|
Assalaamu'Alaykum
Warahmatu Llahi Wabarakaatuh,
Shukrani zote ni zake Subhanah Yule
anaye mjibu (muitikia) mwenye shida pale anapo muomba,
Maalik yawmid Diyn,
Maalik asiye Mpinzani wa Siku isiyo shaka wala
wasi wasi kuja kwake, siku ambayo watu watagawika makundi
mawili makubwa; kundi moja litakuwa la watu wa Peponi, na
kundi jengine ni la watu wa Motoni.
Rehma
na
Amani za
Allah zimfikie
Al-Habibu Musttafa (Salla
Llahu 'Alayhi Wa'ala Aalihi Wasallam) aliyepewa
ujumbe kupitia Qur-an kututaka waislamu tujihadhari,
tujitayarishe na tujiandae na siku hiyo, kwani kila mmoja
wetu atalipwa kwa alichochuma na kuwa mmoja kati ya makundi
mawili, Qur-an inasema :
وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ
تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ
“Na
iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allah, kisha kila nafsi
italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa”
al-Baqarah
aya ya 281.
Ayuhal Ahibaa,
Namshukuru Mola wangu na wako, Mola
Mlezi anaewabashiria wenye kufaulu na kufuzu rehma
zitokazo kwake, na radhi zake, na Jannaatin (mabustani)
ambayo humo watapata neema za kudumu.
Namshukuru Mola wangu na wako, Mwenye kutoa
hakikisho kuwa wenye kufaulu katika mitihani mingi (ukiwemo
huu wa Ramadhan) watadumu humo (katika Jannaatin)
milele.
Namshukuru Mola wangu na wako, Mola aliyetoa
changamoto kwa kila mwenye kujaaliwa kushinda katika
mashindano aliyoyatangaza kuwa kwake Yeye yapo malipo
makubwa yenye kuvutia na kufurahisha kwa kila mwenye
kumtarajiya, kumkumbuka sana na kuyatekeleza yale yote
ayatakayo Yeye Subhanah.
Ndugu yangu katika iman,
napenda kutumia nafasi hii kujiusia nafsi yangu
kwanza na nafsi zenu kumcha
Allah
Subhaanahu Wata’ala kwa kumtii,
na Ndugu kwa kutekeleza kila aloliamrisha kadiri
ya uwezo wetu, na kujikataza na kila alichokikataza mara
moja.
Ndugu
yangu katika iman, kwa munasaba huu mtukufu napenda
kusema: ‘Iyd Mubarak kwa nyote na familia zenu na kwa
kila aliyejaaliwa kutekeleza ibada ‘adhiymu ya
saum kama alivyotakiwa aitekeleze na
Dhul Jalaali wal Ikraam.
Ndugu yangu katika iman, ‘iyd katika
Uislamu ni ibada hivyo tunatakiwa tujiandae na ibada hii,
ibada ambayo inaonyesha shukrani zetu kwa Rahmaan kwa
kutuwezesha kuishi na Ramadhan na kutuwafikisha
kumuaga mgeni wetu, mgeni ambaye tunamtarajia awe
amekubaliwa na Mwenye kuwakubalia
Muttaqiyn.
Ndugu
yangu katika iman, kuondoka kwa mgeni wetu mtukufu
kunatupeleka kuwa na siku yenye kueleweka na sote kuwa ni
‘Iydul-Fittri
, siku ambayo ni mahafali (sherehe) kwa sisi sote
tuliojaaliwa kuhudhuria mafunzo/masomo katika chuo kikuu cha
Ramadhan.
Ndugu yangu katika iman, kwa kuwa sote
tulihudhuria darasa katika masiku machache yaliyopita hivyo
ni vyema tuelewe kuwa siku ya kuwepa shahada na nishani zetu
ndio imefika, kama tulihudhuria darasa na kuwa haadhir
katika darasa letu kwa kuiishi na kukaa vyema na mgeni wetu
mtukufu (Ramadhan), basi insha Allah tutapata
yale wanayoyatarajiwa waliohudhuria darasa (waliofunga na
kusimama) katika masiku machache ya mgeni wetu
Ramadhan.
Ndugu
yangu katika iman, mgeni wetu Ramadhan
ameondoka baada ya kuishi na kukaa na sisi na insha Allah
amewafikishwa kuifanya kazi ngumu kabisa, kazi ya
kutusafisha na kutukosha kwa vyenye kusafisha na kukosha
(sala, sadaqaat, saumu, dhikr, visimamo vya usiku,
tiwatul Qur-an, kufutarisha, kuhudhuria mihadhara,
kusikiliza mawaidha, istighfaar na kadhalika) na
kutusuuza kwa maji safi yenye uwezo wa kusuuza na kuondowa
kila aina ya uchafu tuliokuwa nao na kuondoka hali ya kuwa
tuko katika usafi insha Allah usafi wa mtu
aliyezaliwa na mama ake!
Ndugu
yangu katika iman, Ramadhan imeondoka baada ya
kutusafisha na kutuweka safi, itakuwaje tujitose katika
uchafu wa matope wa kila aina ya mambo yaliyokatazwa na Mola
wangu wa wako siku ya kwanza tu baada ya Ramadhan
kuondoka!
Ndugu
yangu katika iman, kama tuna uhakika (hakuna wenye
uhakika sote tunataraji tu) wa kukubaliwa kwa mgeni wetu (Ramadhan)
na Rahmaan, basi siku ya ‘iyd ni siku ya
kushukuru na kufurahi kuwa saumu yetu imekubaliwa, na
furaha na shukrani za kukubaliwa kwa ‘amali yo yote
ile huwa kwa kufanya yenye kuridhiwa na Jabbaar na
sio kinyume chake.
Ndugu yangu katika iman, kama tulikuwa
hatuna furaha kwa kuwa Ramadhan imekuja kutunyima
uhuru wetu (kufanya tuyatakayo) na sasa tumefurahi kwa
kuondoka kwake, kwani tumepata uhuru wetu hivyo
tutawaonyesha wasio jijuwa na kuelewa demokrasia (mtu
kufanya au kusema alitakalo hata kumuasi Mola wake),
maendeleo na vipi kuishi katika dunia hii (bila ya
kuingiliana kwa kuamrishana mema na kukatazana mabaya),
tutawaonyesha kwa kupanga kufanya kila lenye kumuasi Mola na
Mjumbe wake, kumuudhi Mola na Mjumbee, kutuondoshea utu
wetu, kuthibitisha kuwa sisi hatuna haya wala hatuoni
vibaya, tutahakikisha kwa wale waliokuwa wakitutaka tule na
tunywe (katika masiku ya Ramadhan) kuwa tulikuwa
hatufungi lakini tulikuwa tukitekeleza ada, mila na desturi
tulizokuwa tukiwaona wakitekeleza wazee wetu, bali tulikuwa
tukiwacheza shere hawa wasiotaka maendeleo au wasioendelea
juu ya kuwepo kwao huku ulaya bado wanasali na kufunga kama
wajinga wenzao waliotangulia. Hivyo tutapanga kufanya na
kuhakikisha tunatoa kila tulichanacho (nafsi zetu na mali
zetu) katika kumuasi na kutekeleza yote yale aliyoyakataza
Rahmaan (twamuomba Jabbar atuhifadhi na shari
za watu hawa na wengine kama hawa hata kama ni ndugu zetu au
jamaa zetu na jirani zetu), kama walivyopanga kufanya
majahili kama hawa:
(TAARIFA
YA MALIKO, BISMILLAAHI RAHMAANI RAHIIM
Kwa kusherehekea kumalizika mwezi mtukufu wa
Ramadhan, Bi XXX wa Slough na Bi YYY wa Derby pamoja na
wenzao wana furaha ya kuwaalika waislam wote wa kike na wa
kiume katika sherehe za Idi zitakazofanyika katika ukumbi wa
Britwell, Slough; siku ya Jumatatu tarehe 23/10/06 kuanzia
saa nane za mchana hadi saa nne za usiku.
Chakula na
vinywaji vya aina zote vitakuwepo, vikifuatiwa na burudani
ya Rusha Roho na Disco Toto pamoja na magoma moto moto ya
aina zote.
Nyote munakaribishwa pamoja na watoto wenu
kuja kufurahia siku kuu.
Kingilio ni £ 5.00 . Tafadhali muarifu
mwenzako.)
Mambo kama
haya hayafanywi, hayatangaziwi, hayaenezwi na wala hashiriki
au hata kutowa fikra na mawazo wachilia mbali kuhudhuria
(hata kama utakodiwa na kulipwa kupeleka watu au vifaa au
vyakula au vinywaji) mwenye kutaraji kukubaliwa Ramadhan
yao, kutolewa katika moto na kusamehewa majidhambi yao,
wachilia mbali wenye kutarajia kukutana na Mola wangu na
wako Mlezi.
Ndugu
yangu katika iman, kumalizika kwa mwezi tena mtukufu
sherehe huwa na heshima na desturi zilizowekwa na
Rahmaan. Ndugu yangu katika iman, fikiria ni
wangapi ulisali nao ‘iyd mwaka jana? Wako wapi leo,
wamekwenda wapi?
Ndugu
yangu katika iman, ni kweli sherehe itakuwa sherehe
ya kusheherekea kumalizika funga kwa kukusanyika wake kwa
waume na vinywaji vya aina zote! Ni kweli sherehe itakuwa
sherehe yenye kustahiki kuhudhuriwa na waliokuwa wenyeji wa
Ramadhan katika masiku machache na matukufu huku
wakijigamba (kama inavyothibitisha matendo na mipango yao)
na kujisifu kuwa wao hawana khofu wala wasi wasi na moto wa
Jahannam!
Ndugu
yangu katika iman, roho unairusha, itaangukia wapi
kama sio motoni? Motoni ambako huna uhakika kama ulikuwa
miongoni mwa waliotolewa (na kama ulikuwa miongoni mwa
waliotolewa –jambo ambalo ni muhali- huoni haya kurudi jela
siku ile ile uliotolewa) katika Ramadhan au bado
umebakishwa humo humo kwa upotofu wako! Qur-an
inasema:
أُوْلَـئِكَ
الَّذِينَ اشْتَرُوُاْ الضَّلاَلَةَ بِالْهُدَى فَمَا رَبِحَت
تِّجَارَتُهُمْ وَمَا كَانُواْ مُهْتَدِينَ
“Hao
ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini biashara yao
haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka”
al-Baqarah aya ya 16.
Ndugu
yangu katika iman, muislamu hutarajiwa kununuwa
uongofu na sio upotofu (kingilio
ni £5.00), Qur-an inasema:
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي
لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ
عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا
أُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ
مُّهِينٌ
“Na
miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili
wawapoteze watu na njia ya Allah pasipo kujua, na
wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya
kuwafedhehesha
“ al-Luqmaan aya ya 6.
Ndugu
yangu katika iman, kiingilio
£5.00, vipi kuhusu
zakaatul fittri! Magoma ni moto moto, wewe ulikuwa
ukiomba katika masiku machache na matukufu utolewe katika
moto na baada ya kuondoka Ramadhan unanunua Moto
mmoja kwa moto moto! Tunajilinda na Allah, Moto wa
Jahannam haukutoshi unataka zaidi!
Ndugu
yangu katika iman, hii ndio hali zetu kwa uhakika (Bi
XXX wa Slough na Bi YYY wa Derby pamoja na wenzao wana
furaha ya kuwaalika),
huu ndio uislamu wetu, hii ndio iman, ‘aqidah na
matarajio yetu kwa Mola wetu! Hivyo kweli sisi ni waislamu
! Qur-an inasema:
الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ
يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ
وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ نَسُواْ اللّهَ فَنَسِيَهُمْ إِنَّ
الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ
“Wanaume
wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja.
Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao.
Wamemsahau Allah, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika
wanaafiki ndio wapotofu.” At-Tawbah
aya ya 67.
Ndugu
Waislamu, lengo letu katika maisha yetu ya kila siku hapa
duniani liwe ni kumridhisha Jabbar pekee, hivyo kila
tunachokisema au kukitenda au kiandika tuwe na ikhlasi
ndani yake kwa iman na kusudio la kumridhisha
Allah pekee.
Ndugu
Waislamu, ni vyema tuelewe kuwa al-Habibu Mustafa (Salla
Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) hakutumwa isipokuwa
awe ni mwenye kupendwa, kigezo na mfano wa kufuatwa na kila
mwenye kumtaraji Allah katika kila nyanja ya maisha
yetu ya kila siku, hivyo tuwe na hadhari na familia zetu kwa
tunaempenda, kumsikiliza, kumfuata, kumsaidia na kumfanya
kuwa rafiki (shoga) au hata kumkaribisha nyumbani kwako au
kumchukuwa kama kigezo chetu au kuwa ndio mfano wetu.
Ndugu
Waislamu, ‘iyd haiwi ‘iyd kama hatutokuwa
tayari kusameheyana, kukumbushana, kuwaidhiana, kuusiana na
kuamrishana mema na kukatazana maovu (kama hayo
waliyoyaandaa wanawake wawili na kundi lao) katika maisha
yetu ya kila siku. Ndugu Waislamu, ni vyema tuelewe kuwa
sisi ni waislamu, na hatutokuwa na maendeleo yo yote yale
wala heshima wala 'izzah bila ya kurudi katika dini
yetu na kujinasibisha nayo katika maisha yetu ya kila siku.
Ndugu
Waislamu, Uislamu ndio dini pekee ya haki mbele ya Allah, sisi
kama Waislamu nini tunafanya katika kuonyesha na
kuthibitisha haya (rusha roho, magoma moto moto, vinywaji wa
kila aina, wake kwa waume, tafadhali muarifu mwenzako –
laiti tungekuwa tuna arifiana mambo ya kheri- )? Uko wapi
utekelezaji wetu wa maamrisho ya Allah na utekelezaji
wetu wa makatazo ya Allah, uko wapi ulinganio wetu
kwa watu kurudi katika dini ya Allah na kwa wasiokuwa
waislamu kuingia na kufuata dini ya Allah, dini ya
haki inayokenda sambamba na maumbile yetu.
Ndugu
katika iman, fanya kila ulifanyalo lakini hakikisha
kuwa litakupelekea kuweza kujihakikishia kuwa siku ya
‘iyd kwako ni ile siku utakayopewa kitabu chako kwa
mkono wa kulia, Qur-an inasema:
“Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono
wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
(tafadhali
waarifu wenzako) Hakika nalijua ya kuwa
nitapokea hisabu yangu. Basi yeye atakuwa katika maisha ya
kupendeza. Katika Bustani ya juu (ukumbi
wa Britwell, Slough).
Matunda yake yakaribu. Waambiwe: Kuleni na
mnywe kwa furaha (Chakula
na vinywaji vya aina zote vitakuwepo)
kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita (kuanzia
saa nane za mchana hadi saa nne za usiku).”
Al-Haaqqah aya ya 19-24.
Ndugu yangu katika iman, fanya
ulifanyalo litatokuhakikishia kuwa ‘iyd yako na
furaha yako ya kweli na sherehe za kusheherekea iwe ile siku
utakayo epusha na Jahannam Moto (Rusha Roho,
Disco Toto pamoja na magoma moto moto ya aina zote) na
kuambiwa kwa heshma na ta’adhima ingia Peponi, Qur-an
inasema:
كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ
الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ
الْقِيَامَةِ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ
الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما
الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ
“Kila
nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu
kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na
akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu
ila ni starehe ya udanganyifu.”
Al ‘Imraan
aya ya
185.
Hivyo ni
vyema kila tunapokutana kuwaombea dua na kuwaombea
maghfirah msamaha kwa Ghaffar Mola wetu na Mola
wa waliokuwa kabla yetu na watakao kuja baada yetu.
Ndugu
Waislamu, tumuombe ar-Rahmaan aturejeshe katika dini
yake urejesho ulio mzuri,
tumuombe ar-Rahmaan atukubalie yetu Ramadhan,
atupe uwezo wa kutekeleza ayatakayo Yeye Subhanah
Muumba wetu, na kuachana na makatazo yake, atupe
uwezo wa kufikisha amana kama ilivyofikisha al-Habibu
Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam),
atutie mapenzi baina yetu mapenzi yatayozaa kuwa tayari
kusameheyana, kuhurumiana, kupendana, kustahamiliana,
kamrishana mema na kukatazana maovu na kadhalika.
Kila mwaka na nyinyi muko katika kheri
Wassalamu'alaykum Warahmatu Llahi Wabarakatuh
Mkusanyaji
Ndugu yenu katika
imani
Abu Fatimah
|