|
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa
Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:
Niya ni muhimi katika kitendo chochote cha ibada na hakuna
ikhtilaaf baina ya Maulamaa kuhusu hili. Na hii ni rai ya
Maalik, Ahmad ibn Hanbal na Abu Daawuud kwa kutoa dalili ya
Aayah:
((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ
لَهُ
الدِّينَ))
((Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa
kumtakasia Dini))
[Al-Bayyinah: 5]
Kumaubudu Allaah
سبحانه وتعالى
Pekee kwa ikhlaas ni kitendo katika moyo, nacho ndio nia na
amri katika Aayah hiyo inaonyesha kuwa ni fardhi.
Vile vile katika Sunnah Mtume
صلى الله عليه وآله وسلم
amesema katika Haidiyth iliyopokelewa na 'Umar
ibnul-Khatwaab
رضي الله عنه
((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ
ما نَوَى)) البخاري
و مسلم
((Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia
na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia))
[Al-Bukhaariy na Muslim]
Lakini
inapasa kutambua kwamba niya ya ibada yoyote kama ni kujitia
tohara, wudhuu, tayammum, Swalah, Swawm, kutoa Zakaah na
kadhalika haitamkwi kwa sauti bali huwekwa moyoni. Niya
inaunganika na elimu. Ikiwa mtu anajua anachotaka kufanya
basi tayari niya yake imeshaingia moyoni.
Kuitamka kwa sauti itakuwa sio kufuata mwendo wa Mtume
صلى الله عليه وآله وسلم
au Maswahaba zake, kwa hiyo kuitamka kwa sauti itakuwa ni
Bid'ah (uzushi). Na kama ingelikuwa ni jambo lililokuwepo
katika sheria basi Mtume
صلى الله عليه وآله وسلم
angeliwafundisha Maswahaba zake na mafunzo hayo
yangelitufikia sisi pia kwani Niya ni jambo ambalo lina
uhusiano na kila ibada ya Ummah huu; mchana na usiku kwa
hiyo ingelikuwa ni muhimu kutaja kwa sauti asingeliacha
kutoa mafunzo.
Kutamka
Niya kwa sauti ni jambo lisokuwa na mantiki, kwani mtu
anapotaka kufanya jambo la kawaida huwa hasemi kwa sauti
kuwa "mimi nataka kufanya jambo fulani", bali hutia niya yake moyoni na kujitayarisha kwa kila
njia na wakati maalum hadi atimize jambo
lake. Kwa mfano mtu
anapotaka kutoka nyumbani kwake na tuseme yuko peke yake,
basi hatosema kwa sauti kuwa 'Mimi natoka kwenda kwa fulani"
Au "natoka kwenda mahali fulani" Na Allaah
سبحانه وتعالى
ni Mwenye mifano bora.
Tutambue kuwa jambo hili limejulikana sana kutokana na
mafunzo yasiyo sahihi tuliyoyapata kutoka kwa wazazi wetu au
waalimu kwamba Niya hutajwa kwa sauti. Kama mfano tunapotaka
kuswali mtu hutia Niya kwa sauti kwa kusema: "Nawaytu
Fardha
Swalaat Adh-Dhuhr Arba'a Rakaat LiLLaahi Ta'ala……" na
kadhalika. Na kwa wengi wetu tunapoambiwa kinyume na hivyo
hushangaa na hata kwa wengine huwa ni vigumu kukubali
mafunzo sahihi. Kuna baadhi ya sehemu hadi sasa, wanaona
wasipokwenda msikitini mwezi wa Ramadhaan kunuizwa na Imaam
(Nawaytu Swawma Ghadin...) basi wanaamini kuwa kesho hawana
Swawm kwa kukosa kunuizwa siku hiyo!! Huo ni ujahili wa
dini, na ni jambo ambalo linatakiwa liachwe lisizidi
kupoteza wengi maskini wasio na elimu ya dini yao.
Basi inampasa Muislamu aliyezoea kuweka niya kwa sauti
ajirekebishe na kuweka niya moyoni katika ibada zake zote,
kutokana na mafunzo haya sahihi tunayoyaeleza pamoja na
dalili zake.
Na Allaah Anajua zaidi
|