|
UTANGULIZI:
Mwenyezi Mungu (SWT)
amesema:
“Sikuwaumba Majini na wanaadamu ila wapate kuniabudu”.
(Qur’an 51: 56)
Ibada
ni neno linalokusanya
mambo meengi. Ujumla wake ni kufungamana na kila
analolipenda na kuliridhia Mwenyezi Mungu na kuacha kila
alilolikataza Mwenyezi Mungu katika maneno na matendo.
Aya nyingi katika Qur’an
zinazozungumzia ibada zimeambatanishwa na neno
ikhlaaswi. Hebu turejee
aya zifuatazo kwa mifano michache:
v
“Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu Allah (SWT) kwa
kumtakasia dini…..”
Qur’an (98:5).
v
“Kwa yakini sisi tumekuteremshia kitabu hiki (Qur’an) kwa
haki, basi muabudu mwenyezi Mungu kwa kumfanya mola yeye tu………”
(Qur’an 39: 2-3).
Hii ni kusema kwamba ibada
yoyote ile ambayo itafanywa pasi na ikhlaaswi, basi hiyo
haitokubaliwa.
Mada yetu hii ya ikhlaaswi
tutaizungumzia katika sehemu sita kama ifuatavyo:
1.
Maana ya ikhlaaswi.
2.
Umuhimu wa ikhlaaswi.
3.
Matunda na faida ya ikhlaaswi.
4.
Mifano ya watu waliokuwa na ikhlaaswi.
5.
Madhara/hatari ya kukosa ikhlaaswi katika ibada.
6.
Jinsi ya kuipata ikhlaaswi katika amali (ibada) zetu.
MAANA YA IKHLAASWI
Maana ya ikhlaaswi
tunaweza kuiangalia katika mtazamo wa kilugha na kisheria.
Lugha: Maana ya
ikhlaaswi ni kitu safi au utakaso.
Sheria: Ni
kukusudia kwa kauli zako na matendo yako na ibada zako zote
kutaka radhi za Mwenyezi Mungu (SWT).
Ushahidi tunaupata katika
Qur’an 6: 162-163., Mwenyezi Mungu (SWT) anaposema:
“Sema: Hakika swala yangu, na ibada zangu (nyingine zote) ……ni
kwaajili ya Mwenyezi Mungu (SWT) mola wa viumbe vyote……..”
Mema tunayoyatenda na
maovu tunayoyaepuka iwe ni kwa ajili ya kutaka radhi za
Mwenyezi Mungu (SWT).
Mifano michache ifuatayo
ya ibada itatuwekea sawa nini tunakusudia tukisema ibada
inatakiwa kufanywa na ikhlaaswi:
1.
Swala:
Mwenyezi Mungu anasema
katika Qur’an 6: 162:
“Sema: Hakika swala yangu, na ibada zangu (nyingine zote) ……ni
kwaajili ya Mwenyezi Mungu (SWT) mola wa viumbe vyote……..”
Tunaona katika sehemu
nyingine Mwenyezi Mungu amewaonya wale wenye kuswali, si kwa
kutaka radhi zake, bali kwa kutaka kuonekana, pale aliposema:
“Basi adhabu itawashukia wanaosali, ambao wanapuuza sala zao,
ambao hufanya amali zao ili watu wawaone tu/riya”
(Qur’an 107: 4-6).
2.
Zaka na sadaka:
Itakuwa ni batili kama
sadaka au zaka itatolewa kwa ajili ya mtoaji kutaka
kuonekana kuwa ametoa.
Allah (SWT) anasema:
“Enyi mlioamini, msibatilishe sadaka zenu kwa masimbulizi na
udhia kama wale ambao hutoa mali zao kwaajili ya kutaka
kuonekana na watu…”
(Qur’an 2:264).
3.
Kutafuta elimu:
Aya ya ya kwanza kumshukia
mwanadamu imesisitiza umuhimu wa elimu.
“Soma kwa jina la Mola wako aliyekuumba.”
(Qur’an 96:1).
Tunaona kuwa aya hii zaidi
imesisitiza kuwa elimu lazima iwe ni kwa jina la Mola
aliyetuumba. Kinyume na hivi mtu hatopata malipo bali
ajiandalie makazi ya motoni. Mtume (SAW) anasema:
“Mwenye kutafuta elimu
kwa lengo la kutaka kuonekana kuwa amesoma au ili abishane
na wajinga, basi mtu huyo ataingizwa motoni na Mwenyezi
Mungu”
TIRMIDHIY.
Na katika riwaya nyingine
amesema Mtume (SAW):
“Mwenye kutafuta elimu
kwa lengo la kutaka kuonekana kuwa amesoma au ili abishane
na wajinga, basi mtu huyo ajiandalie makazi yake yake motoni.”
TIRMIDHIY.
Kwahiyo, ibada zetu zote
tunazozifanya ni lazima ziwe ni kwaajili ya Allah (SWT) tu,
vinginevyo hatutaambulia thawabu/malipo yoyote katika ibada
hizo.
Kwa mfano alikuja mtu
mmoja kwa mtume (SAW) akasema: “Mimi ninatoa sadaka kwaajili
ya kutaka radhi za Allah na vilevile ninapenda niambiwe
mkarimu.” Palepale
Allah akateremsha aya isemayo:
“….
anaependa kukutana na (jaza ya) mola wake (siku ya kiama)
basi na afanye (atende) vitendo vizuri, na wala
asimshirikishe kwa ibada ya Mola wake na (mtu) yeyote.”
(Qur’an 18:110).
UMUHIMU WA IKHLAASWI
Yafuatayo ni maelezo kwa
ufupi juu ya umuhimu wa ikhlaaswi katika maisha yetu ya kila
siku:
i-
Ni sharti la kukubaliwa amali zetu:
Ili amali ikubaliwe,
lazima ifanywe kwa nia
ya kutaka radhi
za Allah
(SWT).
Mtume (SAW) anasema:
“Hakika amali zote
huzingatiwa kwa nia
na hakika kila mtu atalipwa kulingana na nia aliyonuia. Yule
ambaye amehama (kutoka Maka kwenda Madina)kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu na mtume wake, basi hijra
yake hiyo (ndiyo hasa) kwa
ajili ya Allah na Mtume, Na ambaye amehama kwa malengo ya
kidunia au kwaajili ya mwanamke anayetaka kumuoa, basi
hijra (kuhama)
kwake huko ni kwaajili ya hilo alilohamia.”
BUKHARI & MUSLIM.
ii-
Dawa ya unafiki:
Ibada zetu zikifanywa kwa
ikhlaaswi zinatupelekea kuondokana na unafiki.
Miongoni mwa dalili za
wanafiki zilizotajwa katika Qur’an ni (4: 142):
-
Kusimama katika swala kivivu,
-
kuzionyesha swala zetu, na
-
kutomtaja Mwenyezi Mungu.
Basi aya zifuatazo zinatoa
maelezo ni namna gani mtu atatoka katika unafiki kwa kuwa na
ikhlaaswi katika ibada zake:
“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa la
moto na wala hawatopata wa kuwanusuru. Isipokuwa wale
waliotubia, na wakafanya vitendo vizuri, na wakashikamana na
dini ya Mwenyezi Mungu, na wakawa na
ikhlaaswi
katika dini yao kwa ajili ya Allah (SWT) basi hao watakuwa
pamoja na waumini (Watatoka katika unafiki)….”
Qur’an 4:145-146.
iii-
Dawa ya Riya:
Riya maana yake ni kutaka
kila amali yako ya kheri ionekane au ijulikane. Kwa hivyo,
ili uondokane na riya, basi ni lazima ufanye ibada zako kwa
ikhlaaswi.
MATUNDA/FAIDA ZA IKHLAASWI
Miongoni mwa faida za
ikhlaswi ni:
i-
Kuweza kumshinda shetani.
ii-
Kuweza kutenda mema na kuyaepuka maovu mahali popote
pasi na kumuogopa mtu yeyote au kutaraji malipo kutoka kwa
mtu yeyote.
iii-
Amali iliyofanywa kwa ikhlaaswi inaweza kumnusuru mtu
wakati anapofikwa na matatizo.
Kwa ufafanuzi zaidi wa
faida hizo hapo juu tunanukuu kisa kifuatacho kutoka katika
hadithi ya mtume iliyopo katika kitabu cha Imamu Bukhari na
Muslimu. Hadithi hii inapatikana pia katika kitabu cha
riyadhu swalihina,
katika mada ya ikhlaswi.
Ni hadithi No. 12.
Ifuatilize hadithi hii kwa makini:
Imepokelewa kutoka kwa Abdallah bin Umar bin al-Khattab
(radhi za Allah ziwe juu yake) akisema: Nimemsikia mtume
(SAW) akisema:
“Waliondoka watu watatu katika watu waliokuwepo kabla yenu
(masahaba), mpaka ukawaingilia usiku wakaingia katika pango
(ili wapate kulala). Jiwe likaanguka kutoka mlimani na
kuziba mlango wa lile pango”.
Watu hawa watatu wakawa hawana njia ya kutokea. Wakasema:
“Hakuna kitakacho tuokoa kutokana na hili jiwe isipokuwa ni
kumuomba Allah (SWT) kwa vitendo vvyetu vizuri (ambavyo
tumekwisha wahi fanya).”
Wa kwanza wao akasema: “ Eeeeh Mola wangu!, mimi nilikuwa na
wazee wangu wawili, watu wazima, nilikuwa nikiwapa maziwa
kabla ya kumpa yeyote katika watoto wangu, watumishi au
wangu au mtu yeyote wa nje. Siku moja nilikwenda mbali
kutafuta kuni, sikuweza kurudi (mapema) mpaka walipokuwa
wamelala. Nikakamua maziwa, na kama kawaida yangu nikaenda
kuwapelekea yale maziwa. Kwa bahati mbaya nikawakuta
wamelala. Nikachukia kuwaamsha, na pia sikupenda kumpa
mtuyeyote maziwa yale kabla yao. Watoto wangu walikuwa
wakilia kutokana na njaa chini ya miguu yangu, lakini
nilisubiri na bakuli la maziwa mpaka ilipoingia alfajiri.
Walipoamka alfajiri, nikawapa yale maziwa, wakanywa.
Eeeh Mola wangu wa
haki!, ikiwa mimi nilifanya hivyo kwaajili ya kutafuta radhi
zako, basi tupe faraja katika hili (jambo)”…… JIWE LOKASOGEA
LAKINI HAWAKUWEZA KUTOKA.
Wa pili wao akasema: “Eeeh Mola wangu wa haki!, hakika mimi
nilikuwa na binti wa baba yangu mdogo, ambaye alikuwa ni mtu
anayependeza sana kwangu. Nilikuwa nikitaka kufanya naye
mapenzi, lakini alikataa. Mpaka ikapita miaka akanijia na
shida yake, nikampa dinari 120 kwa sharti kuwa akubali
nimuingilie. Yule binti akakubali. Lakini nilipokuwa nimekaa
baina ya miguu yake (tayari kumuingilia) akasema: ‘mche
Mwenyezi Mungu, na wala usiivue pete isipokuwa kwa haki
yake.’
Nikaondoka na kumuacha yule mwanamke na hali ya kuwa bado
ninampenda sana. Na nikamwachia zile pesa ambazo nilimpa.
Eeeh Mola wangu wa
haki, ikiwa mimi nilifanya hivyo kwaajili ya kutafuta radhi
zako, basi tupe faraja kutokana na jambo hili tulilonalo.”
JIWE LIKASOGEA TENA KIDOGO, LAKINI BADO HAWAKUWEZA KUTOKA
KWA KUWA UWAZI ULIKUWA BADO NI MDOGO.
Na akasema yule wa tatu: “Eeh Mola wangu wa haki, hakika
mimi nilikuwa nimeajiri watu, na nikawapa ujira wao (baada
ya kumaliza kazi) isipokuwa mtu mmoja ambaye aliondoka bila
ya kuchukua mshahara wake. Nilimuendelezea kile kiasi cha
mshahara wake na kuwa mali nyingi.
Baada ya muda fulani yule mtu (aliyekuwa mwajiriwa) akanijia
na kutaka ujira wake alouacha siku za nyuma. Nikamwambia
kuwa kila alichokiona pale kilikuwa ni kutokana na ujira
wake ambao niliuendeleza. Hivyo achukue kila kitu (Ngamia,
ng’ombe, kondoo, mbuzi n.k.) Mtu yule alifikiri ninamtania.
Lakini nilipomuhakikishia kuwa nilikuwa ninasema kweli,
alichukua kila kilichokuwepo bila ya kuniachia chochote.
Eeeh Mola wangu wa
haki!, ikiwa mimi nilifanya hivi kuzitaka radhi zako, basi
tupe faraja katika jambo hili.” JIWE LIKAFUNGUKA WAKATOKA
KATIKA PANGO NA KWENDA ZAO.
MAELEZO:
Hadithi hii ina mafunzo
mengi sana, mojawapo ni kuwa ibada
au amali
inayofanywa kwa ikhlaaswi
inaweza kumuokoa mja anapopatwa na matatizo/janga.
MIFANO YA WATU WALOKUWA NA IKHLAASWI
Iko mifano mingi,
mwiongoni mwayo ni hii tutakayoielezea hapa chini:
Mfano wa kwanza ni wa
Khalid Bin Walid (R.A)
ambaye aliondolewa kwenye
uongozi wa jeshi na Umar Bin Khattab kabla ya fat-hu
(kukombolewa) Shaam (Syria). Baada ya kuondolewa Khalid Bin
Walid kwenye uongozi, Umar (R.A) alimteua Abuu Ubaida Aamir
Bin Jarrah kuwa kiongozi mpya wa jeshi.
Pamoja na kuondolewa
kwenye uongozi wa jeshi, Khalid alionekana kupigana kwa
nguvu zote katika kuikomboa Shaam. Baadhi ya maswahaba
wakamwambia ‘mbona bado uko mstari wa mbele, una pigana kama
kawaida ili hali wewe si kiongozi wa jeshi tena?’ Khalid
akawajibu: “ Ninataka kuikomboa Shaam kwa ajili ya
Allah (SWT) na wala siyo kwaajili ya Ummar Bin Khattab.
Hii ndiyo ikhlaaswi.
Pamoja na kuwa Khalid Bin Walid aliuzuliwa u amiri jeshi,
bado alikuwa katika mstari wa mbele ili kuikomboa Shaam
kwaajili ya kuzitafuta radhi za Mwenyezi Mungu (SWT) na wala
siyo kwa ajili ya kumridhisha Umar, au kwa sababu alikuwa ni
kiongozi, au Imam.
Mfano wa pili tunaupata
katika vita nyingine ambayo walipata kupigana waislamu.
Katika vita hivi walikutana na ngome ngumu ya makafiri.
Takriban miezi saba (7) waislamu walishindwa kuingia katika
ngome hii.
Mmoja kati ya waislamu
alikuwa akiamka usiku na kuchimba shimo chini kwa chini (kwa
siri) na ifikapo asubuhi, alikuwa akiliziba na kujiunga na
wenzake. Baada ya muda kadhaa ulipatikana mwanya wa
kuwawezesha waislamu kuingia katika ngome ya makafiri.
Alipofanikiwa kupata mwanya huu, aliingia kwenye ngome ya
makafiri na kupiga takbir
ya nguvu kama ishara ya
kuwajulisha waislamu kuwa ngome inaingilika. Waislamu
waliivamia ngome hii lakini hakujulikana ni nani aliyechimba
lile shimo.
Kiongozi wa jeshi la
waislamu, kwa furaha kubwa alisimama na kutangaza kuwa
aliyechimba lile shimo ajitokeze ili apate kumlipa. Siku
tatu zilipita baada ya tangazo hili hakuna aliyejitokeza.
Siku ya nne (4) kiongozi yule alitoa tangazo jingine kuwa
kujitokeza kwa aliyechimba shimo lile ni wajibu, kwani
lasivyo atakuwa amemuasi kiongozi wa jeshi.
Hapa ndipo yule
aliyechimba shimbo akajitokeza mbele ya kiongozi wa jeshi,
lakini akiwa amejifunga kitambaa usoni na kusema:
“Mimi nimetumwa na aliyechimba shimo, lakini kabla
hajajitaja anakupa masharti matatu:
1-
Usimlipe kwa lile alilolifanya,
2-
Usilitaje jina lake kwa amiir Muuminina, na
3-
Usimuulize jina lake.”
Alipomaliza kauli hii
alikimbia huyu bwana na akajifungua kitambaa, lakini
kiongozi wa jeshi hakufanikiwa kumuona na kumtambua kuwa ni
nani.
Baada ya tukio hili, yule
kiongozi wa jeshi alikuwa kila akiingia vitani anaomba dua
hii: “Eeeh Mola! Nakuomba unifufue na yule
aliyechimba shimo, mimi pamoja na Mtume (SAW).”
Na mfano wa tatu ni wa
Abubakar, ambaye alikuwa akiwaacha huru watumwa kwaajili ya
kutafuta radhi za alla (SWT). Tukio hili limetajwa katika
Qur’an tukufu (92: 19-20):
“Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe
anamlipa. Isipokuwa (anafanya haya) kwa kutaka radhi ya Mola
wake Mtukufu”
MADHARA/HATARI YA KUKOSA IKHLAASWI
KATIKA IBADA
Kukosekana kwa ikhlaaswi
katika ibada zetu husababisha madhara mengi sana. Tutayataja
machache hapa chini:
i-
Hubatilisha amali za mja na kumfanya asipate chochote
isipokuwa ghadhabu za Allah (SWT). Allah (SWT) anasema:
“Enyi mlioamini, msibatilishe sadaka zenu kwa masimbulizi na
udhia kama wale ambao hutoa mali zao kwaajili ya kutaka
kuonekana na watu…”
Qur’an 2: 264.
Pia Allah
(SWT) anasema:
“Ole wao wenye kuswali ambao huswali kwa ajili ya
kuwaonyesha watu swala zao.”
Qur’an 107: 4-6.
ii-
Kumtia mtu katika Riya, kisha humtia katika shirki.
Mtume (SAW) anasema:
“Ninachokiogopea sana
kwa umma wangu ni shirki ndogo”, wakamuuliza (maswahaba):”
Shirki ndogo ni ipi?” Akasema (Mtume): “Ni Riya.”
Na katika hadithi
nyingine, Mtume (SAW) anasema:
“Mwenye kuswali
kwaajili ya kutaka kuonekana atakuwa amefanya shirki, na
mwenye kufunga kwaajili ya kutaka kuonekana atakuwa amefanya
shirki, na mwenye kutoa sadaka kwaajili ya kutaka kuonekana
atakuwa amefanya shirki.”
IMAM AHMAD.
iii-
Kwa kuwa ikhlaaswi ndiyo roho ya ibada (amali), ibada
yoyote isiyo na ikhlaaswi haiwezi kudumu.
Mifano:
a)
Kuna Binti ambaye alitaka kuolewa na bwana mmoja ili
apate makaratasi ya kumuwezesha kuishi katika nchi moja ya
ughaibuni. Baada ya kuolewa na kupata hayo
makaratasi, alimfanyia
vituko mumewe huyo mpaka ndoa yao ikavunjika.
b)
Kuvunjika na kusambaratika kwa taasisi nyingi za
kiislamu. Hii ni kwasababu hazikuasisiwa chini ya misingi ya
ikhlaaswi, bali kwaajili ya malengo ya kidunia tu.
iv-
Aliyefanya ibada kwaajili ya kutaka kuonekana
ataingia motoni hata kama alikufa katika jihadi, au alisoma
na kufundisha Qur’an au alitoa sadka na zaka.
Ushahidi wa hili tunaupata
katika hadithi ndefu ya Mtume (SAW) ambayo inapatikana
katika kitabu cha Imamu MUSLIM:
Mtume (SAW) anasema:
“Katika watu wa mwanzo watakaohukumiwa siku ya kiama ni mtu
ambaye alikufa katika jihadi. Ataletwa mbele ya Allah (SWT)
kisha atafahamishwa neema aliyopewa, ataifahamu. Kisha Allah
(SWT) atamuuliza:
Allah :‘umeifanyia
nini neema hiyo?’
Atajibu :‘Nimepigana
kwaajili yako mpaka nimekufa shahidi’.
Allah :
‘Muongo, lakini wewe ulipigana ili uitwe shujaa, na
umeshaitwa (shujaa duniani).
Kisha ataburutwa uso wake ukiwa chini mpaka atupwe motoni.
Na mtu mwingine atakayehukumiwa mwanzo ni yule aliyejifunza
elimu, kisha akaifundisha (kwa watu) na akasoma Qur’an. Naye
ataletwa mbele ya Allah (SWT) na na kufahamishwa neema
aliyopewa na Allah (SWT), naye ataifahamu. Kisha Allah (SWT)
atamuuliza:
Allah :
‘Umeifanyia nini
neema hiyo?’
Atajibu : ‘Nimejifundisha
elimu, na nikawafundisha watu, kisha nikasoma Qur’an
kwaajili yako.’
Allah :
‘Muongo, wewe ulisoma elimu ili uitwe mwana chuoni, na
ulisoma Qur’an ili uitwe msomaji mzuri. Na umeshaitwa (huko
duniani.)
Kisha ataburutwa uso wake ukiwa chini mpaka atupwe motoni.
Na mtu mwingine atakayehukumiwa ni yule ambaye Allah (SWT)
amemjaalia mali za aina kwa aina. Naye akazitoa sadaka na
kuzitolea zaka. Ataletwa mbele ya Allah (SWT) na
kufahamishwa neema aliyopewa na Allah (SWT), naye
ataifahamu. Kisha Allah (SWT) atamuuliza:
Allah :
‘Umeifanyia nini
neema hiyo?’
Atajibu : ‘Sikuacha
katika njia ambayo wewe unapenda watu watoe katika njia hiyo,
isipokuwa nimetoa kwaajili yako.’
Allah :
‘Muongo, wewe umetoa mali yako ili uitwe mkarim. Na
umeshaitwa (huko duniani.)
Kisha ataburutwa uso wake ukiwa chini mpaka atupwe motoni.”
Hadithi hii ni ushahidi
tosha kuwa kama mtu atakufa katika jihadi, au atatafuta
elimu, au atatoa sadaka, zaka, kujenga misikiti, kuwalisha
mayatima n.k. kwaajili ya kutaka kuonekana au kupata sifa
kutoka kwa watu, basi mtu huyo ataishia motoni.
Allah (SWT) aliwaambia
watu wote hawa watatu kuwa ni wa waongo kwa kuwa yeye Allah
tu ndiye ajuaye yaliyomo katika vifua/mioyo yetu. Allah (SWT)
anasema kumwambia Mtume (SAW):
“Sema: Kama mtayaficha au mtayadhihirisha yaliyomo katika
nyoyo zenu, basi Allah anayajua, na anajua yaliyomo mbinguni
na ardhini. Na Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni muweza”.
Qur’an 3: 29.
JINSI YA KUIPATA IKHLAASWI KATIKA
AMALI (IBADA) ZETU.
Zipo hatua kubwa tatu za
kuzingatia ili kupata ikhlaaswi katika amali zetu. Nazo ni
kujichunga kabla, wakati na baada ya kutenda amali.
i-
Kabla ya amali:
Ni lazima tuzichunge
nia zetu. Na
tujiulize ni kwanini tunafanya amali hiyo? Je tunafanya
amali ile kwaajili ya Allah (SWT) au kuna malengo mengine?
ii-
Wakati wa amali:
Wakati tukiwa ndani ya
amali, tujaribu kujikumbusha mara kwa mara, Je? Nia yetu
haijabadilika?
iii-
Baada ya amali:
Baada ya kumaliza amali
yeyote, tujaribu kuleta istighfaar
(kuomba msamaha) kwani
pengine ndani ya amali ilitupitia kufanya dhambi ya Riya.
Pia tuwe wenye kumuomba Allah (SWT) azikubali amali zetu.
Tutatolea mfano wa swala
jinsi gani mtu anaweza kujitahidi kupata ikhlaaswi katika
ibada hii.
Mara baada ya mtu kunuwia
kuswali ni sunnah kusoma dua ya istiftaahi,
yaani dua ya kufungulia
swala. Ndani ya dua hii kuna ile aya inayosema: “Inna
swalaatii, wanusukii, wa mahyii wa mamatii lillahi rabbi al
aalamiin” Kwa maana ya kuwa:
“Sema: Hakika swala yangu, na ibada zangu (nyingine zote)
……ni kwaajili ya Mwenyezi Mungu (SWT) mola wa viumbe
vyote……..” Qur’an
6:162:
Katikati ya ibada ya swala,
kwa mfano imamu akimaliza kusoma surat-al-faatiha, kisha
akisoma suratul mauun, yaani “Araita al-ladhii yukadhibu
biddiin…. (107: 1-6).” Ndani ya sura hii kuna aya isemayo
“Ole wao wenye kuswali kwaajili ya kutaka kuonekana.”
Qur’an 107:6. Kwa kusoma
aya hii, imamu huwa anajikumbusha yeye na sisi kuwa tuwe
ndani ya mstari wa ikhlaaswi katika ibada zetu. Ndiyo maana
Allah (SWT) akasema:
“Inaposomwa Qur’an, isikilizeni na mnyamaze kimya….”
Mara baada ya kumaliza
kuswali, ni sunnah kusema astaghfirullah
mara tatu (x3). Hapa
tunapata funzo kuwa tunalizapo ibada zetu, tujaribu kuomba
msamaha, pengine ndani ya ibada ile tulifanya jambo la
kumuudhi Allah (SWT).
MWENYEZI MUNGU NDIYE MJUZI ZAIDI.
Swaleh Mwanjia Kaima,
Coventry,
U.K
|