TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 »  Sira  

Makhalifa Wake

 1    Abubakar  (RA)
 2    Omar bin Khattab (RA)
 3    Othman bin Affan(RA)
 4    Ali Bin Abu Talib (RA)
 5    Omar bin Abdul Aziz (RA)

Waislamu amkeni!

Shukrani zote ni zake Allah, tunamshukuru, tunategemea msaada kutoka kwake, tunafuata uongozi wake, tunajilinda kwake kutokana na shari za nafsi zetu na amali zetu zilizo ovu. Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu hapana wa kumpotosha, na atakayeachwa kupotea (kwa sababu ya kukataa kwake kufuata uongofu), hatapata mwengine wa kumuongoza.

Nashuhudia kuwa Hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah, na kwamba Muhammad (SAW) ni Mja wake, Mtume wake na mbora wa viumbe vyake. Ameifikisha amana, amewanasihi Umma, amewatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na kuwaingiza katika Nuru ya Uislamu na amepigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki. Kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimia Mtume huyu mtukufu pamoja na Aali yake na Masahaba wake wema.

Amma baad,

Waislamu  wanaanza kupoteza mwamko wa dini yao, na hii inatokana na mazingara mbali mbali wanayofaridhishiwa na nchi za kikafiri, kama vile kuenezwa kwa filamu chafu, madishi ya televisheni yasiyosimamiwa yanayotuletea picha zenye utovu wa adabu, kuenezwa kwa vitabu mbali mbali vilivyojaa kufru na maasia, michezo isiyokuwa na asili ya Kiislamu, utumiaji wa madawa ya kulevya pamoja na kushughulishwa Waislamu na kuhifadhi majina na historia za maisha ya wanamichezo mbali mbali, waigizaji wa sinema, waimbaji, na kila aina ya watu mafasiki badala ya kuhifadhi majina ya viongozi wao wema walioisimamia dini hii na kuieneza kila pembe ya dunia tokea siku za mwanzo..

Kwa ajili hiyo nikaona bora niandike juu ya maisha ya Makhalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ili tukumbushane jinsi Masahaba hawa watukufu walivyomuamini Mtume wao (SAW) tokea siku zile za mwanzo, wakaishi pamoja naye, wakapata tabu na kuteswa pamoja, wakahama pamoja, na kwa juhudi na ushirikianao mkubwa baina yao wakaweza kuianzisha dola kubwa ya Kiislamu katika mji wa Madina, dola iliyofanikiwa kuieneza nuru ya Kiislamu mashariki ya ardhi na magharibi yake, kueneza uadilifu baina ya watu na kuwatoa watu kutoka katika kiza cha kufru ya kuabudu masanamu, kuabudu viumbe, kuabudu mizimu, kuabudu wanyama, kuabudu moto nk. na kuwaingiza katika nuru ya kumuabudu Mungu mmoja Subhanahu wa Taala asiye na mshirika.

Umma Bora

Rudi Juu

Ikiwa kila umma unajivunia historia yake, basi sisi Waislamu tuna haki zaidi ya kujivunia historia yetu iliyojaa uadilifu, huruma, ushujaa, pamoja na uongozi mwema wenye hekima.

Abubakar, Omar, Othman na Ali pamoja na masahaba wengine (Radhiyallahu Anhum), na baadaye akafuata Omar bin Abdul Aziz (RA), wote hawa waliweza kuibeba bendera ya Tawhidi mara tu baada ya kuondoka duniani kwa kipenzi chao, mwalimu wao na mwalimu wa ulimwengu mzima, Muhammad (SAW), na kuifanya ipepee bendera hiyo katika kila pembe ya dunia, hata wakastahiki kupewa sifa ya kuwa umma bora kupita umma zote zilizodhihirishiwa watu.

Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala anasema;

"Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu."

Aali Imran - 110

Na akasema:

"Na kumbukeni (enyi Waislamu) mlipokuwa wachache, mkionekana madhaifu katika ardhi; akakupeni mahala pazuri pa kukaa (Napo ni hapa Madina) na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili mupate kumshukuru."

Al Anfal – 26

Na akasema;

"Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye  kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakirukuu na kusujudu pamoja wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi yake. Alama zao zi katika nyuso zao kwa taathira ya kusujudu" .

Al Fat- h 29

Rudi Juu

Hawa ndio mfano bora wa kuigwa

 

Katika hadithi sahihi iliyopokelewa na Abu Daud, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) anasema:

·          "Anayejifananisha na kundi, yuko pamoja nalo".

Na Mwenyezi Mungu amekwisha tufahamisha kuwa siku ya kiama kutakuwa na makundi mawili tu:

Kundi la watu wa Peponi na jingine la watu wa Motoni.

Mwenyezi Mungu anasema;

·          "Kundi moja litakuwa Peponi na kundi jingine Motoni".

Ashu ura -7

Kwa hivyo ndugu zangu Waislamu tujitahidi kusoma juu ya maisha ya Makhalifa wa Mtume (SAW) na juu ya Masahaba wake waliokwisha bashiriwa Pepo, kisha tuwaige na kufuata nyayo zao, kwani hawa ni wanafunzi waliohitimu katika chuo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ambao Mwenyezi Mungu Subahanhau wa Taala anatujulisha katika kitabu chake kitukufu kuwa kesharidhika nao.

Mwenyezi Mungu anasema:

·          "Na wale walio tangulia wa kwanza, katika Wahajiri (watu wa Makkah waliohamia Madina) na Ansari  (watu wa Madina ambao ndio waliowakaribisha na kuwapokea waliohama kutoka Makkah), na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa".

At Tawba  100

Ikiwa Mwenyezi Mungu kesharidhika nao, bila shaka na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) naye pia kesharidhika nao.

 

Amma kuhusu wale wanaopenda kuwaigiza makafiri, basi Mwenyezi Mungu anasema:

·          "Hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila yao, Sema: "Hakika uongozi wa Mwenyezi Mungu ndio uongozi (khasa). "Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yale yaliyokufikia ya ujuzi (wa kweli) hutapata msaidizi yoyote wala mlinzi kwa Mwenyezi Mungu".

Al Baqarah - 120

 

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anawaambia wale wanaojifanya kama vikaragosi kwa kufuata na kuwaiga Mayahudi na Wakristo kuwa wasifikiri kuiga kwao huko kutawafanya makafiri hao wawapende, bali kinyume cha hivyo; wanajidharaulisha mbele yao na wamo katika hatari ya kutopata mlinzi wala msaada wowote mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiama.

 

Katika kuyadurusu maisha ya masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), tutapata mafundisho mengi ndani yake yakiwemo ucha Mungu wao, jihadi yao, uadilifu wao, kupendana kwao, namna walivyoishi na kustahamili kila aina ya taabu, mateso, na kuvumiliana wao kwa wao, na mafunzo haya yatatuwezesha kutuangazia njia walioipitia ili nasi tujaribu kufuata hatua zao.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujulishe nini haki ili tuifuate na atujulishe nini batili ili tujiepushe nayo   -  Aamin .

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Rudi Juu

Dibaji

 

Nabii Ibrahim, ndiye aliyejulishwa na Mola wake mahali pa kuujenga msikiti mtukufu wa Al Kaaba hapo Makkah. Akazinyanyua nguzo zake akisaidiana na mwanawe Ismail - Sala na Salaam za Mwenyezi Mungu ziwafikie wao pamoja na Mtume wetu mtukufu Muhammad (SAW).

Baada ya kulikamilisha jengo la msikiti, Mwenyezi Mungu akamtaka Nabii Ibrahimu awatangazie watu habari za Hija, awafundishe namna ya kuhiji na namna ya kumuabudu Mwenyezi Mungu wa Haki asiye na mshirika.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na (kumbuka) tulipomkalisha Ibrahimu mahali penye ile Nyumba (Na kumwambia) "Usinishirikishe na chochote na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya waizungukao na wanaokaa hapo (kufanya Ibada zao) na wanaorukuu na kusujudu (wanaosali)."

Na (tukamwambia) "Utangaze kwa watu habari za Hija, watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda (kwa machofu ya njiani) wakija kutoka katika kila njia ya mbali."

Al Hajj - 26-27

Waarabu wakauitikia mwito huo, wakawa wanakuja kuizuru nyumba kongwe hiyo kama walivyofundishwa na Nabii Ibrahim hata baada ya kufariki kwake.

Lakini baada ya miaka mingi kupita na vizazi vipya kuja, mafundisho ya kutomshirikisha Mwenyezi Mungu yakaanza kutoweka, itikadi sahihi ikaanza kubadilishwa, na masanamu yaliyoingizwa ndani ya msikiti huo ndiyo yaliyokuwa yakielekewa, yakiabudiwa, yakiombwa na kutegemewa.

Masanamu hayo yaliingizwa na mtu mmoja aitwae Amru bin Luhay, aliyekuwa mkuu wa kabila la Hudhayl, na hili ni kabila lililokuwa likitawala mji wa Makkah wakati huo.

Lata, Uzza, Manata, Hubal ni miongoni mwa masanamu yaliyokuwa yakiabudiwa huko Sham (Syria), na Amru bin Luhay alipokuwa huko katika safari zake za kibiashara akayachukuwa na kuja nayo mpaka Makkah na kuyaingiza ndani ya nyumba ile kongwe, kisha akawaamrisha watu wake kuyaabudu na kuwaambia kuwa masanamu hayo yalikuwa ni picha za watu wema waliotangulia waliokuwa wacha Mungu sana, na kwamba kwa kufanya hivyo Mwenyezi Mungu ataridhika nao na atazikubali amali zao.

Kwa vile Amru alikuwa mtu mwenye kuheshimika sana, watu wake wakamsadiki na kuanza kuyapa heshima kubwa masanamu hayo, ikawa hata watoto wanapozaliwa wakiletwa mbele ya masanamu na kujulishwa nayo, na haukupita muda mrefu karibu waarabu wote wakawa wanayaabudu masanamu hayo.

Amru akapendekeza kila kabila liwe na sanamu lake, kila kijiji kiwe na sanamu lake, kila taifa liwe na sanamu lake, na kwa ajili hiyo masanamu yakaongezeka na kuanza kujaa msikitini humo, na idadi yake ikafika masanamu 360, yaliyobomolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) siku Waislamu walipouteka mji wa Makkah.

 

Maqureshi walikuwa wakiheshimiwa sana na mataifa yote ya Kiarabu, kwa sababu wao ndio walokuwa walinzi wa nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Safari ndefu zilikuwa zikifungwa kuelekea huko, majangwa yalikatwa kwa ngamia, kwa farasi, wengine walipanda punda na wengine walitembea kwa miguu kuelekea katika nyumba kongwe hiyo, kila mmoja alikuwa na sanamu lake, kila kabila lina mungu wake, na wengine wanapokuwa safarini walikuwa wakifinyanga tende mfano wa sanamu kisha wanaliabudu, na njaa inapowashika, humuomba msamaha mungu wao huyo, ambaye ni tende na kumla.

Mila ya Nabii Ibrahim ikapotea, na Tawhid aliyoitamka, pale aliposema:

"Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule aliyeziumba mbingu na ardhi hali ya kuwa nimeacha dini za upotevu. Mimi (ni Mwislamu) si miongoni mwa washirikina".

Al An Am - 79

Tauhidi hii ilipotea kabisa.