume itawalazimikia zakah hio wasimamizi wao, ama
Wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.
*Na
inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya Swalah ya iddi.
Imepokewa
hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (r.a) amesema: Amefaradhisha
Mtume (s.a.w.) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi
ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana),
mume na mke, mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha
(hiyo
zakah ya fitri)
itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi).
(Al Bukhariy na
Muslim).
*Na wajibu ni
kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji uliopo
(ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4
kg) takribani kwa nafaka kama mchele na mfano wake)
(au thamani yake kwa baadhi ya wanachuoni).
2- Takbir,
inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi
wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua
mpaka wakati wa Swalah ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti
kwa wanaume njiani, masokoni na hata majumbani.
3- Swalah ya
iddi, kwa wanaume na wanawake.
*Na inasuniwa
ifanyike katika viwanja, na hata akina mama walio katika
siku zao (hedhi) inasuniwa na wao wahudhurie ingawa wao
hawatoshiriki katika kuswali.
4- Na
inasuniwa kula tende
kwa idadi ya
(witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili
ya Swalah ya iddi al-fitri.
5- Pia
inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye
Swalah ya iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (r.a)
amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (s.a.w) inapokuwa siku ya
iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al
Bukhary).
6- Kuvaa
mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.
*Na
inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri
watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).
7- Na pia
inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani kufunga siku sita
katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali). Amesema Mtume (s.a.w):
{Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita
katika mwezi wa shawwali
(mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).(Muslim).
8- Na tukumbuke ya kwamba
siku hii ya iddi inakatazwa (ni haramu) kufunga ndani
yake. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al
khudriy (r.a):( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w)
amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri
na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh`ha)).(Al Bukhariy
na Muslim).
MWISHO.
Namalizia makala hii kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.t) alie niwezesha kufanikisha
lengo langu hili.
Na kisha natoa shukurani
zangu za dhati kwa wale wote waliochangia kwa njia moja au
nyengine kukamilika kwa makala hii.
Na ninamuomba Mwenyezi
Mungu (s.w.t) atupe kila la kheri hapa duniani na kesho
akhera. Amiin.
وصلى الله على نبينا محمد وعلى آ له وصحبه وسلم
.
*KILA MTU ANAYO
HAKI NA ANASHAJIISHWA KUSAMBAZA MAKALA HII KWA NJIA YEYOTE
ITAKAYO KUWA RAHISI KWAKE KWA SHARTI LA KUTO KUIFANYIA
MAREKEBISHO YEYOTE KABLA YA KUWASILIANA NA MTAYARISHAJI WA
MAKALA HII.
*UKIWA NA
MASWALI MAPENDEKEZO MAREKEBISHO AU AINA YEYOTE YA USHAURI,
WASILIANA NAMI KWA ANUANI IFUATAYO:
IBRAHIM
ALLY HAMAD GHULAAM
P.O BOX 5189
SANAA YEMEN.
SIMU NAMBARI:
BARUA PEPE:
ibralhamd2000@yahoo.com
|