Sifa zake
Alipofariki dunia mwaka
1982 Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy alikuwa bila shaka
yoyote mwanachuoni na mwana historia mkubwa wa Kiislamu
na mmojawapo wa washairi wakubwa.
Atakumbukwa daima kwa uso
wake mkunjufu usioacha kutabasamu na kwa mwenenedo na
tabia zake njema. Wakati wote alikuwa akizungukwa na
watu wanaotaka kumsalimia au kupata kutoka kwake mafunzo
ya Dini.
Umaarufu wake ulikuwa si
katika kisiwa cha Zanzibar na nchi za Afrika ya
Mashariki peke yake, bali ulienea hadi Somalia ya kusini
na ya kaskazini, Cape Town upande wa kusini mpaka
kufikia Malawi, mwahali alipokuwa akitoa darsi zake
kabla ya kuhamia Kenya kwa kuhofia kukamatwa na serikali
ya Zanzibar.
Alizaliwa Zanzibar mwezi wa
February mwaka 1912 katika ukoo maarufu, akajifunza
Qur-aan kutoka kwa Fatma Hamid Said (1854-1936),
aliyesoma kwa Sheikh Amin bin Ahmed aliyekuwa
akifundisha Qur-aan kijiji cha Jongeani mahali
alipozaliwa Sheikh Abdullah Farsy na kukulia.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
alihifadhi Qur-aan yote pamoja na hadithi nyingi za
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam)
akiwa na umri mdogo sana, na shauku yake kubwa
isiyotoshelezeka ya kujifunza masomo ya Kiislamu na ya
kiulimwengu ilionekana pale wenzake walipokuwa
wakijishughulisha na michezo na anasa za kidunia, wakati
yeye alikuwa kila siku akizama katika kusoma kitabu
kipya cha mafunzo ya Kiislamu.
Alikuwa akipenda sana
kusoma kiasi ambapo maisha yake yote yalifungika ndani
ya maktaba 'library' yake kubwa ya nyumbani.
Alipofariki dunia, Sheikh
Abdullah Saleh al-Farsy alikuwa Aalim mwenye kutambulika
na kuheshimika kupita wote katika nchi zinazotumia lugha
ya Kiswahili. Mchango wake usiokuwa na mfano katika
kuelimisha watu dini ya Kiislamu ulifikia kiwango chake
cha juu baada ya kuchapicha tafsiri kamili ya mwanzo ya
Qur-aan Takatifu ya Kiswahili iliyokubaliwa rasmi yenye
kurasa 807.
Elimu yake
Alipokuwa kijana,
mwanachuoni huyu mwenye hamasa na uhodari alibahatika
wakati ule kuwepo na kuenea kwa vyuo vikongwe vya
Kiislamu vilivyojaa wanafunzi chini ya uongozi wa
Maulamaa weledi mfano wa Sheikh Abu Bakar bin Abdullah
bin Bakathir (1881-1943) aliyekuwa mwanafunzi maarufu wa
Sayyid Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait (1961-1925)
Katika mwaka wa 1922 Sheikh
Abdullah Saleh Farsy alijiunga na chuo cha Msikiti Barza
baada ya Maulamaa wawili kumtaka afanya hivyo:
Wa kwanza
alikuwa Sayyid Hamid bin Mansab (1902-1965) aliyemfunza
RISALATUL JAMI'A, yenye mafunzo ya taasisi ya Kiislamu.
Imamu huyu wa msikiti wa Forodhani aliyefariki dunia
wakati akitoa darsi ndani ya msikiti Gofu alikuwa
mwanafunzi wa Sheikh Muhammad Abdul Rahman Makhzymy
(1877-1946), mmojawapo wa waalimu wa Sheikh Abdullah
Saleh Farsy.
Wa pili
alikuwa Sayyid Alawy bin Abdul Wahab (1902-1960)
aliyemsomesha vitabu 12 vya Fiq'hi katika lugha ya
kiarabu pamoja na sharhi ya MARDFIN RABBIYYAH juu ya
elimu ya urithi.
Baada ya kuwa mjuzi katika
elimu ya taasisi ya Kiislamu katika chuo cha Msikiti
Barza, Sheikh Abdullah Saleh Farsy alikuwa mjuzi pia wa
elimu ya nahau ya lugha ya Kiarabu. Na alipokuwa na umri
wa miaka 20 alikuwa akiandika mashairi ya Kiarabu,
dalili ya daraja kubwa ya elimu ambayo Maulamaa wa
Zanzibar wakati ule waliweza kuieneza.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
alijifunza chini ya Maulamaa wengi wakubwa kama vile
Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry (1873-1936)
aliyemfundisha vitabu 25 vikiwemo Tafsiri ya Jalalayn
kilichoandikwa na Jalal al-Din Mahali (1389-1450) kutoka
Misri na Jalal al-Din Suyuti (1445-1505), Syria, na hawa
ni Maulamaa wakubwa na maarufu wa madhehebu ya Imam
Shafi.
Baada ya kuhitimu darsi
zote katika chuo cha Msikiti Barza, Sheikh Abdullah
Saleh Farsy aliruhusiwa na Sheikh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry
kusomesha katika chuo hicho katika mwezi wa Ramadhan
chini ya uangalizi wake.
Alijifunza pia kutoka kwa
Sheikh Abu Bakar (1881-1943), mtoto wa Sheikh Abdullah
bin Abu Bakar Bakathir (1860-1925), mwanafunzi wa Sheikh
Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait.
Sheikh Abu Bakar bin
Abdullah bin Bakathir aliyejifunza kutoka kwake elimu ya
Fiq'hi kupita Maulamaa wengi hapo Zanzibar, alikuwa
akihudhuria darsi za Sheikh Abdullah Saleh Farsy kwa
ajili ya kumpa moyo, kisha akamchagua kuwa Imamu wa
Swalah ya Witri kutoka mwaka 1933 mpaka terehe 28
October 1939, alipomruhusu pia kusoma Qur-aan katika
Msikiti Gofu na hatimaye akawa anasalisha Swalah ya
Alfajiri mpaka mwaka 1966 alipochukuwa mahali pake mtoto
wa dada yake Saleh bin Salim bin Zagar.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
alisoma vitabu vingi vya Fiq'hi kutoka kwa Sheikh
Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy vikiwemo vitabu vya
Fathul Muin na Iqnai, ambavyo mwanzo vilikuwa
vikisomeshwa na Sheikh Abdullah bin Abu Bakar bin
Bakathir hapo Msikiti Gofu katika mwaka 1917.
Alijifunza kutoka kwake pia
elimu ya kupanga nyakati za Swalah na kuujua upande wa
Qiblah.
Juu ya kuwa hapo mwanzo
Sheikh Abdullah Saleh alisoma Minhaaj At Tabiiyn kitabu
cha Sheikh Zakariya Muhyddin Yahya Sharaff ad-Din al-Nawawi
(1213-1277) ambaye ni mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya
Kishafi, lakini baadaye alisoma tena kitabu hicho kwa
Sheikh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy.
Msimamo wa kisheria wa
kitabu hiki hapo Zanzibar umeanzia zama za Imam Abu
Hamid bin Muhammad al-Ghazzali (1058-1111), aliyekuwa
mwanafunzi wa Imam wa Haramayn Ahmed Malik al-Jawayti
(1085) kutoka kwa Ayoub al-Buwati (845), mwanafunzi wa
Imam Muhammad Idriys al-Shafi'i (767-820), mwanzilishi
wa Madrasa ya Shafi'i, yenye wafuasi wengi Zanzibar na
Misri.
Sheikh Muhsin bin Ali bin
Issa Barwan aliyekuwa mwalimu wake Msikiti Gofu, alikuwa
mwanachuoni wa mwanzo katika mwaka 1944 kumruhusu Sheikh
Abdullah Saleh Farsy kusomesha Jalalayn Msikiti Barza
katika mwezi wa Ramadhani. Baadaye Sheikh Abdullah Saleh
Farsy alijifunza kwa Sheikh al-Amin Ali bin Abdullah bin
Nafi al-Mazrui mwaka (1875-1947), aliyeupendezesha kwa
watu Uislamu wa kisasa kama ulivyoshereheshwa na Shekh
Muhammad Abduh (1845-1905), aliyemsomesha Sheikh Ahmed
Muhammad Mlomry katika chuo kikuu cha al Azhar, Misri.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
alipewa Ijaza (shahada) na Sheikh ‘Umar
bin Ahmad bin Abu Bakar al-Sumait (1896) aliyemsomesha
vitabu vya Fiq'hi, Mantiq (Logic) na Hadith,
pamoja na vitabu vingine. Bahati mbaya mwanachuoni huyu
alirudi Yemen katika mwaka wa 1965 kutokana na udikteta
uliokuwepo Zanzibar chini ya serikali iliyoongozwa na
mkiristo Julius Kambarage Nyerere.
Umahiri aliouonyesha Sheikh
Abdullah Saleh Farsy katika elimu ya mambo ya kidunia
ulikuwa mkubwa pia. Alikuwa hodari sana katika elimu
hiyo, na alipokuwa Central Primary School aliyojiunga
nayo mwaka 1924, mwalimu wa lugha ya Kiingereza
alishindwa kuamua darasa lipi ampeleke. Sheikh Abdullah
Saleh Farsy aliyemaliza miaka minane inayotakiwa katika
shule ya msingi katika muda wa miaka mitano tu.
Miongoni mwa walimu wake
maarufu alikuwa Sheikh Abdullah bin Ahmed bin Seif
(1900-1940) na Sheikh Abdul Bary kutoka chuo kikuu cha
Al-Azhar aliyeajiriwa na Sayyid Ali bin Humoud mwaka
(1902-1911).
Qur-aan Takatiku
Aliandika tafsiri yake ya
Qur-aan Takatifu kuanzia mwaka wa 1950 hadi mwaka 1967,
wakati fikra za umoja wa Kiislamu na Uislamu wa kisasa
ulipokuwa ukifanyiwa kampeni kubwa hapo Zanzibar.
Wakati huo huo Tafsiri hii
ilikuwa ni jibu la tafsiri ya Qur-aan Tukufu
aliyoiandika Padri Godfrey Dale kwa ajili ya
kuwawepesishia wahubiri wa Kiafrika walioajiriwa na
University Mission to Central Africa (UMCA),
iliyoanzishwa mwaka 1873 na Padri Dr. David Livingston
(1813-1873) huko Zanzibar.
Tafsiri ya Padri Dale
iliyoandikwa kwa Kiswahili cha Kiunguja ilikuwa na
kurasa 542 pamoja na kurasa 142 za sharhi, ilipigwa
chapa mwaka 1923 huko London na jumuiya ya kueneza elimu
ya Kikristo (Society for Promoting Christian
Knowledge).
Kwa vile tafsiri hiyo
iliandikwa kwa njia ya kuutetea Ukristo, jambo
lisilokubalika kwa Waislamu, Sheikh Mubarak bin Ahmed
bin Ahmad, mkuu wa Makadiani Afrika Mashariki (Ahmadiyah
Muslim in East Africa) aliamua kuanza kuandika
tafsiri yake mwaka 1936 iliyokubaliwa na kutambuliwa na
wamisionari hapo Zanzibar.
Katika mwaka 1942 nakala ya
tafsiri ya Makadiani iliyopigwa taipu ilipelekwa mbele
ya kamati ya lugha ya Kiswahili (Inter-Territorial
(Swahili) Language) kwa ajili ya kukubaliwa
rasmi kilugha. Na katika mwezi wa April mwaka 1944,
kamati ilijibu kwa kuikubali lugha iliyotumika ikitaka
baadhi ya marekebisho kufanyika. Juu ya kuwa masahihisho
yote hayakufanyika kama ilivyotakiwa, tafsiri hiyo
ikapelekwa mbele ya baadhi ya viongozi wa Makadiani wa
Afrika ya Mashariki na kukubaliwa kuwa lugha iliyotumika
ni nzuri na yenye kukubalika.
Sheikh Amri bin Abeid
(1924-1964), aliyejifunza Ukadiani huko Pakistan mwaka
(1954-1956) alijaribu kuitetea tafsiri ya Makadiani,
lakini tafsiri hiyo iliyopigwa chapa kwa mara ya mwanzo
mwaka 1953 ilisababisha mgogoro mkubwa kutoka kwa
Masunni waliowatuhumu Makadiani kuwa wamebadilisha na
kugeuza baadhi ya maneno kwa kusudi la kuunga mkono
fikra zao.
Ili kupambana
na tafsiri za Wakristo na Makadiani zilizogeuzwa na
kubadilishwa ilionekana kuwepo umuhimu na dharura ya
kupatikana tafsiri yenye kutambuliwa rasmi. Jukumu hilo
akabebeshwa Sheikh Abdullah Saleh Farsy, aliyekuwa
akimuomba Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu asife kabla ya
kuikamilisha tafsiri hiyo.
Fikra hii adhimu ilianza
baada ya Sheikh kupiga chapa kitabu chake cha mwanzo
kiitwacho 'Maisha ya Mtume Muhammad' (Swallah Llahu
alayhi wa Sallam) kilichofuatiliwa na kitabu cha
Sura za Swalah na Tafsiri zake mwaka (1950).
Kabla ya kudhihirisha
kutoridhika kwake na tafsiri ya Makadiani katika
kijitabu kidogo ‘Upotofu wa Tafsiri ya Makadiani’,
Sheikh Abdullah Saleh alikwishawahi kuandika tafsiri na
sharhi ya Surah Yaseen, Al-Waqiah na Al- Mulk
kilichopigwa chapa na A.A. Vasingstake, Uingereza na
kutolewa mwaka 1950 Zanzibar.
Tafsiri yake aliyoiandika
kwa kuitegemea zaidi tafsiri ya Jalalayn ilianza kupigwa
chapa juzuu baada ya juzuu, na baina ya mwaka 1956 na
1961 juzuu kumi na mbili zilikwishapigwa chapa.
Kutokana na upungufu wa
fedha, tafsiri iliyokamilika ilipigwa chapa mwaka 1969
na wadhamini walikuwa The Islamic Foundation.
Msaada mkubwa uliotolewa na
Sultani wa Qatar, Sheikh Ahmad bin Ali uliwezesha
kugawiwa bure misahafu 4,000 na kuuzwa misahafu mingine
3,000 kwa bei nafuu ya shilingi kumi tu.
Kuanzia mwaka 1950 hadi
1960 kampeni kubwa dhidi ya Makadiani ilifanywa na
Jamaat al Islam huko Pakistan chini ya uongozi wa
Sheikh Maududi (1903-1979) aliyezikaribisha juhudi kubwa
za Sheikh Abdullah Saleh Farsy, juu ya khitilafu
iliyokuwepo baina ya misimamo ya Zanzibar na Pakistani,
kwani Sheikh Abdullah Saleh Farsy hakuwa akiona tofauti
yoyote baina ya Makadiani na Ahmadiya waliojitenga na
Makadiyani. (Ahmadiya ni kundi lililojitenga na
Makadiani kutokana na baadhi ya khitilafu baina yao)
Islamic
Foundation
ya Nairobi yenye kuunga mkono Jamaat al Islam ya
Pakistan, ndiyo iliyopiga chapa kwa mara ya mwanzo
Tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Farsy, aliyeandika kuwa
Maududi ameikubali tafsiri yake ya QURANI TAKATIFU. Na
Sheikh Abdullah Saleh Farsy naye alieleza kuikubali
kwake tafsiri ya Maududi inayoitwa 'Qur'an Fahmi Ke
Bunyadi Usul' (Msingi wa kuifahamu Qur-aan), na
akaruhusu uandikwa utangulizi wa Tafhim Al-Qur-aan
katika Qurani Takatifu.
Mafundisho yake
Kuanzia tarehe 7 Januari
1960 hadi 19 Februari 1960 Sheikh Farsy alikuwa
safarini Nyasaland 'Malawi' na Rhodesia ya Kusini akitoa
darsa na kuwahutubia Waislamu na kuwanasihi juu ya
umuhimu wa kujifunza masomo ya dini.
Tarehe 11 April 1960 baada
ya kurudi kutoka Nyasaland, Sheikh Farsy aliandika
ripoti aliyoeleza ndani yake umuhimu wa mafunzo ya dini.
Aliwataka wanaohusika kutilia nguvu umuhimu wa kuwapatia
Waislamu elimu katika skuli za serikali.
Aliandika:
"Kwanza, upeo wa elimu ya
watoto wa Kiislamu ni duni ukilinganisha na wasiokuwa
Waislamu katika Nyasaland. Kuwepo kwa jamii mbili katika
nchi, mojawapo imeelimka na nyengine haijaelimika ni
hatari kwa serikali na kwa jamii. Serikali ni baba wa
wananchi wote, na kwa ajili hiyo inapaswa kutopendelea
upande mmoja."
Aliendelea kueleza:
"Serikali inatoa misaada
mbali mbali kuipa skuli za wamishionari bila ya
kuzilamisha kujiunga na skuli za serikali. Jukumu la
serikali ya Nyasaland lazima liwe kuinyanyua daraja ya
elimu kwa Waisalmu iwe sawa na ile ya jamii nyingine
nchini.”
Matakwa ya Sheikh Farsy juu
ya kuelimishwa Waislamu hayakuwa kutaka wajengewe skuli
zao tu, bali yalikuwa makubwa kuliko hivyo. Alitilia
mkazo jambo la kuajiriwa waalimu wa dini ya Kiislamu
katika skuli za serikali pia. Alisema: "Shule za
serikali hazina budi kuwa na walimu watakaosomesha
mafunzo ya Kiislamu wenye kulipwa na serikali.
Inashangaza kuona kuwa waalimu wa Kikristo katika shule
hizo wanalipwa na serikali wakati waalimu wa Kiislamu
wanalipwa na jamii. Haya hayafahamiki."
Kupitia darsi zake za
misikitini na kwa njia ya vitabu, Sheikh Farsy alitumia
juhudi zake zote katika kuwaelimisha vijana misingi
asili ya Kiislamu. Alihimiza na kutilia nguvu umuhimu wa
kufufua, kufuata na kuyafahamu mafundisho sahihi ya dini
kama yalivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam) na Sahaba zake (Radhiya
Llahu anhum) pamoja na mafundisho ya watu wema
waliotangulia 'Salafus Swaalih'.
Mafundisho haya yalikuwa
yakifundishwa kabla yake na Sheikh Al-Amin na Sheikh
Muhammad Kassim hapo Mombasa.
Lengo la
Sheikh Farsy lilikuwa kubwa kupita wadhifa wake wa Kadhi
mkuu wa Kenya. Lengo lake lilikuwa ni kupata jukwaa
litakalomwezesha kuifufua na kuieneza elimu sahihi ya
dini kama ilivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam), na kuwakataza watu kufuata
uzushi ‘bid’aah’ na itikadi zisizo na misingi ya
Kiislamu, na mambo yaliyo batili ambayo hao wanaoyaeneza
wanajaribu kuyanasibisha na Uislamu.
Sheikh Farsy alifanikiwa
kiasi kikubwa sana, na watu wengi waliokuwa wakihudhuria
darsa zake walikuwa wakihisi kuwa mafunzo yake yanaingia
moja kwa moja ndani ya nyoyo zao. Kwa juhudi zake,
alifanikiwa kuanzisha kizazi kilichoiendeleza kazi yake
hiyo ya kupiga vita uzushi na ushirikina, na kufanikiwa
kuondoa itikadi nyingi ambazo watu wakati huo walikuwa
wakidhani kuwa yamo katika dini.
Safari zake
Baada ya kukamilisha
masosmo yake katika Chuo cha Ualimu 'Teachers
Training College (TTC)', Sheikh Abdullah alisomesha
shule za msingi kuanzia mwaka 1932 hadi 1947, na
kutokana na jitihada zake kubwa katika kazi, alipewa
cheo cha Mkaguzi mkuu wa shule za msingi za Unguja na
Pemba kuanzia mwaka 1949 hadi mwaka 1952. Kisha akapewa
cheo cha Principal wa Muslim Academy Secondary School
kuanzia mwaka 1952 hadi 1956 kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwalimu
mkuu 'Headmaster' wa Arabic Medium School
kuanzia mwaka 1957 hadi 1960.
Mwezi wa Machi mwaka 1960,
Sheikh alikwenda kuhiji na katika mwaka wa 1967
alijiuzulu kazi katika Wizara ya Elimu alipokuwa mwalimu
katika Chuo cha Ualimu 'Teachers' Training College.
Katika mwaka 1960,
alichaguliwa kuwa Kadhi mkuu wa Zanzibar, na aliendelea
na kazi hiyo muda wa miaka saba, mpaka alipoamua kuiacha
na kuhamia Kenya baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964
yaliyosababisha umwagaji mwingi wa damu huko Zanzibar
pamoja na kukamatwa na kutiwa ndani bila sababu kwa
viongozi wengi wa kisiasa na wa kidini.
Mwenyeji wake huko Kenya
alikuwa Sheikh Muhammad Kassim al-Mazrui, sahibu yake wa
zamani tokea waliposoma pamoja chini ya mwalimu wao
Sheikh al-Amin bin Ali al-Mazrui, aliyekuwa akifundisha
dini huko Zanzibar.
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
hakuwa mgeni huko Kenya ambako sifa zake kuwa
mwanachuoni mkubwa zilitangulia kufika kabla yake.
Sheikh Muhammad Kassim al-Mazrui ndiye aliyempendekeza
kwa Rais Jomo Kenyatta kupewa cheo cha Kadhi mkuu wa
Kenya, jambo ambalo Rais Kenyatta alilikubali bila
kipingamizi.
Kwa muda wa miaka 14
alikuwa Kadhi mkuu wa Kenya, daraja yenye heshima kubwa
sana aliyoitumikia kwa muda wote huo kwa ikhlasi, hekima,
uwezo wa hali ya juu, na uerevu mkubwa sana mpaka
alipoamua kustaafu katika mwaka 1980.
Kifo chake
Sheikh Abdullah Saleh Farsy
alifariki dunia tarehe 9 Novemba mwaka 1982 karibu miezi
minane tokea alipoondoka Kenya kuelekea Muscat - Oman
kwa ajili ya kuungana na aila yake.
Huzuni kubwa iliyoingia
nyoyoni mwa Waislamu wa Afrika Mashariki kutokana na
kifo chake itaendelea muda mrefu sana, na pengo lake
kamwe si rahisi kuzibika, na watu wataendelea kufaidika
na elimu aliyowarithisha daima milele.
Wadhifa zake
·
Mwalimu – Shule za msingi
(1932 - 1947)
·
Mkaguzi mkuu wa Shule za
Msingi - Zanzibar na Pemba (1949 - 1952)
·
Principal - Muslim Academy
Secondary School (1952 - 1956)
·
Mwalimu mkuu - Arabic
Medium School (1957 - 1960)
·
Kadhi mkuu wa Zanzibar
(1960 - 1967)
·
Mwalimu - Teacher Training
College (? - 1967)
·
Kadhi mkuu wa Kenya
(1974 - 1980)
Darsi zake
Alipokuwa Mombasa, Kenya
Sheikh Farsy alikuwa akitoa darsa zake katika misikiti
ifuatayo:
·
Msikiti Sakina (Majengo)
kila Jumanne
·
Msikiti Al-Azhar (Guraya)
kila Al Khamisi
·
Msikiti Shihab (Mwembe
Tayari) kila Jumatano
·
Msikiti Mlango wa papa (mji
wa Kale) Jumatatu
·
Msikiti Ridhwaan (King’orani)
Ijumaa
·
Msikiti Muhammad Rashid (Kaloleni
Mazui) Jumatatu-mara moja kila mwezi
·
Tunah (Majengo) Ijumaa moja
·
Msikiti Nur (Ijumaa moja)
·
Malindi,
Kenya
·
Msikiti Sheikh Nassor. (Jumamosi
baada ya Swala ya Magharibi)
Vitabu vyake:
·
Tafsiri ya Qurani Takatifu.
Ilipigwa chapa mara ya mwanzo mwaka 1969
·
Maisha ya Nabii Muhammad
·
Mawaidha ya Dini
·
Tarehe ya Imam Shafi na
Wanazuoni wakubwa wa Afrika ya Mashariki
·
Baadhi ya Wanachuoni wa
Kishafi wa Mashariki ya Afrika.
·
Sayyid Said bin Sultan
·
Urathi
·
Jawabu za Masuala ya dini
(sehemu ya kwanza, pili na tatu)
·
Tafsiri ya Suratul Kahf na
hukumu ya swala ya Ijumaa
·
Sura za swala na tafisir
zake
·
Swala na maamrisho yake
·
Ndoa na maamrisho yake
·
Saumu na maamrisho yake
·
Mambo anayofanyiwa Maiti na
Bidaa za Matanga na hukumu za Eda
·
Bidaa I na II
·
Khitilafu za Madhehebu Nne
katika swala
·
Sifa za Mtume, mawaidha na
Dua
·
Mashairi I-II
·
Maisha ya Sayyidnal Hassan
·
Maisha ya Sayyidnal Hussein
·
Utukufu wa swala na namna
ya kusali
·
Mafunzo ya dini
·
Tafsiri ya Maulidi Barzanji
neno kwa neno
·
Wakeze Mtume wakubwa na
wanawe wengine
·
Wakeze Mtume wadogo
·
Tafsiri ya Baadhi ya Sura
za Qurani: Yasin, Waqia na Mulk Sayyidna Khalid bin
Al-Walid
·
Vyakula alivokula Mtume
·
Tunda la Quran
·
Upotofu juu ya Tafsiri ya
Makadiani
·
Kisa cha Miraji
·
Maisha Ya Mtume Muhammad
Vitabu vya Kiarabu:
·
Al-Busa’idiyyun hukkam
Zinjibar. Muscat: Ministry of National Heritage and
Culture 1982.
Vitabu vyake visivyopigwa
chapa: (kiarabu)
·
1. Inayatullaahi al-adhym
bi al Qurani al-Karim
·
2. Irfaani al ihsaan bi
tarjamati al qarii Hafs bin Suleiman
·
3. Nuru al basira wal al
basar fi taraajimi al quraa al arba’atashar
·
4. Al khulafau al Amawiyin
[28] |