TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 »  Nasaha  

NASAHA KWA WAUME

ABU AMMAAR

Moja katika mambo makuu yanayohusu ndoa na kusikika kila siku ni jinsi mke anavyopaswa kuishi na mumewe. Makala mengi na mawaidha hutolewa  kuelewesha haki na wajibu wa ndoa ikizingatia zaidi upande wa mke. Hali hii imejitokeza kutokana  khulka ya mwanamke kimaumbile kuwa dhaifu na kwa wanaume kupewa
jukumu la kuwa walinzi kwa wanawake na kwa hivyo kasoro nyingi katika ndoa hunasibishwa na kuwepo kwa hali hizi.

Ni mara chache sana kusikia vipi mume, kama upande wa pili wa ndoa, anapaswa au kuaswa  kuishi na mkewe.

Kwa kiasi fulani maelekezo haya yana nia nzuri tu ya kumuongoza mke katika njia iliyo sahihi ya kuishi pamoja na kumuenzi mume,lakini kwa upande mwengine yanaweza kuleta taswira mbaya kwa mume kana kwamba yeye huwa hatendi mambo kinyume na misingi na taratibu za ndoa ambayo pia kwa upande wake ni wajibu.

Moja katika tatizo kubwa la ndoa zetu ni kwamba wanandoa wanaandaliwa au kujiandaa kuingia katika maisha ya kuishi pamoja kama mume na mke wakiangalia zaidi upande wa maisha. Sijui tuilaumu jamii au tulaumu mabadiliko ya mifumo ya maisha yaliyopelekea kujikuta  katika hali hii. Au tuwalaumu wadau katika upande wa dini kwamba jambo hili hawalitilii mkazo unaopaswa.

Ndugu yetu wa kiislam tayari akishajiona keshajijenga kimaisha ya kumwezesha kumudu maisha ya ndoa hujiunga katika chuo cha ndoa na kuomba nusra.Na kwa mantiki hii ile misingi ya ndoa ya kiislam haipewi umuhimu unaostahiki.

Zile mila za wazee wetu zamani kumweka kitako kijana wao na kumfundisha maisha ya ndoa zimeanza kutoweka kwa kasi kubwa kiasi ya kutishia ndoa nyingi kwa kutokuwa na misingi madhubuti ya kimaadili, khulka na silka za kiislam.

Ninachokusudia ni kwamba ndoa zetu zimekosa mwelekeo halisi hasa hasa kiutaratibu. Kwani ndugu zetu wanaingia katika chuo hiki muhimu katika maisha yao ihali ya  kuwa wengi wao hawana  maarifa ya kutosha kuhusu umuhimu wa ndoa katika uislam, haki na wajibu wa mume na mke na pia hadhi kubwa ambayo uislam umeipa ndoa . Na athari zake ni matukio tofauti yanayojitokeza (mengine ya kusikitisha) katika ndoa zetu na kwa kiasi kikubwa yasingepaswa kutokea kama wanandoa wangelikuwa wanaelewa fika kuhusu taratibu za ndoa ya kiislamu na  haki na wajibu kwa kila mmoja wao.

 

Ieleweke kwamba ndoa ni moja katika alama na miujiza yake Allah Subhaanahu Wataala Arruum/21

                                                                    

  وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجاً لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآياتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ
 

Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.

 

Katika aya hii  Allah Subhaanahu Wataala katika kuonesha ihsaani  kwa waja wake ametaja vitu vitatu muhimu vinavyojenga ndoa madhubuti. Utulivu katika maisha, mapenzi na kuoneana huruma.Hivyo kila mume wa kiislamu anatakiwa avizingatie sana vitu hivi ambavyo ametuzawadia Subhaanahu Wataala na kuhakikisha vinakuwepo katika ndoa yake, pia anavienzi na kuvitekeleza ipasavyo.

 

Kwa mtu kuamua kuoa ieleweke kuwa sio kwamba anapata mke tu bali ni kuelekea katika kukamilisha dini  ukijumuisha na ulimwengu  ndani yake kama hadithi ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) inavyothibitisha kwamba :

 

من تزوج فقد استكمل نصف الإيمان فليتق الله في النصف الباقي » [صحيح الجامع:

 

"Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani (dini yake) na amuogope Allah  katika nusu itakayobakia".
                                                                  Sahihul Jaami’i

 

Katika hadithi hii Mtume (Sallallahu ‘alayhi Wasallam) anatufahamisha hadhi na daraja ya ndoa kwa muislam ni kama mtu kuwa tayari nusu ya dini yake imekamilika sasa iweje leo ghafla mtu anaweza kuamua kuondoka katika daraja hii ya juu kabisa ya imani katika dini kwa kufanya matendo yanayokwenda kinyume na maadili ya dini?


Baada ya kufunga ndoa ifahamike kwamba tokea wakati huo watu wawili hukutana pamoja na sio kama marafiki tu bali kama patna, mwenza  sahiba na kushirikana katika furaha na huzuni, mafanikio na misiba, matarajio na matatizo na pia kukabiliana na mitihani na majaribu ambayo yanapatikana ndani yake. Mmojawapo akipatwa na mitihani anajua kama ana mwenzake wa karibu na kuhakikisha anamsaidia.

Mnapoamka asubuhi macho yenu yanapofumbua macho hukutana na kusabahiana na mchana mtakuwa pamoja ikiwezekana na kama mmetingwa na shughuli bado huwa pamoja kwa kila mmoja kumjali mwenzake na kumtakia kila la kheri katika amali zake na ukifika wakati wa usiku kitu cha mwisho kwa macho yenu kabla ya kulala ni   kutakiana usingizi wa kheri,kwa ufupi ni kama aya ya Suuratul Baqarah /187 ambayo  imekhitimisha maana kamili ya ukaribu wa mume na mke  kwa kusema:

 

هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ

 

Wao ni mavazi kwenu na nyinyi na mavazi kwao

Mahusiano ya ndoa kati ya mume na mke ni aina ya mahusiano ya ajabu kabisa kulinganisha na aina nyengine zote za mahusiano ya binadamu.Daraja ya mapenzi na mahaba,kuenziana, na kuhurumiana ,amani na "raha" inayajaa katika nyoyo za mume na mke hazina mfano wake.Kwa ufupi ni vigumu kulijua hili isipokuwa kuirudisha kwa mwenyewe muumba kwamba ni moja katika rehema zake kwa waja wake.

Maisha ambayo waume siku hizi wanaishi ni maisha yaliyojaa pirika na
kuhangaika na maisha kwa kiasi kikubwa na jambo hilo kupewa kipaumbele kwa sababu nyingi  zikiwemo zile "kama mimi nikikaa ndani tutakula nini ?".Kutingwa huku kwa shughuli za "kimaisha" kwa kiasi kikubwa kumepelekea mume na mke kuwa na muda mdogo sana wa kukaa pamoja na hivyo kupelekea ile furaha iliopo na mahaba  pia kupungua(ambayo tumetakiwa na Allah tuyaenzi ). Na hasa ukizingatia mume huyu atakuwa amerudi ilhali ya kuwa amechoka hata kufanya jambo jengine lolote hawezi isipokuwa kuupumzisha mwili kwa kujiandaa na pirika za siku inayofuata. Maisha haya ya kileo yamembadilisha binadamu kutoka hali yake  na kuwa mashine kama ya "robot" ambayo haina hisia na wala kujali kitu chengine zaidi ya vile ilivyosetiwa..

Tuna mifano mingi hai ya aina ya waume ambao wameondoka na kwenda nchi za mbali kwenda kutafuta maisha na kuwaacha wake zao nyumbani huku wakijitahidi kuwahudumia kwa kila wanachokipata. Na hudiriki kuwa mbali na familia – aila - zao kwa muda mrefu tu .Wengine huwepo hapo hapo nyumbani lakini pirika za maisha kama tulivyozieleza hazimpi muda wa kutosha kustarehe na mke.Na wengine ambao wamekwenda nchi za nje pamoja na aila zao lakini mfumo tofauti wa maisha wanaokuta huko huwafanya kuwa mbali na wake zao kama wale wanaoingia kazini nyakati za usiku tu mfululizo na wengine kufanya kazi za sulubu na kuwachosha kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao muhimu.

Aina ya pili ya waume tulio nao ni ile ya wale waliokuwa wakionesha mapenzi ya dhati kabla ya ndoa zao na baada ya fungate  tu ile huba iliyokuwepo inapungua kwa daraja ya kutisha kwa dhana ile ya kuwa sasa tayari nimeshamfunga na kumtia shemere.Badala ya kuwepo mapenzi na huba hugeuka na kuwa mazoea tu ndiyo yanayowaweka wanandoa wawili na kama wakijaaliwa watoto basi huwa  ni watoto.  Ndoa zilitakiwa zikakamae kwa maana ya kwamba kila siku zikipita ndoa zizidi kuimarika ,lakini kwa bahati mbaya zetu zinakwenda kinyume chake yaani kila siku kukicha  uimara wake unazidi kupungua na lau kama hakuna kitu chengine cha kuifanya isimame kama watoto au mazoea basi tayari isingelikuwepo.

Na tumuangalie tena ruwaza (kigezo) - Mtume wetu Muhammad (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) vipi alivyokuwa akitufundisha sisi waume kuenzi ndoa. Anasema Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) katika hadithi:

             خيركم خيركم لأهله، وأنا خيركم لأهلي

 

"Mbora  miongoni mwenu wenu ni yule aliye mbora kwa mkewe na mimi ni mbora kuliko nyinyi wote  kwavni mimi ni mwema sana kwa wake zangu."

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alikuwa akionesha mapenzi ya hali ya juu kwa wakeze kwani alikuwa akicheza na kuwa na wasaa wa  kutosha kuwa pamoja nao na yatosha kupigiwa mfano kitendo chake cha kumwekea goti mkewe ili aweze kupanda ngamia .Mtume (Salla Allahu ‘alayhi Wasallam) anatoa bishara njema kwa mume na mke wanaoamshana usiku kwa ajili ya kufanya ibada na kumhimiza yule anayewahi kuamka kumwamsha mwenziwe hata ikiwa kwa kumrushia maji baridi kwenye uso wake.Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alikuwa akitoka "out " na wakeze kama ilivyoripotiwa alipomchukua mmoja wa wakeze kwenda kuangalia michezo ya wahabeshi.

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alikuwa akifanya haya kama ni kigezo kwetu jinsi ya kuyahuisha mapenzi na mahaba katika ndoa na kuienzi ili iimarike.

 

Hakuna sababu nyengine kubwa ya kuweza kuweka misingi madhubuti katika ndoa kama hapajawekwa misingi madhubuti ya mahusiano ya mtu na Allah (Subhaanahu Wataala). Ni lazima mume awe na utulivu wa nafsi na moyo wake  kwa Allah(Subhaanahu Wataala) kwanza kwa kutekeleza yale yote ambayo Allah(Subhaanahu Wataala) ameamrisha na kuacha yale yote ambayo amekataza na msingi huu moja kwa moja utampelekea mume kuwa na mahusiano mazuri kati yake na mkewe.Na endapo mume atakuwa mukhlis kwa Allah(Subhaanahu Wataala) moja kwa moja mume huyo atakuwa mukhlis kwa mkewe pia.

Na kwa kulisisitiza jambo hili Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anatufahamisha misingi ya uchaguaji mke kwamba katika kuoa, kati ya yale mambo mane ambayo kwa ajili yake mwanamke huolewa (uzuri, nasaba, mali na dini) tumchague mwenye dini kwani huyo ndiye atakayekusaidia katika kuhakikisha mahusiano ya mume na Allah (Subhaanahu Wataala) yanakuwepo pale pale hasa pakitokea ile hali ya imani kuanza kupungua.Kama anavyosema katika hadithi:

 

أن رسول الله (صلى الله عليه وسلم) قال: تنكح المرأة لأربع لمالها , ولحسبها

, ولدينها , فاظفر بذات الدين تربت يداك ولجمالها

روى البخاري ومسلم

 

Hakika Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema :

 

Mwanamke huolewa kwa mambo mane: Kwa (ajili ya) mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini (kwani) mikono yako itatakatika na michanga.  

 

                                                                 Bukhari na Muslim

 

Kwa maana hii hali itakuwa tofauti pale ambapo mke hana msingi wa dini kwani yeye ni mtu pekee wa karibu wa kuweza kuielewa hali yako na vipi ataweza kuchangia kuweza kukusaidia.

 

Yaliyobakia uzuri,nasaba na mali kama yakiwepo basi huwa ni “bonus” lakini la msingi kulitazama ni maadili na msingi wa kidini. Wanazuoni wanafafanua busara hizi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wassallam kwamba uwezo na mali bila ya kuwa na dini na taqwa ni hasara. Uzuri usiokuwa na chembe ya dini ni kiburi na ufisadi. Na nasaba (ukoo) usioambatana na dini pia ni upotevu na ujilabu na si vyenginevyo. Tunaona mifano hii katika maisha ya waliooa kwa kufuata moja ya mambo haya bila ya kuzingatia msingi wa kidini yanayowafika katika maisha yao ya ndoa.

Ndugu yangu, mume wa kiislam, jitahidi kadri ya uwezo wako kuwa mukhlis kwa mkeo kwa maneno na vitendo kwa kuongea nae, kucheka nae, kustarehe nae, kufurahi nae, kutafuta ushauri wake, kumsikiliza na kumpa umuhimu anaostahili kama mke wako.Usiwe mbinafsi wala kutokuwa na imani na mkeo .Kuwa mvumilivu kwa mitihani itakayokukabili katika ndoa na Allah (Subhaanahu Wataala) amekuandalia malipo mazuri kama hadithi ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) inavyofahamisha:

 

"Mume atakayevumilia usumbufu wa mkewe (kwa ajili ya Allah) basi Allah atamlipa mume huyo malipo sawa na malipo aliyomwahidi Nabii Ayyub (‘Alayhi Ssalaam)".

Shirikiana nae katika kazi za nyumbani pale inapowezekana.Tokeni pamoja na wala msione taabu kufanya hilo na wala isiwe kwa ajili ya kwenda hospitali tu au kuwaangalia wazee bali mtoke "out " kutembelea ndugu, jamaa na marafiki .Wala watoto wasiwe kizingiti cha kukuzuieni kufanya baadhi ya mambo yenu kwani mnaweza kuwa na utaratibu wa kuyafanya yote pasipo kuleta athari. Kumbuka ndoa hii ina mlinzi anaelinda  na anaeiangalia Annisaa/1

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُواْ رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالاً كَثِيراً وَنِسَاء وَاتَّقُواْ اللّهَ الَّذِي تَسَاءلُونَ بِهِ وَالأَرْحَامَ إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

 

Enyi watu! Mcheni Mola wenu  aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Allah ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Allah ni Mwenye kuwaangalieni

 

Pia ndoa hii ina wa kuisaidia – Allah Subhaanahu Wataala- kama anavyosema Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika hadithi:

 

« ثلاثة حق على الله تعالى عونهم: المجاهد في سبيل الله ، والمكاتب الذي يريد الأداء

والناكح الذي يريد العفاف » [صحيح الجامع 

 

Watu watatu ni hake yake Allah kuwasaidia; mwenye kupigana jihadi kwa ajili ya Allah, mwenye kuandikiana na Mtumwa (Kwa ajili ya kuachiwa huru) huku akiwa na nia ya kulitekeleza hilo, na mwenye kutaka kuoa akitaka kupata sitara na kujizuia na maovu.”

                                                                      Sahihul Jaami’i

 

Mhifadhi mkeo na kila jambo ambalo litapelekea kutiwa motoni siku ya kiama . Hakikisha unatekeleza haki zake na kutimiza wajibu wako katika ndoa . Usimchukie mkeo kwa ugomvi mdogo tu na wala usichukue maneno maneno ya nje tu na kuyatolea hukumu bila ya kuwa na ushahidi kwani maudhi ya mke ni mengi na ni nadra kuweza kukaa na mke bila ya kuudhiana - ni maumbile. Mtunukie zawadi kwani ni kitu ambacho kinavuta na kuenzi mapenzi katika ndoa. Pia msitiri mkeo kwani si miongoni mwa tabia za mume wa kiislamu kumtajia aibu na dosari za mke wake aliekabidhiwa kwa neno lake Allah Subhaanahu Wata’aala.

 

Kwa kuhitimisha, ile kauli wanayoitoa watu wa dini nyengine pale wanapofunga ndoa kwamba wanakula kiapo cha kupenda na kuienzi ndoa mpaka kifo kitakapowatenganisha haina nafasi katika uislam kwani mapenzi hayaishi kwa kutenganishwa na kifo kwani sisi waislam tunaamini kuwepo maisha baada ya kufa na hivyo kukutana na wake zetu.Attuur/21

 
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن

شَيْءٍ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ

 

Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma

 

Ndugu yangu, mume wa kiislam, mpende mkeo na penda vile ambavyo mkeo anapenda na sio mpaka kifo kitakapokutenganisheni bali mpaka mtakapokutana tena huko akhera Inshaallah.

 

Wabillahi Ttawfiq