TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 » Sunnah  

NJIA 10 ZA KUUKARIBISHA VIZURIMWEZI WA RAMADHAAN

Anasema Allaah سبحانه وتعالى

}}يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ{{ 

}} أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ{{ 

}} شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ{{ 

{{Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu}}

{{(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua}}

{{Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru}} Al-Baqarah: 183-185

Inaputasa tumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa Kutujaalia uhai na afya mpaka tunakaribia kufika mwezi mtuku wa Ramadhaan na hii ni fursa nyingine Anayotupa katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake.  

Na hii ni neema ya Allaah سبحانه وتعالى  Ambaye Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na SALE dukani, ambayo kawaida yake huwekwa muda mdogo tu.  Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Hali kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine.  Ikiwa mtu atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa'a kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa ameghufuriwa madhambi yake. Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

  (( من صام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم  

((Atakayefunga Ramadhaan kwa imaani na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) Al-Bukhariy na Muslim  

Ramadhaan ni mwezi ambao tunatimiza Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na rahma za Allaah سبحانه وتعالى. Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili.

Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza:

1.    Du'aa

Anza kwa kuomba Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi.

 ((عن أنس بن مالك رضي الله ع  أنه قال كان النبي صلى الله عليه وسلم إذا دخل رجب قال:  اللهم بارك لنا في

 رجب وشعبان وبلغنا رمضان))  رواه أحمد والطبراني

((Imetoka kwa Anas Bin Maalik رضي الله عنه kwamba unapoingia mwezi wa Rajab, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisema: Ya Allaah tubarikie Rajab na Shaaban na tufikishe Ramadhaan)) Ahmad na At-Tabariy

Na anapouona mwezi wa Ramadhaan husema:

((اللهُ أَكْـبَر، اللّهُمَّ أَهِلَّـهُ عَلَيْـنا بِالأمْـنِ وَالإيمـان، والسَّلامَـةِ والإسْلامِ،  وَالتَّـوْفيـقِ لِما  تُحِـبُّ وَتَـرَْضى،

 رَبُّنـا وَرَبُّكَ اللهُ )) رواه الترمذي والدارمي وصححه ابن حبان .

 ((Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, Ewe Mwenyezi Mungu Uanzishe kwetu kwa amani na imani, na usalama na Uislamu, na tawfiq ya kile Unachokipenda Mola wetu na Kukiridhia, Mola wetu na Mola wako ni Mwenyezi Mungu)) At-Tirmidhy, Ad-Daraamiy na kasahihisha Ibn Hibbaan

2.           Mazoezi katika mwezi wa Sha'baan  

Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha'abaan, soma Qur'aan Juzuu moja kila siku au chini yake, amka usiku uswali japo Raka'a mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe tayari umeshapata mazoezi mazuri.

3.          Shukurani   

Mshukuru Allaah سبحانه وتعالى  Kukupa uhai na siha hata uifikie Ramadhaan nyingine.  Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah سبحانه وتعالى.  Kwa hivyo fanya 'Sajdatus-Shukur' kwa neema hii tukufu.  

4.          Furaha   

Furahia kukufikia mwezi wa Ramdhaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote.  Maswahaaba (Mwenyeezi Mungu Awe radhi nao), walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri za mwezi wa Ramadhaan:

((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب  الجحيم وتغل فيه الشياطين

 فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد  

((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa)) Ahmad

5.               Jipangie wakati na weka maazimio

Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia mwezi wa Ramadhaan na kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera.  Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaani katika televisheni ambavyo sio vya dini kama 'silsilal' (maonyesho ya sinema yanayoendelea), au kucheza karata, dhumna, au kukutana barazani na kupiga gumzo na kadhalika, hali ambapo huu ni mwezi wa kufanya ibaada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:

·            Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka 'azma ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.

·                 Weka mpango ma'aluum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur'aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.

·          Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.

·          Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi inayowafikiana na hali yako.

·            Nasiha kwa kina Dada:

Msipoteze muda mwingi jikoni kwa kuanda vyakula vingi kisha hata visiliwe vyote, mkaingia katika israaf.  Na wakati mko jikoni mtajeni Allaah سبحانه وتعالى  huku mnafanya kazi zenu, kwa Dhikr na Tasbiyh, kwa hali hiyo mtaweza kupata thawabu za kupika na kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  kwa wakati mmoja.

6.             Tawbah na Maghfirah      

Omba Tawbah Nasuuha kwa Mola wako na waombe  msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swawm na Swalah zako na  pia kukupa imani kuwa huna haki ya mtu.

7.      Jifunze Fiqhi ya Swaum

Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako.  Jifunze Swawm kama aliyokuwa akifunga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.

Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:

 ((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع  طعامه وشرابه))       البخاري   

((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) Al-Bukhariy

7.                Jitayarishe kuchuma mema mengi :  

Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma Rahma na mapenzi.  

·             Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu, jamaa.

·             Kama inakupasa kutoa Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia.

·              Weka 'azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.

 ((قال صلى الله عليه وسلم :  من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من  أجر الصائم شيء ))

 أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان

((Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Atakayemfuturisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Sh Albani

·               Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'awah kwa jirani yako.

8.      Hitimisha Qur'aan, Hifadhi na jifunze Tarjama 

Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur'aan kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur'aan na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl عليه السلام   kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kusoma naye Qur'aan yote

((عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود  ما يكون

   في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛  فلَرسول الله صلى الله

 عليه وسلم أجود بالخير من الريح المرسلة  ((رواه البخاري ومسلم

 ((Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba

  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم      alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhaan wakati Jibriyl anapokutana naye, na alikuwa anakutana naye kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur'aan na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni mbora wa kheri kuliko upepo uanovuma))  Al-Bukhariy na Muslim  

Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur'aan kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur'aan. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka katika Ramadhaani uwe una sura zaidi za kusoma katika Swalah zako. 

9.      Darsa

Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha.  Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha imani yako.  Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku.  Kama huwezi kuhudhuria msikitini, Alhamdulillah, TAWHIYD.CO.UK imewatayarishia mawaidha mengi ya kusikiliza na ya VIDEO.  Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipate manufaa. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha ni mojawapo wa chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza imaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu.  

10.   Fungua 'Swafha' (Ukurasa) mpya katika maisha yako  

Baada ya kuweza kuyatimiza hayo yote, bila ya shaka hali yako ya imani imekuwa bora kabisa na utakuwa umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na ulivyo.  Kwa hivyo weka 'azma ya kuendelea hata baada ya Ramadhaan kuwa katika twa'a na ibada, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Swalah ya usiku),kusoma Qur'aan japo kidogo KILA SIKU, na iwe umefungua UKURASA MPYA wa maisha yako na kumuomba Allaah سبحانه وتعالى  Akuendeleze katika hali hii.

Tunachukua Fursa hii ya kuwaombeeni Ramadhaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke katika mwezi huu tukiwa tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye kubeba thawabu nyingi ziwe nzito katika Miyzaan ya Hasanaat siku ya Qiyaamah. 

 

اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنّأ وَ مِنْكُم صَالح الأّعْماَل

Allaahumma Taqabbal Minnaa wa Minkum Swaalih al-A'aamal.  Aamiyn