|
Ukimuuliza Muislamu yeyote suala hili bila shaka utapata
jawabu la “ndio”, Ramadhani huisha ile siku tunayojumuika
pamoja kwa furaha kusheherekea ‘Eid-el-Fitri. Maamrisho ya
kujizuwia kula, kunywa na mashirikiano ya kimwili kati ya
mke na mume wakati wa mchana wa Mwezi wa Ramadhani
tunayapata moja kwa moja kutoka kwenye Kurani Tukufu na
Hadithi za Bwana Mtume (S.A.W). Lakini kwa kweli kama
tutachunguza kwa undani baraka za Mwezi huu Mtukufu wa
Ramadhani, tutaona kwamba mafunzo yake yanakusudiwa kubakia
na kutekelezwa na kila mmoja wetu baada ya kumalizika kwa
chuo hichi adhimu kwa muda wote utakaofuatia baada ya
Ramadhani.
Kwanza kabisa, suala zima la kujizuwia na kula, kunywa na
matamanio ya kiwiliwili kutoka alfajiri hadi magharibi
tunapata mafundisho maalumu. Katika mafunzo hayo ni pamoja
na:
1) Utulivu na Upole
2) Kuwa na tafakur
3) Kuishi ndani ya Qur'ani
4) Kuwafikiri waja wenzetu na hali ya Umma wa Kiislam
kwa ujumla
5) Kujiweka mbali na mapambo na matamanio ya vitu vya
kidunia
Mafunzo haya na neema nyingi nyingi yatatuwezesha, kwa
uwezo wa Allah, kutupa faida ya hali ya juu ya uvumilivu na
ustahamilivu katika nafsi zetu. Mwenye Enzi Mungu Anasema
katika Kurani tukufu:
((Enyi
mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika
Mwenyezi Mungu Yu pamoja na wanaosubiri))
[Sura Al-Baqarah 153]
Kumpenda Allah (s.w.t) na kumtii kwa maamrisho Yake ndio
msingi wa ibada na ndio lengo hasa la sisi wanaadamu kuwepo
hapa ulimwenguni. Kwa ajili hiyo basi tunapojiuliza na
kutafakari mafunzo tunayopata ndani ya Ramadhani na umuhimu
wake kwa maisha yetu ya kila siku, inatubainikia kuwa lengo
hasa la kuingia kwenye chuo hichi adhimu ni kuziweka nyoyo
zetu ndani ya taqwa ya kumtii Allah (s.w.t.) kwa muda wote
unaofuatia baada ya Ramadhani karimu.
Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Kurani tukufu:
((Enyi
watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na
poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa
Waumini))
((Sema: Kwa
fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake! Basi nawafurahi
kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya))
[Sura Yunus 57 – 58]
Hivyo basi ni wazi kabisa kuwa ibada ya funga ya Ramadhani
ni katika nguzo kubwa iliyo muhimu ya dini ya Kiislam
iliyokusudiwa kutusaidia kama wanaadamu katika kufanikisha
lengo la kuwepo kwetu duniani kama makhalifa wa Allah (s.w.t.).
Kwa kuwa Ramadhani ni chuo adhimu cha kutuleta ndani yake taqwa
pale tunapokuwa wastahamilivu na wanyenyekevu katika kufuata
maamrisho ya Allah ndani ya nafsi zetu tunapata faida ya
kuwa waadilifu na kuipigania njia ya Mwenyezi Mungu ndani ya
nafsi zetu kwanza. Vita hivi vya kuzilea nafsi kwa ajili ya
Allah(s.w.t.), huitwa Jihaad.
Jihad inakusanya yale yote, kuanzia vita dhidi ya makafiri na
ushirikina na yale yote yaliyokatazwa na Allah (s.w.t.) ili
kupata daraja ya juu kabisa ya mafanikio katika maisha ya
Muislamu mbele ya Allah (s.w.t.) Mwenyeezi Mungu Anasema
katika kurani tukufu:
((Wale
walioamini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wanacheo
kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye
kufuzu.
[Sura Taubah 9:20]
Wengi wetu huelewa neno Jihaad kwa maana finyu kabisa, ya
kuchukua silaha na kwenda vitani. Kwa mafundisho ya Bwana
Mtume (s.a.w) kwenda vitani ni katika jihadi ndogo. Jihadi
kubwa haswa ni kupigana na nafsi zetu kwa kuwacha yale yote
tuliyokatazwa na Allah (s.w.t.) na
Mtume
wake (s.a.w.) na kufanya yale tuliyoamrishwa ndani ya
Uislamu.
Kwa kufanya hivyo tu ndio tutafuzu mbele ya Allah (s.w.t.)
kwa kuishi maisha bora hapa duniani na kutarajia mema kesho
akhera.
Hivyo basi kwisha kwa Ramadhani isiwe ndiyo mwisho wa sisi
kufanya mema na kuishi nje ya mipaka ya Allah(s.w.t.), bali
tubebe tabia zote njema tulizojifunza ndani ya mwezi huu
mtukufu na kwa kufanya hivyo tu , ndio tutakuwa Waislamu wa
kweli.
|