|
Mtume Muhammad (Sallallahu 'alyhi wasallam) alimwambia Mu'aadh bin
Jabal alipokuwa katika safari ya kuelekea Yemen: "Unakwenda kwa
watu walio miongoni mwa watu wa Kitaab. Itakubidi ulinganizi wako wa
kwanza kwao uwe ni wa kumuabudu Mwenyezi Mungu. Iwapo watamkubali
Mwenyezi Mungu, basi wapashe habari yakwamba Mwenyezi Mungu
Amewafaridhia juu yao, Swala tano katika nyakati zao za asubuhi na
mchana." [al-Bukhari na Muslim]
Hadeeth hii iko wazi. Haihitaji wingi wa maelezo. Mtume (Sallallahu
'alyhi wasallam) aliitekeleza kanuni hii katika harakati zake za
ulinganizi wa Da'wah katika Uislamu. Aliishi Makkah kwa muda wa
miaka kumi na tatu, akiwafunza na kuwaelimisha maswahaba zake
kuhusiana na Imaan na urekebishaji wa itikadi walizokuwa nazo. Hayo
ndiyo malezi waliyo-lelewa nayo maswahaba.
Amesema Jundub ibn 'Abdullah al-bajaly, "Tumejifunza Imaan (kuamini),
kisha tukajifunza Qur'aan ambayo (nayo) ikatuongezea Imaan yetu."
Nae 'Abdullah ibn 'Umar akasema: "Sisi tuliishi kwenye zama za
wakati ambapo mmoja wetu aliipata Imaan mwanzo kabla hajaipata
Qur'aan, na pindi Sura zilipokuwa zikiteremshwa tulikuwa tukijifunza
maamrisho na makatazo yake na mambo yaliyohalalishwa na kuharamishwa
na jinsi ya kukabiliana nayo. Lakini nimewaona watu wengi miongoni
mwao walikuwa wanapewa Qur'aan kabla ya Imaan na akaisoma kuanzia
mwanzo wake hadi mwisho wake asijue maamrisho wala makatazo yake -
bila ya kuwa na mazingatio yoyote ya hiyo Qur'aan. Mfano wake ni
kama mtu aliezitupilia mbali tende zake (usomaji wake wa Qur'aan
haumfaidishi na chochote)."
Hii ndiyo desturi ambayo Mtume Muhammad (Sallallahu 'alyhi wasallam)
aliyo-walelea nayo maswahaba zake: Imaan mwanzo na kisha Qur'aan.
Hii inalingana na alivyoeleza Imaam Abu Hanifah: "Kuifahamu dini
mwanzo (Tawheed) na kisha kuyafahamu ma'alumati yake (ya kisheria)."
Imaan ni sharuti zitakaswe mwanzo na baadae ifuate miradi mengine ya
dini. Akasema nae Imaam ash-Shafi'i, "Mja yoyote atakaemuona
Mwenyezi Mungu na dhambi za aina yoyote, isipokuwa shirk, ni bora
kuliko kuonana Nae (Mwenyezi Mungu) hali ya kuwa juu ya Imani za
uzushi."
Katika lugha ya kiarabu, neno 'Aqeedah limetokamana na neno 'aqadah.
Kilugha (kiarabu) mtu anaweza kusema "'Aqada Kamba" ikiwa kamba
imekazwa madhubuti. Na, "'Aqada bei" au Amekubaliana nae bei, ikiwa
mtu ameafikiana na kuandikishiana mkataba kuhusu mapatano yao ya
kibiashara. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa ta'aalah) akasema
katika Qur'an, (kama ilivyofasiriwa) "Na wale mliofungamana nao
ahadi wapeni sehemu yao ('Aqadat)" [Surat An-Nisaa (4):33]. Na
pia Akasema tena Mwenyezi Mungu, (kama ilivyofasiriwa) "Lakini
atakukamateni kwa viapo mlivyoapa na nia mlioifunga barabara ('Aaqadtum)"
[Al-Maidah (5):89]. Aya hizi zinamaanisha uthibitisho na mafungamano
na kitu fulani kama ilivyobainishwa kwenye aya isemayo, (kama
ilivyofasiriwa) "Na timizeni ahadi mnazozitoa kwa jina la
Mwenyezi Mungu mnapoahidi wala msivunje hizo ahadi baada ya
kuzithubutisha hali mumekwisha mfanya Mwenyezi Mungu kuwa Shahidi
wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua (yote) mnayoyafanya." Mtu
akisema, "Aqadtu kadhaa na kadhaa," maana yake moyo wake umethubutu
juu ya kadhaa na kadhaa.
Kwahivyo 'Aqeedah au I'tiqaad kulingana na wanavyuoni wa ki-islamu
ni: Imani thabiti iliyotulia juu ya moyo wa mtu pasi na kusita-sita
au shaka yoyote. Haihusiki na dhana yoyote, shaka au tuhuma.
Imaam Abu Hanifa akaiita ilimu hii iliyo pana kwa jina la
Fiqh-ul-Akbar ("Ufahamu Mkubwa") ambayo ndilo shina la kuifahamu
dini hii. Na akayaita maarifa ya kisheria (Shar'), ujuzi wa
kitaalamu. Wanavyuoni wengi wa kiislamu hutumia neno Tawheed kwa
kila kinacho-fungamana na kuamini. Hii ni kwa sababu jambo muhimu
zaidi hapa ni msingi wa Tawheed ulio kwenye matamshi ya, "Hapana
apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah."
Kulingana na wao, Tawheed imegawanyika sehemu mbili: Tawheed ya
kusadiki na kukiri na Tawheed ya makusudio na matendo. Tawheed ya
kusadiki na kukiri ni Tawheed ya Upweke wa Mu-umba na Tawheed ya
Majina Yake na Sifa Zake (hapana mshirika katika Uumba wake na ni
Pekee katika majina Yake na Sifa Zake). Tawheed ya makusudio na
matendo ni Tawheed ya Uola au kuwa hapana apasae kuabudiwa kwa haki
isipokuwa Allah (Yeye ndie wa Pekee anaestahiki kuabudiwa kwa haki).
Jee, katika Qur'aan, mas-ala haya yameitwa kwa jina gani?
Qur'aan imeyataja mas-ala haya makubwa kwa jina la "Imaan". akasema
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa-Ta'aalah) (kama ilivyofasiriwa):
"Na namana hivi tumekufunulia wewe (Muhammad) wahyi kwa amri yetu.
Ulikuwa hujui Kitaab ni nini wala Imaan; Lakini tumefanya kitabu
hiki (Qur'aan) ni nuru, ambayo kwa nuru hiyo Tunamuongoza Tumtakae..."
[Ash-Shura :52]
|
 |
|