TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 » Ramadhaan  

NINI BAADA YA RAMADHAAN?

Imeandikwa na:  Ummu Iyyaad

 

بسم الله الرحمن الرحيم  الحمد لله رب العالمين  والصلاة و السلام على سيدنا محمد وعلى آله وأصحابه أجمعين وبعد

Tunauaga mwezi wa Ramadhaan Mtukufu, mwezi wa Baraka na Rahma, tunaziwaga siku zake za  mchana tukiwa katika subira ya Swawm, na siku zake za usiku zenye ladha ya ibaada.  Tunauaga mwezi wa Qur'aan, mwezi wa Taqwa, mwezi wa Jihaad, mwezi wa Maghfirah na mwezi wa kuepushwa na moto.    Amefaulu aliyetimizia Swawm ilivyopaswa  akachuma mema mengi na akajitahidi kufanya ibaada zaidi na amekhasirika aliyepuuza Swawm na sheria zake na asichume mengi, na akafanya uvivu asiyejitahidi kufanya ibaada zaidi.

Kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى katika aya zilizotufaridhisha kufunga Ramadhaan kuwa lengo la Swawm ni kuingia katika Taqwa.

))يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ(( 

 ((Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu)) Al-Baqarah:183

Kwa hiyo kila Muislamu aliyeingia katika mwezi wa Ramadhaan atakuwa ameingia katika madrasa ya taqwa. Na mtu anapoingia katika madrasa yoyote hutoka humo akiwa amepata shahada yake ya lile somo alilolisoma, na baada ya hapo huitumia ile elimu aliyoisoma aidha kuifanyia kazi au kumsaidia katika kuendesha maisha yake yamuongoze katika uhusiano wa tabia yake pamoja na familia yake, mujtamaa wake na watu wote kwa ujumla.

Na huendelea kuitumia hiyo elimu katika maisha yake yote hadi kufa kwake. Na ni hivyo hivyo ndivyo shahada ya taqwa inayopatikana katika mwezi huu, elimu yake humuongoza Muislamu katika uhusiano wake pamoja na Mola wake, familia yake na watu wote kwa ujumla. Kwa hiyo inampasa Muislamu aendelee kuitumia elimu hii ya taqwa hadi atakapoonana na Mola wake kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى  

(( وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ))

((Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini))

Al-Hijr:99

Na hii ndio maana ya istiqaamah (kunyooka au kuendelea kuthibiti) kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى .

((فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلاَ تَطْغَوْاْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))

((Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaoelekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo))

Huud:112

((فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ))

((Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha))

Fussilat:6

 Kunyooka katika ibaada vile vile ametufundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   katika Hadiythi ifuatayo:

 ((عن أبي عَمْرو، وَقِيلَ: أبي عَمْرَةَ، سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللهِ الثّقَفيِّ رَضيَ اللهُ عَنْهُ قَال: قُلْتُ: يا رَسُولَ الله، قُلْ لي في الإِسْلاَمِ قَوْلاً، لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَداً غَيْرَكَ. قَال: "قُلْ: آمَنْتُ باللهِ ثُمَّ اسْتَقِمْ")).

((Kutoka kwa Abu 'Amr, vile vile (anajulikana kama)  Abu 'Amra Sufyaan Ibn Abdillah رضي الله عنه   ambaye amesema:

Nilisema: Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu, niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza mtu yeyote ila wewe.  Akasema (Mtume صلى الله عليه وسلم )  : Sema;  Namuamini Allaah, kisha kuwa mwenye kunyooka. (kwa kuendelea kufanya ibada na kuwa na msimamo madhubuti katika dini))

[Imesimuliwa na Muslim]

Kuthibitika katika ibaada ya Ramadhaan au msimu wowote wa ibaada ni alama ya kukubaliwa vitendo vya ibaada alivyovifanya Muislamu humo na kupotoka na kuingia katika maasi baada ya kutoka kwenye taqwa ni alama ya kuviharibu vitendo vyake vyema. Na inampasa Muislamu anapotoka katika mwezi wa Ramadhaan, hali yake ya twa'a na Mola wake iwe bora zaidi kuliko ilivyokuwa kabla. Na kuhakikisha hali hii, jiulize na ujibu maswali haya:

1)               Je, Umekufikia mchana mmoja kama mchana wa Ramadhaan  ukiwa katika  

           Swam?

2)               Je, Umekufikia usiku mmoja kama usiku wa Ramadhaan ukiwa katika Qiyaamul-

           Layl?

3)               Je, Umeburudika na kusoma Qur'aan kama ulivyoburudika katika Ramadhaan?

4)              Je, Umeuburudisha moyo wako kwa dhikr, istighfaar   du'aa na kilio kama  

           ilivyokuwa hali yako katika Ramadhaan?

Allaah سبحانه وتعالى Anapenda vitendo vya mwanaadamu anavyoviendeleza japokuwa kama ni kidogo vipi, kuliko vitendo vingi kisha asiviendeleze:

  قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ( أحب الأعمال إلى الله أدومها وإن قل)  متفق عليه

  Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Vitendo Anavyovipenda Allaah سبحانه وتعالى zaidi  (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni vidogo)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]

Kwa hiyo nyooka ewe ndugu Muislamu kwa kujiendeleza kufanya vitendo vyema na ibada katika miezi mingine yote kama ulivyokuwa ukifanya katika mwezi wa Ramadhaan  nazo ni:

SWAWM

 Funga siku sita za mwezi wa Shawwaal ili ujipatie thawabu za kufunga mwaka mzima kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

))  من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر))  رواه مسلم و الترمذي و  ابن ماجه , أبو داود و أحمد 

((Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima)). [Imepokewa na Maimaam Muslim, At Tirmidhy, Ibn Maajah, Abu Dawood  na Ahmad ]

Vile vile kuna Swawm za  Jumatatu na Alkhamiys, siku tatu katika mwezi, (Ayyaamul-Baydh), Swawm ya Arafat, swawm ya 'Ashuraa na zote zimetajwa fadhila zake katika mada inayopatikana katika TAWHIYD  kwenye kiungo hiki kifuatacho:

>>SWAWM ZA SUNNAH NA UMUHIMU WAKE<< 

QIYAAMUL-LAYL (kisimamo cha kuswali usiku)

Ni Swalah ya Sunnah iliyo bora kabisa baada ya Swalah ya Fardh kama ilivyo katika Hadiythi ifuatayo:

((أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))  رواه مسلم.

((Swalah iliyo  bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku)) [Muslim]

Na fadhila zake zimetajwa nyingi sana, ingia katika vitengo vifuatavyo utambue fadhila zake:

>>FADHILA ZA QIYAAMUL-LAYL  -  1<<

>>FADHILA ZA QIYAAMUL-LAYL  - 2<<

SADAQAH 

Ikiwa kutoa sadaqa katika Ramadhaan kumekwisha, basi kuna Fardhi ya Zakaah, na kuna milango mingi ya kutoa sadaqah pamoja na kutoa katika Jihaad fiy Sabiyli-LLah (Jihaad katika njia ya Allaah).  

KULISHA MASIKINI

Ni jambo Analolipenda Allaah سبحانه وتعالى  na Amelisisitiza katika Qur'aan na kuonya asilipuuze mwenye uwezo wa kufanya hivyo kwani miongoni mwa watu wa motoni walipoulizwa  sababu za kuweko humo walijibu kuwa baadhi ya sababu ni: 

((مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ))

((قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ))

((وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ))

((Ni nini kilicho kupelekeni Motoni))

((Waseme: Hatukuwa miongoni waliokuwa wakisali))

((Wala hatukuwa tukiwalisha masikini))

Al-Mudathir: 42-44

 

KUTENDA WEMA NA UKARIMU

Ikiwa Ramadhaan ilikubadilisha tabia yako ukawa unatenda wema kwa wazazi, ndugu, jamaa na jirani, basi  kutenda wema huko kuendelee miezi yote mingine.

Na vitendo vingi vyenginevyo inampasa Muislamu aendelee navyo siku zote wakati wote.     

Tunatoa Nasiha za dhati kwa ndugu Waislamu waliofunga Ramadhaan ipasavyo, kuendelea  kuthibiti katika taqwa na kumshukuru na kumuomba Allaah سبحانه وتعالى  Akusaidie kuwa katika hali hiyo bila ya kurudi nyuma.  Wala usiwe kama yule aliyeshona nguo yake akaipenda sana kisha akaiharibu kwa kuivuta uzi  bila ya sababu kama mfano wa  mwanamke mmoja aliyekuwa Makkah ambaye alikuwa akifuma uzi na kuufanya madhubuti kisha kila ukiwa madhubuti huufumua, naye Amemtaja Allaah سبحانه وتعالى :  

((وَلاَ تَكُونُواْ كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا))

((Wala msiwe kama mwanamke anayeuzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu)) An-Nahl:92

Hii ni kama hali ya mwenye kurudia katika ma'asi baada ya kutoka katika Ramdhaan na akaacha kuwa na twa'a na kufanya mema, akawa badala ya kuitumia neema ya kuwasiliana na Mola wake na kuwa karibu Naye, akarudi katika madhambi.  Waovu walioje watu wanaomtambua Allaah سبحانه وتعالى  katika Ramadhaan pekee. 

Alipofariki Mtume صلى الله عليه وآله وسلم , Maswahaba walikuwa katika vilio  na huzuni kubwa za ajabu hadi wengine walipigwa  na bumbuwazi, na 'Umar رضي الله عنه  alifika hadi kusema "Atakayesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Amefariki nitamuua". Walivunjikwa moyo sana hadi hali ikawa sio ya kupendeza, ndipo  Abu Bakar رضي الله عنه Akawaambia:

"من كان يعبد محمد فمحمد قد مات ومن كان يعبد الله فان الله باقي حي لا يموت"

"Yeyote aliyekuwa anamuabudu Muhammad, basi Muhammad amefariki na yeyote aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hafi"

Hali kadhalika tunasema 'aliyekuwa anaabudu Ramadhaan, basi Ramadhaan inapita na aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hapiti kuondoka (Hafi)"

Kutokuwa katika istiqaamah baada ya Ramadhaan kunadhihirika kwa njia kama zifuatazo:

1)        Kupuuza Swalah

Kutokuswali Swalah za Fardhi, au kutokuziswali  kwa wakati wake au kutokuziswali kwa kwa utulivu kama ipasavyo.

2)       Kuacha kuswali Jama'ah misikitini

Swalah ya Jama'ah ni jambo liliosisitizwa sana na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  sio Ramadhaan tu, bali siku zote za kawaida. Lakini utaona misikiti inajaa watu siku za Ramadhaan khaswa katika Swalah ya Tarawiyh ambayo ni Sunnah, wakati  Swalah za fardhi ndizo muhimu zaidi. Na   fadhila nyingi  zimetajwa katika Sunnah anazozipata Muislamu kuswali Jama'ah.

3)     Kuacha kusoma Qur'aan na kujua maana yake

Wengine  huijua Qur'aan katika Ramadhaan tu, ikimalizika Ramadhaan, misahafu inarudishwa katika kabati ijae vumbi hadi Ramadhaan nyingine, wakati Qur'aan ni uongofu kamili wetu, na ina manufaa makubwa sana katika maisha yetu kwa kila upande kwani imekusanya neema zote humo zenye manufaa kwetu kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى 

 ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))

        ((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))

((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na rehema kwa Waumini))

((Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya) Yunus: 57-58

Vile vile ni muhimu sana Muislamu ajue maana ya maneno ya Mola wake ili atambue maamrisho na makatazo yake, sheria zake anazozihitaji katika maisha yake, na vile vile Qur'aan ni kipumbazo cha moyo kwani humo kuna visa vya Mitume na watu wa kale ambavyo vina mafundisho mazito kwetu na masimulizi ya kuburudisha nyoyo.

4)      Kurudia katika mambo ya upuuzi

Inampasa Muislamu aendelee kujiepusha na mambo ya upuuzi  kama kutazama michezo ya televisheni, kusikiliza nyimbo, kukaa barazani kupiga soga, kusengenya katika simu, kusoma vitabu visivyo vya elimu na haswa elimu ya dini ya Kiislamu na kadhalika, na badala yake anatakiwa ajitahidi autumie wakati wa thamani katika kutafuta elimu ya dini yake tukufu na kuutumia wakati wake wote katika yale yenye kumridhisha Mola wake tu. Kujiepusha na mambo ya upuuzi ni moja wa sababu ya kumrithisisha Muislamu Pepo ya Firdaws kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى katika aya ifuatayo:

          ((وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ))

            ((Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi))

              Al-Muuminuun:3

Ndugu Muislamu, endelea kunyooka katika taqwa siku zote, wakati wote, kwani hujui lini Malaika wa kuchukua roho atakuwa mgeni wako. Jihadhari kukutana naye wakati uko katika ma'asi na jitayarishe uwe katika wale ambao wanapofikiwa na Malaika  wa roho uambiwe :

((يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ))

((ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً))

((فَادْخُلِي فِي عِبَادِي))

((وَاد ْخُلِي جَنَّتِي))

            ((Ewe nafsi iliyo tua))

((Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha))

            ((Basi ingia miongoni mwa waja wangu))

            ((Na ingia katika Pepo yangu))

            Al-Fajr: 27- 30

 

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atutakabalie 'amali zetu zote tulizozifanya katika Ramadhaan na Atuhidi kutuendeleza kunyooka katika taqwa na wenye kuzidisha kufanya vitendo vyema  siku zote, wakati wote hadi tutakapokutana Naye Mola wetu Mtukufu tuwe miongoni mwa wale walioamini na Atuingize Peponi kama Alivyotuahidi katika kitabu chake Kitukufu:

((إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُوْلَئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ))

 ((جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا رَّضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ذَلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ))

 ((Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe))

((Malipo yao kwa Mola Wao Mlezi ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu Yu radhi nao, na wao waradhi Naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi))

Al-Bayyinah: 7-8

Du'aa ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ya kututhibitisha nyoyo zetu katika Dini yetu tukufu.

 اَللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك

Allaahuuma Yaa Muqallibal-Quluub Thabbit Qalbiy 'Alaa Diynik

Allaahuumma, Ewe Mgeuza nyoyo, thibitisha  moyo wangu katika Dini Yako

اّللَّهُمَّ ياَ مُصَرِّفَ الْقُلُوب صَرِّف  قُلُوبَناَ عَلَى طَاعَتِك         

Allaahuumma Ya Muswarrifal-quluub Swarrif Quluubana 'Alaa Twaa'atik

Allaahumma, Ewe Muelekezaji wa nyoyo, Elekeza nyoyo zetu katika Twa'aa Yako

 

Na Allaah Anajua Zaidi