TAWHIYD
    Tawhiyd

Qur'aan

Sunnah

Fiqhi

Makala

Nasiha Ya Ijumaa

Dua na Adhkaar

'Aqiyda-Tawhiyd

Vitabu

Darsa za Wanawake

    Sikiliza

Qur'aan

Mawaidha

Dua

Nashiyd

    Tizama

Video

 »  Nasaha  
 

UJANJA WA KUTENGANA (SEPARATION)

 

Assalaam Alaykum!

Ndugu zangu waislam suala hili limekuwa likijitokeza na kuulizwa katika sehemu nyingi hapa Uingereza ambazo waislamu hukusanyika kwa ajili ya mikusanyiko ya kidini na kutafutiwa hukumu yake. Wengine hujaribu kuvuka bahari na kujaribu kuwauliza masheikh tofauti sehemu mbali mbali duniani kujaribu kupata “fatwa” .Hivyo baada ya kukaa na kulitafakari sana suala hili tumeona tutoe makala juu ya kadhia hii nzima chimbuko, faida, athari na madhara yake kwa mfumo mzima wa maisha ya ndoa ya muislam.

Ingawa suala hili ni nyeti kwa baadhi yetu lakini unyeti wake sidhani kwamba utamzuia muislamu kulizungumzia huku tukiona mmomonyoko wa kimaadili ukiendelea na kuharibu jamii zetu huku tukichelea kujaribu kulizungumzia. Pia kulijitokeza kauli kwamba kwa nini tunakuwa na hamu sana kuyazungumzia masuala kama haya wakati kuna mengine ya kimsingi lakini tunakuwa wazito au woga kuyakemea kwasababu yanatugusa. Binafsi, Wallahu A’alamu, sidhani kama ni sababu kwani kama tulivyoainisha mwanzoni kwamba chimbuko la makala hii ni kukithiri kwa masuala yanayohusiana na kadhia hii .

Lengo la makala hii ni kujaribu kuwazindua na kuwaamsha waliolala na kuwanufaisha wale watakaowaidhika na kuwa ukumbusho kwa kila aliyehusika kwa njia moja au nyengine katika kadhia hii .

Imebidi tuuite ujanja kwani ndiyo hali halisi. Ujanja huu ambao mke na mume huufanya kwa kudai mbele ya serikali kutengana na hali halisi ni kwamba si kweli ila ni mbinu tu ya kupata unafuu wa maisha . Na baada ya kufanyika ujanja huu baadhi ya waislam hurudi tena nyuma na kujaribu kuangalia hukmu yake katika uislam je inakubalika? .Suala jengine ambalo linajitokeza katika kadhia hii ni ile ndoa iliyokuwepo kabla ya ujanja huu bado itaitwa ndoa au kitakuwa kitu chengine tukimaanisha mke kaachika ,ndoa ile bado ipo au imebatilika au…….? Na labda kwa kuwa hawa wanandoa walikubaliana kufanya ujanja huu kwa pamoja , je utakuwa na athari yoyote kwenye ndoa yao halali?

Kwanza kabisa kabla ya hata kuingia katika kadhia yenyewe ambayo tayari imeweza kujipenyeza na kuenea katika jamii yetu kwa kasi sana na kudiriki kusema asilimia kadhaa ya zinazoitwa “ndoa” basi zimo katika mfumo huu. Yaani kiserikali wametengana lakini hali halisi wanaishi pamoja kiada. Au kiserikali hata hawaishi pamoja kumbe huku pembeni ni mke na mume. Tunaita kiada kwani kisheria hatuwezi kuwa na uhakika wa moja kwa moja kwamba ndoa bado ipo au laa.

Hivyo kwa kujaribu kupata ufafanuzi wa kadhia hii ni vyema tukaangalia kwa hawa wenyewe wazungu ni nini maana ya kutengana.

Judicial separation (Kutengana kwa kisheria) ni kule kutengana kwa mke na mume na hivyo kuondokana na ule wajibu wa kuishi pamoja bila ya kubatilisha ndoa au kuachana.Sababu zinazoruhusu wanandoa kutengana kubwa ni mbili nazo ni ukatili(uonevu) na uzinifu (kutembea nje ya ndoa).Baada ya mwaka 1976 sababu hizi zilibadilishwa na kuwa: uzinifu (kutembea nje ya ndoa), tabia isiyoweza kuvumilika, kutoishi nyumba moja kwa muda mrefu zaidi ya miaka miwili.

Kutengana (Separation) katika utamaduni wa kizungu ni kuwa haina maana ya talaka. Bali ina maana ya kutengana kweli kweli, nakusudia kusema kuwa hawa wenye ku-declare separation huwa hawaishi tena pamoja, na huku kutoishi pamoja ndipo pahala tunapopataka hasa, na mara nyingi huko kutengana kwao huwa ndiyo mwanzo wa process ya talaka ,hutengana kwanza na baada ya kupita muda na taratibu za kisheria mwishowe huachana. 

Nayo ni aina mbili:

1.Ya muda  (Temporary)
2.Ya kudumu (Permanent)

Sasa turudi kwa hii aina yetu mpya ya kutengana inaingia katika maana iliyotajwa hapo juu au laa?

Ukiiangalia aina yetu unaikuta haimo katika zote hizi mbili si ya muda na wala si ya kudumu lakini kauli ya kwamba tumetengana imetamkwa ila wanandoa huwa wanaishi kama walivyokuwa, kama kwamba hakuna kilichotendeka.

Na kuna aina nyengine ambayo si kutengana bali ni kudanganya na kusema uongo .Kwamba mke na mume wamefanya mambo yao kila mtu kivyake wakati wakijijua kama ni mume na mke.Hawa hawajatengana bali mmoja wao huishi kama single/lone parent kwa mujibu wa serikali na mke na mume, kiadana kikawaida .

Sababu kubwa inayowafanya wanandoa kufanya janja hizi ni kwa kuyaona “maslahi” yafuatayo:

1. Ujanja wa Mume kutotaka kulipa kodi (rent) na council tax ya nyumba.
2. Uchu wa mwanamke kutaka kuwa na kipato kila wiki bila ya jasho.
3. Kuwa na kiakiba cha fedha .
4. Kupata msaada katika suala zima la huduma (nafaqa).

Inawezekana kuwa uchache wa elimu wa hawa watu kuelewa kuwa jukumu la kuwalisha watoto (nafaqa) ni jukumu lililopewa umuhimu wa juu katika dini kwa mzazi mwenyewe limewapelekea kunasa kwenye mtego wa ujanja huu.

Ieleweke kwamba katika Sheria ya ndoa ya kiislam imeeleza vitu viwili kama ilivyotajwa katika Quraan Al Baqarah/229 ni kwamba

الطَّلاَقُ مَرَّتَانِ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ

“…. Talaka ni mara mbili ima tukae kwa wema (na wake zetu ) au kuachana kwa ihsani……...”

Suala la kutengana halikutajwa kabisa. Hivyo suala la kutengana (separation) si suala la kulitafutia hukmu ya kiislam ila tutakacho kitafutia hukmu ya kiislam ni ile kauli iliyotolewa wakati wa kutengana,Kulitamkwa kauli gani, nimekuacha, nimekutenga, nimekukataa, sikutaki,si mke wangu, simjui aliko…..

Na hapo kuiangalia kauli hiyo je itakuwa katika hukmu ya talaka au si talaka? Na hata ikiwa kama ni uongo na si makusudio ya wanandoa kusema hivyo wakikusudia talaka. Lakini kisheria ni wajibu kuiangalia kauli hiyo kwa makini sana na kisha kuipatia hukmu muafaka.

ATHARI ZAKE

Kinachowapelekea watu kuamua kutengana au kutojitambulisha rasmi kwa wahusika kwamba wao ni wanandoa ( kwa wale ambao wameoana lakini walipofika hapa wamekwenda kufanya mambo kila mtu kivyake),kumeleta athari nyingi sana mbaya kwa dini yetu ya kiislamu kwanza na pia kwa jamii zetu kama hizi zifuatazo:

1. Kuwatukanisha wanawake wa Kiislamu rasmi – official- kuwa wanazaa bila ya kuwa na waume, kwani kila wakienda DSS huwa wanasema hawana waume, lakini kila mara huwa wanazaa au hata baada ya miaka miwili au mitatu.Wakati inaeleweka vyema kwamba kuzaa nje ya ndoa kiislamu ni haramu.
2. Kuwadhalilisha wanawake wa Kiislamu mbele ya makafiri official kuwa wao ni malaya hata kama wanajidai
kuwa hawatendi umalaya.Inayotukanwa hapa ni dini ya Allah Subhaanahu Wataala.
3 Kubwa kuliko hayo ni kuutukanisha Uislam na kuwa kuzuizi cha wasiokuwa waislamu kuingia katika dini ya
Allah, kwani wengi hawana nafasi ya kusoma lakini wana nafasi ya kuona, hivyo da’awah ya vitendo
hapa ndio inafanya kazi zaidi ya da’awah ya maneno au maandishi kuwa wanawake wa Kiislamu huwa wanautukanisha Uislam kivitendo wakati wanapokwenda kuomba msaada wakidai kuwa hawana uwezo!.
4 Wanawake kuwa na nguvu na madaraka juu ya waume zao wengine kufikia kuwafukuza hao “waume” kwenye majumba na hapa kugeuza maana halisi ya ile aya ya 34 ya Suuratu Nnisaai


الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاء بِمَا فَضَّلَ اللّهُ بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُواْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ

“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake kwa kufadhiliwa na Allah baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa”

Na kuwa wanawake ni wasimamizi wa wanaume!.Hivyo kwenda kinyume na maagizo ya Allah (Subhaanahu Wataala) pale alipomkabidhi mwanamme jukumu na uongozi wa familia.Tumeona mifano aina kwa aina jinsi mume anavyodhalilishwa na kudharauliwa na mke ambae ni mume mwenyewe aliemhangaikia safari mpaka akafika hapa . Na kibaya zaidi mume kukubali kudhalilishwa huku kwa kuchelea mambo mengi ya kimaslahi ambayo atakuwa hatarini kuyakosa.
5 Kukosekana uadilifu na kuingiwa na mtafaruku katika nyumba kwa kuingiwa na uchu na tamaa ya fedha ambazo hata walengwa wenyewe huwa haziwafikii kwani pesa ya mtoto mara nyingi huitumia mama huku akijua kwamba si yake na “baba” kukataa kutoa huduma akidai si wajibu wake tena kwani DSS ishamvua jukumu hilo alilokabidhiwa na Allah(Subhaanahu Wataala).

MADHARA YAKE.

Baada ya kuona “maslahi” na athari ya ujanja huu basi ni vyema na tuangalie madhara yake na hapo tunaweza na kuwa picha halisi ya je ujanja huu unafaa kufanywa na muislam wa kweli ambae amemridhia Allah(Subahaanahu Wataala) kuwa mola wake na uislamu kuwa dini yake na Muhammad (Sallallahu “Alayhi Wassallam) kuwa ni Mtume wake?

1 Watoto kukosa mwelekeo sahihi wa malezi kwenye nyumba ambayo tayari haijasimama kwa misingi ya kisheria ya ndoa ya kiislam.Tumeona athari hizi katika majumba ambapo tofauti zinazojitokeza kwa wazazi watoto huziona .
2 Kuweza kula, kunywa, kuvaa kwa haramu kwani hatujui pesa ipi ni halali kwetu na ipi ni haramu .
3 Kuharibika /kubatilika kwa ndoa kwani wengine wanaishi tu bila ya kujijua kama ni mume na mke.
4 Uwezekano wa mtu kuwakosa watoto wake mwenyewe endapo mama atafariki na watoto kutokuwa na “baba”(tayari tunayo mifano hai kwani yashatukuta).
5 Hata ikitokezea watoto kuchukuliwa na DSS, jukumu la kuwalea watoto bado lipo palepale kwa mzazi kwa lolote atakalolifanya mtoto hata akiwa hayuko kwenye madaraka yake.

HITIMISHO

Baada ya maelezo na ufafanuzi huu ,turudi tena kwenye kadhia yetu.Ifahamike kwamba Ujanja wa kutengana (Separation) kuwa:
1 Sio talaka wala haina sura wala maana ya talaka kwa mtazamo wa sheria ya Kiislamu. Hata hivyo athari zake ni mbaya zaidi hata kuliko talaka yenyewe kwani talaka inakuwa imejulikana kama hakuna ndoa tena ,lakini sura yetu hii ya kutengana ni balaa tupu hakueleweki kama ndoa ipo au laa. Hawa watakuwa wanasema uongo na kudanganya ni moja katika dhambi za ulimi.
Ndoa hata hivyo ipo kwani hakuna jambo lililofanyika lililobatilisha ndoa hii ila uongo huu unaweza kuiathiri ndoa  kwa kukosa mwenye kuiangalia kwani Allah (Subhaanahu Wataala) anasema  mwishoni mwa aya ya kwanza Annisaa  ya kwamba “...hakika Allah ni mwenye kukuangalieni” Vipi Allah Aiangalie ndoa ambayo haikusimama kwa misingi aliyoileta?
2 Matamshi yaliyotumika au yanayotumika katika kuji- declare huko ndio muhimu kuyatafuta na kuyatazama, kama Mume (mwanamke hawezi kujiacha, kwa maana ya talaka bali yeye huwa na Khul’u) alitumia matamshi ambayo ni miongoni mwa matamshi ya talaka basi hapa ndio patizamwe, je talaka imepatikanwa/ imesibu au haijasibu? Muhammad (Sallallahu ‘Alayhi Wassallam) anasema katika hadithi “ mambo matatu (ukiyafanya kwa ) utani (huwa) ni kweli na (yakifanywa kwa)  ukweli huwa ni kweli; ndoa, talaka na kumrejea mke”


Imam Shafi na Abu Hanifa wanaona talaka haihitaji nia ikitamkwa tu au kuashiriwa basi tayari ni talaka.

Imam Malik  anasema talaka haisibu mpaka iambatane na nia.
Baada ya ufafanuzi huu tunaweza kutoa tahadhari kwa wanandoa hawa isije mpangilio wao huu ukaweza kuathiri ndoa ya kiislamu na kuhesabika kuwa talaka japo hawakukusudia lakini maneno yalitamkwa au kuandikwa na katika suala la talaka kitachoangaliwa je! kulitamkwa talaka ? Bila kujali kama matamshi hayo yalikusudiwa ndoa ya kiislamu au ya kiserikali ambayo kwa mtazamo wa kiislamu si ndoa na wala haina athari  na hivyo matamshi pia hayatokuwa na athari kwa ndoa ya kiserikali lakini yanaweza kuiathiri ndoa ya kiislamu.

3 Hata kama tunasema kuwa walikubaliana, bado jukumu kubwa ni la Mume kwani yawezekana kuwa mwanamke hana budi kutokana na vitisho / hila / mbinu za mumewe ndio akakubali, hivyo mume ndio muhusika wa kwanza na wa mwisho katika hukumu ya ujanja huu.Kwa sababu yeye ndie aliepewa jukumu la kuisimamia familia yake na kuiongoza.


عن عبد الله رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : " كلكم راع فمسؤول عن رعيته فالأمير الذي على الناس راع وهو مسؤول عنهم والرجل راع على أهل بيته وهو مسؤول عنهم والمرأة راعية على بيت بعلها وولده وهي مسؤولة عنهم والعبد راع على مال سيده وهو مسؤول عنه ألا فكلكم راع وكلكم مسؤول عن رعيته " رواه البخاري (
2416 ) ومسلم ( 1829)

Kutoka kwa Abdullah Allah amuwie radhi kwamba Mtume Muhammad (Sallallahu ‘Alayhi Wassallam) amesema :
“Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya mlivyovichunga. Kiongozi anaewaongoza watu ni mchunga na ataulizwa juu wachungwa wake. Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa wake. Na mwanamke ni mchunga kwa nyumba ya mumewe na watoto wake nae ataulizwa juu ya wachungwa wake .Mtumwa ni mchunga katika mali ya bwana wake na anawajibika juu ya mali hiyo. Hakika nyote ni wachunga na na kila mmoja wenu anawajibika juu ya wachungwa wake”
 
Imesimuliwa na Bukhari na Muslim

WITO

Ujanja huu madhara yake ni makubwa mno katika dini na hata dunia yetu kushinda hata “faida” zinazoonekana kupatikana kihali na mali na Allah Subhaanahu Wataala anatuonya kwa ukali kuchunga nafsi zetu pamoja na familia zetu kama anavyosema katika Suuratu Tahreem/6


يأَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ قُواْ أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَاراً وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَـئِكَةٌ غِلاَظٌ شِدَادٌ لاَّ يَعْصُونَ اللَّهَ مَآ أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

Enyi mlio amini! Jilindeni(jiokoeni) nafsi zenu na ahli(familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.
Hivyo tunawaasa kwa nia njema kabisa wahusika waliofanya janja hizi kwa kukusudia,au kwa bahati mbaya au kwa kutokuelewa, kutubia mara moja kwa mola wao na kuondokana na kila aina ya maasi na kuzidi kurudi kwake Subhaanahu Wataala kwa maghfira na toba .

Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’aala atupe nguvu na uwezo wa kuweza kuyaacha yote aliyoyakataza na kufanya kila aliloliamrisha. Amin


Wallahu A’alamu

Abu Ammaar 
 
yasihali@hotmail.com