|
Namshukuru Allah (sw),
sala na amani juu ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) huu ni
mtazamo kwa ufupi jinsi ya kuingiya kwa mwezi wa Ramadhani
na kufunga na kutoka kwa mwezi wa Ramadhani na kufunguliya.
Ndugu Muisilamu mas-ala
ya mwandamo wa mwezi yameleta mijadala na mipasuko mikubwa
miyongoni mwetu Waislamu kila mmoja anajaribu kuleta hoja
zake kuhalalisha mitazamo yake namna ya kufunga wengine
wanasema kufunga ni mwezi ukionekana popote pale ulimwenguni
wengine wanasema kila nchi ina machimbuko yake ya mwezi.
InshaAllah katika makala hayo uliyo nayo mbele yako hivi
sasa tutajaribu kukaguwa hoja za pande zote mbili ili ninyi
wenyewe Waislamu mjionee haki iko wapi bila kujiingiza
katika ushabiki usiyo na maana yoyote. Tafadhali soma kwa
makini hoja zote ili uchukuwe maamuzi mwenyewe.
Wapendwa Waislamu
mas-ala ya kufunga na kufunguwa yametundikwa kwa kuonekana
mwezi haturuhusiwi waislamu kufunga na kufunguwa mpaka
uonekane mwezi au tukamilishe siku 30. Na huu mwezi una kazi
kubwa sana na manufaa mengi katika maisha ya mwanadamu
miyongoni mwa manufaa ni hili suwala la kutekeleza Ibada na
funga ya mwezi wa Ramadhani na kuna manufaa mengine mengi
lakini hatuwezi kuelezeya manufaa yote hayo kwa kuwa siyo
dhumuni letu.
Kwanza kabisa kuhusu
suwala la mwezisayari ndugu Muislam mwezisayari umetajwa
ndani ya Qu-r an zaidi ya mara 25 lakini leo sisi
tutachukuwa aya sita tu ambazo zinazungumziya huu
mwezisayari. Ya kwanza kasema Mwenyezi Mungu:
(Ndiye
anayepambazuwa asubuhi na umeufanya usiku kuwa mapumziko na
juwa na mwezi kwenda kwa hesabu…)Qur-an 6:96.
Ushahidi juu ya aya hii
kuwa mwezisayari umeumbwa kwa ajili ya mahesabu. Kasema
tena:
(Yeye
Mwenyezi.Mungu Ndiye aliyelifanya juwa kuwa mwanga na mwezi
kuwa nuru na akaupimia vituwo (huwo mwezi)ili mjue Idadi ya
miyaka na hesabu (nyinginezo)…)Qur-an 10:5
Hapa tunapata wazi kuwa
mwezisayari una vituo na madhumuni ya kuumbwa kwake tupate
kujuwa idadi ya miyaka kwa kupitia hesabu za kila mwezi
siku kwa kuonekana kwa huo mwezisayari. Kasema tena M.Mungu:
(Na mwezi
kadhalika ni alama kwao tumeupimiya vituwo (hiki baada ya
hiki) mpaka unakuwa (mwembamba) kama chaparare la mtende kuukuu (lililonywea)
Qur-an 36:39.
Hapa vile vile M.Mungu
anatuelezeya kuwa mwezisayari una vituo na hivyo vituwo
ndiyo Idadi ya hesabu ya masiku yetu. Na kasema tena:
(Na juwa na
mwezi (huenda) kwa hesabu (yake)).Qur-an 55:5
Hapa vile vile tunapata
kuwa huu mwezisayari hutembea katika vituo vyake
alivyovipangilia Mwenyezi Mungu. kasema tena:
(Na kwa mwezi
unapokamilika)
Qur-ani84:18
Hapa Mwenyezi Mungu
anaapa kwa mwezisayari unapokamilika , kwa hiyo hapa kuna
dalili ya wazi kuwa mwezisayari unakuwa mdogo mpaka
unakamilika na halafu unarudi kuwa mdogo kasema tena
MwenyeziMungu:
(Na kwa mwezi
unapoliandama)
Qur-an 91:2.
Hapa vilevile M.Mungu
anaapa kwa mwezisayari unapoandama unapokamilisha mahesabu
ya vituwo vyake na kuanza upya. Ndugu Muislaam sasa
tuvitazame vituwo vya mwezisayari je kuna vituo vingapi?
Majina ya vituwo 10
vya mwezisayari
Ndugu Muislam mwezisayari
una vituwo 10 katika mwezi mzima kama alivyosema
MwenyeziMungu
(…Na
mwezi kuwa nuru na akaupimiya vituwo….)
na vituwo vyote kwa lugha
ya kiarabu kila kituwo kina jina lake, tukianza kituo 1-3
kinaitwa Ghurar, kituwo 4-6 kinaitwa Nuqal, kituwo cha 7-9,
kinaitwa Tus’o, na kituwo 10-12 U’shru, kituwo 13-15,
kinaitwa Albiidh, kituo 16-18 Dur’o kituo cha 19-21 kinaitwa
Dhulum, kituwo 22-24 kinaitwa Hinas, kituwo 25-27 kinaitwa
Daadi na kituwo cha mwisho 28-30 kinaitwa Muhaq.
Ndugu Muisilam hizi ndizo
aya na viyuo zenye kuonesha sisi tuzingatiye sana hesabu za
siku zetu kwa kutumiya mwezi sayari ili tupate Idadi na
hesabu ya siku tunazozihitaji na vilevile tumepata fundisho
lingine kuwa hapa MwenyeziMungu ameumba mwezi mmoja tu si
zaidi ya mmoja kwa hiyo utakapoandama popote pale ndipo
hesabu zake zinapoanza na kuelekea katika vituo vyake kama
Yeye Mwenyewe Alivyosema kuwa Ameumba mwezisayari na
Akaumba vituwo vyake. Kutokana na mafundisho haya si dhani
kuwa mwezisayari utakapo onekana nchi ya mbali na nchi
nyingine haikuuona kuwa eti vituo na hesabu zitatofautiana.
Kwa Mfano nchi hiyo iliyouona mwezisayari itakuwa tarehe
moja kwao na nchi ya pili itakuwa wao bado wapo tarehe 29 au
30. Hili ni muhali halitewezekana kamwe katika
maumbile ya MwenyeMungu ama katika mafundisho yake ya Qur-an
kama tulivyoona aya za nyuma.
Nini maana ya saumu
Kilugha saumu ni
kujizuiya na kutenda kitu ambacho unaweza kukitenda au
kujitowa katika hali fulani na ukajiweka katika hali
nyingine, na mtu kiziwi anaitwa kwa kiarabu ”Assam” na
anaambiwa aliye nyamaza “saum” kwa kuwa kajizuiya na
kuongeya kama pale ilipotwambiya Qur an
(…sema hakika
mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma ya
kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu)
Qur-ani19:26
Kisheriya saumu ni
kujizuiya Mwisilam kula na kunywa na kumuingiliya mkeo
kuanziya alfajir inapotoka mpaka juwa linopozama na hiyo
saum itatimia na kukamilika kama imeepukana na mambo yaliyoharamishwa.
Lini itafaradhishwa
hii saum ya Ramadhani?
Saumu ya Ramadhan
ilifaradhishishwa tarehe 15 Shaaban mwaka wa 2 Hijiriya, na
Mtume mwenyewe katika maisha yake kufunga Ramadhan 9 kauona
mwezi kwa macho yake mara 2 kaletewa habari za mwezi mara 3
toka Madina na mara 4 toka nje, na akawa amefariki mwezi
Rabii’al awal mwaka 11 Hijiriya,[s.a.w]
Dalili ya kufaradhishwa Mwezi wa Ramadhan
Saumu ya Ramadhani imefaradhishwa kutoka ndani ya Qur-an na
sunna sahihi ya Mtume (s.a.w.). Kasema MwenyeziMungu:
(Enyi
mlioamini mmelazimishwa kufunga saum)
kama
walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha
Mungu )Qur-an
2:183.
Na
katika sunna kasema Mtume (s.a.w.)
{Uislam umejengeka katika nguzo tano kushuhudia ya kwamba
hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mungu mmoja
tu ambaye ni Allah na Muhammadi ni Mtume wa Allah na
kusimamisha sala(tano ). Na kutoa zaka na kufunga saum ya
Ramadhani. Na kwenda kuhiji kwa mwenye uwezo wa kwenda }
Albukhari
Tunathibitisha vipi kuingiya kwa mwezi wa Ramadhani?
Kuingiya mwezi wa Ramadhani kunathibitishwa kwa njia 6 kuu.
1].kuona mwezisayari mtu peke yake itamlazimu nafsi yake
afunge
2]Wakiona mwezisayari watu wengi itawalazimu watu wote
wafunge
3]
Wakiuona mwezisayari watu wachache na wakamueleza Kiongozi
wa kiislaam itawalazimu watu wote wafunge.
4].Akiona mwezisayari mtu mmoja na akatowa habari kwa
wengine katika eneo lina kiyongozi wa kiislam itawalazimu
watu wote wafunge
5.Akiona mwezisayari mtu mmoja na akatowa habari katika eneo
lina Kiongozi wa kiislam lakini hashughulikii mambo ya
waislam itawalaazimu watu wote wafunge.
6]Kuelekea katika mji ambao umeonekana kwao mwezisayari,
tazama kitabu cha “Attalkhiss” kasema Imam Ibn hajar.
Dalili za kufunga Ramadhani kwa kuonekana mwezisayari popote
pale duniyani
Waislam watawajibika kufunga Ramadhani kama utaonekana
mwezisayari popote pale duniyani maadamu tu uonekane huwo
mwezisayari na Mwislam hata kama aliyeuona ni mtu mmoja
pasina kuweka kiwango cha msafa fulani, au kwenda kiwango
cha kutofautiyana machomozo ya mwezisayari, haya yote
hayana dalili ndani ya mafundisho ya qur-an na sunna na hata
Mtume (s.a.w.) aliyefaradhishiwa hii funga alipokuwa
akiletewa taarifa ya kuonekana mwezisayari hakuwauliza
waliomleteya habari hizo kuwa wanatokeya umbali gani au
machomozo ya mwezi wao vipi, alikuwa akitosheka na ile
taarifa ya kuonekana huo mwezisayari. Wala hayakupatikana
mafundisho kutoka kwa Mtume (s.a.w) aliwaambiya Waislam eti
kila nchi ina muandamo wake.
Wakati wa uhai wake nchi ya Yemeni na Sham zilishaingiya
uislam na maeneo mengine mbalimbali uliingia uislam,
hatukuona wala kusikia eti walikuwa wanatafutiana kufunga
kama utakavyokuja kuona mafundisho ya Mtume hapo mbele, na
kama hawakuuona mwezisayari au hawakupata taarifa alikuwa
akikamilisha Shaabani siku 30, haya ndiyo mafundisho ya
Mtume (s.a.w.).
Na
kuna hadith nyingi sana juu ya ibada hii ya funga tukianza
na hadithi ya kwanza kasema Ibn Omar (R) katika hadithi
alisimuliya ya kuwa (Aliuona mwezi
na akamwambia Mtume (s.a.w.) kuwa ameona akafunga Mtume na
akawaamrisha watu wote wafunge )[ Imepokewa na Abuu
Dawdi na Ibn Hibban,]
Hapa
tumeona kuwa Mtume (s.a.w.) ametosheka na taarifa ya mtu
mmoja wala hakumuuliza umeonekana wapi na umbali gani.
Na
kutoka kwa Rabii ibn Harash kutoka kwa mtu mmoja miyongoni
mwa masahaba wa mtume (s.a.w)kasema:”
{Wamekhitalifiyana watu siku moja juu ya siku ya mwisho wa Ramadhani
kuendelea kufunga au kufunguliya, wakaja mabedui wawili
wakashuhudiya mbele ya Mtume (s.a.w.)kuwa wameona mwezi jana
jiyoni, palepale akawaamrisha Mtume (s.a.w.)watu wafungulie}
Ahmad na Abu Dawd
Vile vile
Mtume [s.a.w] hakuwauliza mbona sisi hatukuuona na mmetoka
umbali gani au mbona machomozo yenu siyo sawa na sisi na
kadhalika imekuja hadith kutoka kwa Abu Hurayra[R.A] Kasema
Mtume: “ sumuu liruuyatihi,
waaftiru liruuyatihi yaani “Fungeni kwa kuonekana
kwake[mwezi] na funguweni kwa kuonekana kwake”.
Hadith hii
ni amri yenye kueneya kwa umma mzima ilipotamkwa
“suumuu” tamko hili linafidisha umuum katika qaida za usul
fiqhi linaitwa “Al- Amru liljam-i biswighatil Jam-i” tazama
kitabu Irshadul Fuhuuli uk 121-122.
Na amesema
Imam Ibn Qayyim kuwa maneno yote anayosema Mtume [s.a.w] ni
yenye kueneya kwa umma mzima madamu tu hakukusudiya kwa
Fulani pekee. Tukitazama hadith hiyo anasema Mtume tufunge
utakapoonekana mwezi na siyo tutakapouona sisi ndiyo tufunge
na kufunguwa bali utakapoonekana na waislamu popote pale
ulimwenguni watu wafunge wala hakusema watu wa nchi Fulani
wakiuona mwezi sayari haiwalazimu watu wa nchi nyingine
kufunga. Kwani kama tulivyoona Mtume[s.a.w] yeye mwenyewe
katika maisha yake kafunga Ramadhan 9 kauona mwezi mara 2
tu mara 7 zote kaletewa taarifa.
Hoja na majibu kwa wale
wanaohalalisha kuwa kila nchi ina machimbuko yake ya mwezi
Hoja yao
kubwa siyo Quran wala Sunna ya Mtume[s.a.w] ambavyo ndiyo
dira yetu tunapokhitilafiyana kama alivyosema Allah Taa’ala
katika Qur an “… Na kama
mkikhitilafiyana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa
MwenyeziMungu na Mtume, ikiwa mnamuamini MwenyeziMungu na
siku ya mwisho, hiyo ndiyo kheri nayo ina matokeo bora
kabisa[Qur 4:59]
Hoja kubwa
ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi wake ni moja
tu nayo ni kisa cha Kuraybu mtumwa wa Ibn Abas
walipojadiliyana na Ibn Abas mwenyewe anasema Kuraybu kuwa
“Ummullfudhli binty Harith
[mama yake huyu Ibn Abasi] alinituma kwa Muawiyya katika mji
wa Shamu nikafika Shamu na kutekeleza haja zake [zote]na
ukaonekana mwezisayari wa mwezi wa Ramadhan, na mimi nipo
Shamu, tukauona mwezisayari usiku wa kuamkiya Ijumaa, baada
ya hapo nikarudi Madina mwisho wa mwezi [wa Ramadhan]
akaniuliza Ibn Abas, kisha akautaja mwezi akasema : lini
mliuona mwezi? nikamwambiya usiku wa kuamkiya Ijumaa.
Akasema kuniuliza wewe umeuona usiku wa kuamkiya Ijumaa?
Nikajibu ndiyo na wameuona watu [wote] na wakafunga, na
akafunga Muawiyya [piya] akasema Ibn Abas lakini sisi
tumeuona mwezi usiku wa kuamkiya Jumamosi na tutaendeleya
kufunga mpaka tukamilishe siku 30, au tuuone[wenyewe],
nikamwambiya [Ibn Abas] je hukutosheka kwa kuuona Muawiyya
na kufunga kwake akajibu kwa kusema hivi ndivyo
alivyotuamrisha Mtume [s.a.w].
Ndugu
waislamu hii ndiyo dalili kubwa ya wenye kuhalalisha kila
nchi kuwa na mwezi mwandamo wake kwa hakika hawana dalili
nyingine zaidi ya kisa hiki, hebu tukichambuwe kwa undani
sote ili kila mmoja wetu apate faida je kinafaa kuwa ni
dalili ya kutegemeya?
Kumjadili Kuraybu na uchambuzi wa kisa hiki
Kwanza
watukufu waislamu kabla hatujasogeya kwenda mbali inabidi
mpate faida kumjuwa huyu Kuraybu ni nani? Hili jina la
Kuraybu ni la baba yake ambaye na wanachuwoni wa hadith
wanamkubali huyu baba yake kuwa alikuwa mtu mkweli sana na
anategemewa katika upokezi wa hadith tazama kitabu
'Tahdhibu' cha Imam Ibn Hajar Al Asqalani [ jalada la 3 uk
468 chapa ya Beurut tazama mahala pa herufi kafu]
Na tazama
vile katika Taqribu Tahdhibu cha huyu huyu Ibn Hajar Al
Asqalani jalada la 2uk 28. lakini huyu aliye katika kadhiya
hii na Ibn Abas jina lake kamili ni Muhamad Ibn Kureybu Ibn
Abi Muslim AL Hashimiy alikuwa ni mtumwa wa Ibn Abasi na
mama yake Ibn Abasi UmulFadhli alikuwa akimtuma sana kwenda
Shamu kwa Muawiyya.
Na yeye
huyu si Sahaba bali ni katika tabiin na si mtu kuaminika
katika elimu ya hadith hakubaliki. Hebu tuwasikilize
wanachuwoni wetu wa hadith wanavyomchambuwa huyu Muhamad Bin
Kuraybu.
Amesema
Athram toka kwa Ahmad bin Hanbal kuwa "huyu Muhammad Bin Kuraybu hadith zake ni 'Munkar'" Na amesema Ad
Duuriyu toka kwa Ibn Maiyn kuwa "hadith
zake huyu si chochote". Na amesema Ibn Numair;
"upokezi wake haufai kabisa ni
dhaifu". Na amesema Ibn Hatim toka kwa baba yake
kuwa "Huyu Muhamad Bin Kureybu
hazitolewi hoja hadith zake". Na amesema Abi Zur’a
kuwa "Hadith zake ni laini mno".
Na amesema Imam Bukhar kuwa
"Hadith zake huyu ni za kuchunguzwa sana". Na
akaendeleya kusema Imam Bukhari kuwa
"Hadith zake huyu ni Munkar
hazikubaliki".
Kumbuka
ndugu Muislamu pindi imam Bukhar anaposema kuwa hadith za
mtu Fulani ni munkar basi wanachuwoni wote wa hadith
wamekubaliyana kuwa zinawekwa upande wa dhaifu.
Na amesema
Imam Nnasai "Huyu Muhamad Ibn
Kureybu ni dhaifu". NA vivyo amesema Imam Adar qutni
[Tamaza Tah-dhibu Tah-dhibu ya Imam Ibn Hajar AL Asqalani
jalada la 3 uk 684-685 chapa ya Beirut. Tazama mahala pa
herufi mimu ] piya Taqribu Tah-dhibu jalada la 2 ukurasa
86. Na amesema Abubakar Al Athram:
"Nilimuuliza Imam Ahmad Bin Anmbal
kuhusiyana na hadith za huyu Muhamad Bin Kuraibu akasema 'Ni
Munkar kwa sababu analeta hadith za ajabu kabisa".
[tazama Al Jarhu Wataadil cha Imam Ibn Abi Hatim jalada la 8
uk.68chapa ya Indiya]
Na amesema
Imam Ibn Hiban kama alivyonukuliwa katika Mizanul i’tidali
ya Dhahabi kuwa "Huyu Muhamad bin
Kureybu alikuwa ni mudalisi[mrongo]". Na amesema Abu
Na’im Ad Damishq kuwa, "Huyu
Muhamd Bin Kureybu alikuwa anachanganya hadith sahihi na
dhaifu".
Kkumbuka
ndugu muislamu hakuna hata mwanachuwoni mmoja wa hadith
aliyemtaja huyu Muhamad Ibn Kureybu kuwa ni mkweli.
Baada ya
kumaliza kumkaguwa huyu Kureybu ebu sasa ndugu Muislamu
tuje kukikaguwa kisa chenyewe , tukianza na qauli ya Ibn
Abas kukataa kufunguliya kwa mwezi ulioonekana katika mji wa
Shamu kasema Imam Alqarafi katika kitabu cha “Adhakhira” ya
kuwa, "Siku ile habari ya mwezi
alipopewa Ibn Abas kutoka kwa Kureybu kulikuwa hakuna
mawingu yaliyotandaa katika mji wa Madina, na wala
haukuonekana mwezi siku hiyo , Ibn Abas akatanguliza kuuona
yeye mwezi kuliko ile habari au taarifa alioletewa na
Kureybu, na ndiyo maana akasema : hivi ndivyo
alivyotuamrisha Mtume[s.a.w] Kwa maana tusichukuwe
habari za dhana na tukaacha yakini, japokuwa hakuna tafauti
ya kuutazamiya mwezi kukiwa kuna mawingu au hakuna mawingu,
lakini yeye alihukumu kwa kuuona mwezi. Anasema Imam
Alqarafi kuwa "Hiki kisa kishakuwa
na na utata mkubwa" tazama J. 2 uk 490.
Na qauli ya
Ibn Abas ya kukataa kufunguliya mwezi ulioonekana Shamu na
kusema hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume[s.a.w] na akaishiya
hapo hakuendeleya na wala hakufafanuwa zaidi na kisa hiki
kikaishiya hapo. Na utata ukawa mkubwa katika safu za
Waislamu kutokana na kutokupatikana ufafanuzi zaidi juu ya
kisa hiki.
Sasa basi
tujiulize sote kwa pamoja kaamrishwa na Mtume[s.a.w] nini?
Wamekhitilafiyana wanazuwoni katika makundi manane juu ya
hii amri anayosema Ibn Abas kaamrishwa na Mtume[s.a.w]
1)
Kundi la kwanza la wanazuwoni wanasema kaamrishwa na Mtume
[s.a.w] asifunge wala kufunguwa katika siku itakayokuwa
mawingu yametanda angani wakamilishe 30 shaaban au 30
Ramadhan
2)
Kundi la pili wao wanasema: kaamrishwa na Mtume[s.a.w]
asipokee taarifa ya kufunga au kufunguwa kutoka kwa mtumwa
kwa sababu wale wote walioleta habari ya mwezi wa kufunga au
kufunguwa zama za Mtume [s.a.w] walikuwa si watumwa, na
Kureybu alikuwa ni mtumwa wa Ibn Abas [r.a]
3)
Kundi la tatu wao wanasema kaamrishwa na Mtume[s.a.w]
asipokee taarifa au habari ya mwezi kutoka kwa mtu mmoja tu
mpaka apatikane mwingine mwenye kumshuhudiya huyo mtowa
habari.
4)
Kundi la nne wanasema kaamrishwa na Mtume [s.a.w] kwa
yeyote yule atakaye safiri kutoka katika mji ambao
haukuonekana mwezi na kuelekeya katika mji ambao umeonekana,
basi hukumu yake atafunga pamoja na watu wa mji huo na
atakuwa ni mmoja kati ya watu wa mji huwo. Kwa mujibu ya
mafundisho haya ya Kureybu, atatakiwa afunge siku 31.
5)
Kundi la tano wao wamesema kaamrishwa na Mtume[s.a.w]
asikubali mwezi aliyouona Muawiyya kwa sababu mtazamo wake
yeye Ibn Abas[r.a.] alikuwa hautambui utawala wa Muawiyya na
alisimama pamoja na Ally bin Abi Twalibu dhidi ya Muawiyya.
Kwa mafundisho haya asikubali mwezi ulioonekana na kiyongozi
asiyetambulika.
6)
Kundi la sita wamesema kaamrishwa na Mtume [s.a.w] asikubali
kufunguwa na kulipa siku badala yake ile waliokula mchana na
isipokuwa kwa mashahidi wawili kwa hilo kuhofiya kuwalipisha
watu funga ya siku moja iliyowapita kutokana na taarifa ya
mtu mmoja.
7)
Kundi la saba wanasema kaamrishwa na Mtume [s.a.w] kila nchi
ina machomozo ya mwezisayari wake na masafa yake, na masafa
yanayokusudiwa ni KM.133.056.
QAULI YA MADHEHEBU MANNE JUU YA QADHIYA HII
Ndugu Muislamu kuna madai ya uwongo kabisa yaliyozoeleka
midomoni mwa baadhi ya ndugu zetu kuwa eti wanazuwoni wengi
wamesema kila nchi ifunge kwa machomozo ya mwezi wake
wasitegemee machomozo ya wenzao. Qauli hii si sahihi kabisa.
Kwa kweli mwenye kueneza qauli ya namna hii hana uaminifu
katika elimu kwani anaeneza qauli ya upande mmoja ambao
ambao ndiyo mtazamo wake yeye na anaficha huja za upande
mwingine. Tafadhali mpendwa Muislamu ebu soma kwa makini
tunataja misimamo ya madhehebu manne na wewe mwenyewe pima
kwa akili yako bila matamaniyo ya nafsi au ushabiki je
wanazuwoni wengi wapi wameegemeya:
a)
Tukianza na wanazuwoni wa ki-Hanafi wao wanasema:
"Kutafautiyana kwa machomozo ya
mwezi haizingatiwi katika madhehebu yetu, na ndiyo
wanazuwoni wengi walikwenda hivi, na hii ndiyo fatwa yetu,
inawalazimu watu mashariki kufunga kwa kuonekana mwezi na
watu wa Magharibi kama itathibiti kwao wameuona huo mwezi,
kwa njiya za kisheriya".
b)
Wanazuwoni wa Ki-Maliki wao wanasema:
"Utakapoonekana mwezi, itaeneya
uwajibu wa kufunga nchi zote, iwe nchi hiyo ya karibu au
mbali, wala haizingatiwi katika
hilo umbali wa masafa, na vile vile haitazingatiwa kuwafikya
machomozo au kutafautiyana machomozo, wajibu kufunga kila
atakaeletewa taarifa ya kuonekana mwezi wawe walioleta
taarifa hiyo, mashahidi wawili au watu wachache au hata watu
wengi."
c)
Wanazuwoni wa Ki-Hanbal wao wamesema
"Iitakapotihibiti kuonekana kwa
mwezi sehemu Fulani, iwe karibu au mbali, italazimu watu
wote wafunge , na hukumu ya wasiouona ni hukumu ya
waliouona".
d)
Wanazuwoni wa Ki-Shafi’i wao wamesema:
"Utakapoonekana mwezi katika mji
itawalazimu hukumu ya kufunga watu wa mji wa karibu si watu
wa mbali kwa kadiri ya tafauti yao ya machomozo ya mwezi,
na tafauti ya machomozo kati ya sehemu moja na nyingine
isipunguwe chini ya Farsakh 24 sawa sawa na kama KM
133.056".
Kwa
maana hiyo nchi kama ya Tanzaniya ina mikowa 26 na kutoka mkowa mmoja kwenda mwingine
haiupunguwi chini ya KM 200 kama tutafuwata madhehebu haya ya Kishafi’I itabidi katika
mikowa 26 kila mkowa utakuwa na funga yake. Kwa mfano Dar
es salaam kwenda Morogoro ni kilo KM.198 hawa watakuwa
wamevuka kiwango cha kufunga pamoja kwa kipimo cha madhehebu
ya Kishafi’I ambacho ni KM 133.056, kwa maana hiyo Morogoro
wao watafunga pamoja na watu wa Kibaha kwa kuwa masafa kati
ya Morogoro na Kibaha ni KM 148 takriban. Sasa je ndugu
Muislamu hili linawezekana na linaingiya akilini? Mpendwa
Muislamu tumiya akili yako kujadili hoja hizo maana wewe
mwenyewe ndiye utaulizwa kesho akhera na si sheikh Fulani au
Imamu
Wabillah Tawfiiq Waswalallahu ala Muhammad waala ali Muhamad
Kama una hujja yoyote au maswali basi tuandikiye
Vijana wa Salafiyya
Box 16101 Dar es salaam
Lukwati @yahoo.co.uk
|