|
Ndugu Waislam, baada ya kuuaga mwezi
mtukufu wa Ramadhaan, ambao umejaa fadhila nyingi na kheri
zisizopatikana katika miezi kumi na moja iliyobaki, kuna
umuhimu mkubwa wa kuendeleza zoezi hili la Funga baada ya
mwezi huu mtukufu hususan, na kwa mwaka mzima kwa ujumla
InshaAllah.
Swawm kwa ujumla na Swawm za Sunnah haswa ni jambo kubwa
sana la kiibada. Na ni bora sana ieleweke ndugu zangu, kuwa
Swawm si Ibada ifanyikayo katika mwezi wa Ramadhaan pekee,
bali ni jambo ambalo linalofanyika mwaka mzima katika
nyakati mbalimbali kama tutakavyoona katika makala haya.
Kama ilivyo katika Ibada ya Swalah, kuna Swalah za Sunnah au
Rawaatib au Nawaafil, ambazo ndizo zitakazokuwa viraka siku
ya Qiyaama wakati zile Swalah za Fardh zitakapopelea katika
Mizani. Nazo Swawm za kujitolea au za Sunnah, ndizo
zitakazomuongezea mja thawabu na ujira pamoja na ile Swawm
yake ya Fardh ambayo ni Ramadhaan.
Hapa chini tutaziorodhesha Swawm za SUNNAH ambazo Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kazipendekeza kwetu
tuzitekeleze:
SWAWM YA SIKU SITA ZA MWEZI WA SHAWWAAL
Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa
Ramadhaan na siku ya 'Iyd ul Fitr. Na Mtume(Swalla Allahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) anasema:
))
من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر))
رواه
مسلم و الترمذي و ابن ماجه, أبو داود و أحمد
.
((Atakayefunga mwezi wa Ramadhaan, kisha akafuatia kwa
kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira
wa aliyefunga mwaka mzima)). Imepokewa na Maimaam Muslim,
At-Tirmidhy, Ibn Maajah, Abu Dawuud na Ahmad.
Maulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka
mzima kwa atakayefunga Ramadhaan na siku sita hizo za
Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi,
kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhaan atapata ujira
mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za
Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo
300+60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa
mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa
kuifunga Swawm hii ndugu zangu.
SWAWM YA SIKU YA 'ARAFAH (Kwa wale wasio katika
Hajj)
Hadiyth ifuatayo inaonyesha uzito na muhimu wa Swawm ya siku
hiyo:
عنْ أَبي قتَادةَ رضِي اللَّه عَنْهُ ، قالَ
:
سئِل رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ
وسَلَّم : عَنْ صَوْمِ يوْمِ عَرَفَةَ ؟ قال
:
(
…
يكفِّرُ
السَّنَةَ المَاضِيةَ وَالبَاقِيَةَ
((
رواه مسلمٌ
.
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba
aliulizwa Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Swawm ya 'Arafah akasema
((Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka uliopo))
Muslim
SWAWM YA SIKU TATU KATIKA KILA MWEZI
'AYAAMUL-BIYDH'
Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alisema:
))من
صام
ثلاثة أيام من كل شهر فذلك صوم الدهر فأنزل الله عز وجل تصديق
ذلك في كتابه { من جاء بالحسنة فله عشر أمثالها } فاليوم بعشرة
أيام))
رواه
الترمذي
قال
الشيخ الألباني : صحيح
((Yeyote atakayefunga kila mwezi siku tatu,ni sawa amefunga
mwaka mzima, kisha Mwenyeezi Mungu akashusha Aya
ithibitishayo maneno ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) isemayo: ((Atakayetenda jambo zuri basi
malipo yake ni mara kumi mfano wake}}. Siku moja kwa malipo
ya siku kumi))
Imepokewa na At-Tirmidhy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa
ni Sahihi
Ukiitazama hadithi hii, utakuta makusudio yaliyotajwa kuwa
malipo ya Funga hiyo ya siku tatu za kila mwezi, ni sawa na
ya mwaka mzima, ni kuwa, ukipiga hesabu ya hizo siku tatu za
kila mwezi, mara miezi kumi na mbili ya mwaka, ni sawa na
siku 36.
Na siku hizo 36 mara 10 ambazo ndizo malipo ya kila siku kwa
mara kumi, basi utapata jumla ya siku 360 ambazo ni takriban
idadi ya mwaka mzima wa Kiislam. Fadhila zilizoje na Ujira
mrahisi kiasi gani wa kuuchuma ndugu watukufu!
Masiku haya matatu, Masiku Meupe ''Ayaamul-Biydh'',
yametajwa katika hadiyth ifuatayo:
Abu Dharr Al-Ghifaariy anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
))يا
أبا ذر
إذا صمت من الشهر ثلاثة أيام فصم ثلاث عشرة وأربع عشرة وخمس
عشرة))
رواه
الترمذي قال الشيخ الألباني: حسن صحيح
((Ee Abu Dharr! Endapo utafunga siku tatu za kila mwezi,
basi funga siku ya 13, ya 14, na ya 15))
[Hizi huitwa 'Ayaam ul Biydh' Masiku Meupe kwa sababu
katika masiku hayo kunakuwa kweupe zaidi kwa mwanga wa
mbalamwezi]. Imepokewa na At-Tirmidhy na kasema Shaykh Al-Albaaniy
kuwa ni Sahihi
SWAWM YA JUMATATU NA ALKHAMIYS
عن
أبي هريرة رضي الله عنه قال: كان رسول الله صلى الله عليه
وسلم يصوم الإثنين والخميس وعندما سئل قال: (( تُعْرَضُ
الْأَعْمَالُ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ وَالْخَمِيسِ فَأُحِبُّ
أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ }))
رواه
الترمذي وقال حديث حسن
Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu)
anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alikuwa akifunga Jumatatu na Alkhamiys. Alipoulizwa
sababu ya Swawm katika siku hizo, akajibu: ((Matendo ya
Wanaadam huwekwa mbele ya Mwenyeezi Mungu kila siku ya
Jumatatu na Alkhamiys, nami napenda matendo yangu yawekwe
mbele ya Allaah nikiwa nimefunga)). [Imepokewa
At-Tirmidhy na kasema ni Hadiyth Hasan]
SWAWM YA SIKU YA TASU'AA NA 'ASHURAA
Hizi ni Swawm za siku ya tisa na ya kumi ya mwezi wa
Muharram (Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislam). Hizi
ni Swawm kwa kumbukumbu na kumshukuru Allaah (Subhaanahu Wa
Ta'ala) kwa kumuokoa Nabii Muusa (‘Alayhis-Salaam) pamoja na
watu wake, kutokana na Fir’auni na jeshi lake.
SWAWM NYINGINEZO
Swawm katika mwezi wa Muharram zina fadhila nyingi kama
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alivyomwelezae Abu Hurayrah. ia Swawm katika mwezi wa
Sha'aban, ambapo Bi 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) anasema
kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa akikithirisha sana kufunga.
NIA
Swawm kama amali zingine, ni lazima kuwepo na Nia ndani yake.
Nia katika Swawm za Sunnah ni tofauti na Nia katika Swawm ya
mwezi wa Ramadhaan, Mwezi wa Ramadhaan Mtu anatakiwa anuie
kabla ya alfajiri. Lakini katika Swawm za Sunnah, Nia Mtu
anaweza kunuia wakati wowote, hata mchana wa Swawm maadam
hajala au hajafanya chochote kiharibishacho Swawm toka
alfajiri.
Ushahidi wa jambo hili ni maelezo ya Mama wa Waumini,
Bibi 'Aaishah (Radhiya Allahu 'anha)
aliposimulia kuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) aliwajia siku moja na kuwaauliza je, mna chakula
chochote hapa nyumbani? Tukasema: Hakuna! Akawaambia: Basi
Nafunga! Na siku nyingine alikuja akiwa amefunga (Swawm ya
Sunnah), na sisi tulikuwa tumepewa zawadi ya 'Hais' (aina
ya chakula alichokuwa akikipenda), nikamwambia Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa tuna 'Hais'
tumezawadiwa hapa, nimekubakishia je, unataka?
Akasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
'Kisogeze hapa, ingawa nilikuwa nimeamka na Nia ya kufunga
lakini nitafungua na kukila'. Kisha akasema Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 'Mfano wa Swawm ya
kujitolea (Sunnah) ni sawa na Mtu ana pesa zake, kisha akawa
na khiari ya kuzitoa Sadaka au kutozitoa"
Imepokewa na Imaam Ibn Maajah.
MUHIMU:
Ni bora watu wafahamu kuwa Nia pahala pake ni moyoni, na si
kutamka, ukishapitisha uamuzi wa kufunga, basi hiyo yatosha
na sio kukariri maneno au kutafuta mtu akufundishe namna ya
kuitamka Nia kiarabu au vinginevyo kama wanavyodhania baadhi
ya watu.
Wa
Allaahu A’alam, wa BiLlaahi At-Tawfiyq
|