BismiLlaahi waswalaatu wassalaamu
‘alaa RasuulliLlaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa
ba’ad,
Ndugu Wapenzi
Waislam,
Tunaukaribia
mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Mwezi wenye fadhila tele zisozohesabika
idadi yake. Mwezi ambao ndani yake utakapofunga Swawm yake kwa
Iymaan ya dhati na kuitakidi kuwa kuna malipo, basi utasamehewa
madhambi yako yaliyotangulia. Mwezi ambao haufananishwi na miezi
mingine kwa mavuno na ujira, du’aa ya mfungaji haikataliwi,
anapofunga Muislam huwa na furaha mbili; furaha wakati anapofungua
na furaha wakati anapokutana na Mola wake. Mwezi ambao Swawm
itamuombea shufaa mja siku ya Qiyaamah, itakaposema siku hiyo
kumuambia Allah, “Ee Mola, nimemzuia chakula chake, na matamanio
yake ya kimwili mchana kutwa, basi niache nimwombee shufaa.” *
Mwezi ambao ni
hifadhi na kinga nzito kabisa ya mja kutokana na moto, na harufu ya
mdomo wa aliyefunga (japo atakuwa anapiga mswaki) itakuwa ni bora
kuliko harufu ya misk mbele ya Mwenyeezi Mungu. Atakayefunga siku
moja katika mwezi huo akitaka radhi za Mwenyeezi Mungu na ikiwa hiyo
itakuwa ndio siku ya mwisho ya maisha yake, basi ataingia peponi.
Kuna pepo maalum kwa wale wafungao iitwayo Ar-Rayyaan, ambao
wataingia wao tu, na watakapoingia mlango wake utafungwa na
hatoingia yeyote mwengine. Huo ndio mwezi ambao ni nguzo ya Uislam,
ndani yake kunapatikana usiku mtakatifu ambao ni bora kuliko miezi
elfu moja, katika mwezi huo milango ya pepo huwa wazi, milango ya
moto hufungwa na mashetani hufungwa minyororo. Mwezi utakapofunga
wote, Swawm yake ni sawa na kufunga miezi kumi. Na katika kila
wakati wa kufutari, Allah Huchagua watu wa kuwaweka huru na moto.*
Ndugu Muislam,
baada ya kujua fadhila zote hizo za mwezi huu Mtukufu, badala ya
watu kujiandaa kwa mambo mema ya kheri kama kuanza kujizoesha na
Swawm za Sunnah kama zile za Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe
n.k., au kutoa Swadaqah kwa maskini ili nao wapate maandalizi mazuri
ya mwezi huo wenye baraka, au kujiandaa kwa kufanya mengi ya kheri
ambayo yametanawai, kinyume chake kumekuwa kuna wengi wenye majina
ya Kiislam ambao huukaribisha mwezi huu Mtukufu kwa kila aina ya
maasi kwa jina la ‘Vunja Jungu’ kama ijulikanavyo katika maeneo
mengi Tanzania, au ‘Mfungo’ kama inavyojulikana katika maeneo ya
Sawaahil (pwani) ya Kenya.
Jambo hilo licha
ya kuwa halipo katika Dini yetu hii Safi, Tukufu, bali ni jambo
ambalo haliwezi kufanywa na Muislam mwenye Iymaan na khofu ya Mola
wake na ndio maana tukawaita hao wayafanyao hayo kuwa ni Waislam
jina.
Katika masiku ya
mwisho ya Sha’abaan, na haswa zaidi siku ile ya mwisho, watu hao
hukusanyana na kufanya sherehe (party) kwa kusikiliza nyimbo
na kucheza muziki na kunywa vinywaji vya haramu. Pombe siku hiyo kwa
wale walevi ndio inanywewa kama kisasi, wengine ndio siku ya uzinzi
kwa kuwa Ramadhaan wanaogopa kuyafanya hayo, wale wavuta sigara
ambao kidogo wanachelea kuvuta katika mwezi wa Ramadhaan nao paketi
zitavutwa kwa mfululizo, wala unga hali kadhalika na mengi mengineyo
machafu huwa ndio siku yake rasmi hiyo. Bila kuwasahau wenye kwenda
mapkniki na kutumbua.
Watu hao kwa
kufanya hivyo, wanamkebehi na wamemfanya Mwenyeezi Mungu kuwa ni
Mungu wa Ramadhaan! Ama miezi kumi na moja iliyobaki, huyo Mungu
anakuwa kama hana thamani, au kuwepo kwake kumekuwa si kiutendaji!
Wengine ndio
wanaukaribisha kwa kufanya manunuzi (shopping) ya mikeka ya
kuswalia – maana miezi yote iliyopita, kwao mungu hakuwepo, kanzu
hununuliwa kwa wingi, misikiti huanza kushehena hadi inakuwa kero
badala ya furaha kwa wale wenye kudumisha Swalah za Jama’ah
kwa miezi
yote ya mwaka kwani hata nafasi za mbele walizozoea kuzipata huwa ni
adimu au hata kukosa kabisa kwa hao wavamizi wa Ramadhaan. Vilevile
kina dada waliokuwa hawajui hata kuvaa Hijaab, basi utawaona
wanaanza kununua leso za kujitanda, kanga zimeongezeka biashara,
wanaojitahidi zaidi baibui nazo zimekuwa ni pato kwa wauzaji. Nyumba
mbalimbali utaanza kusikia Qur-aan zikisomwa kwenye maredio, kofia
na kanzu zimeanza kushamiri kwenye miili ya wengine.
Hayo yote ni dhana ya wayafanyayo kuwa ni ‘heshima’ na ‘taadhima’
kwa mwezi huu. Ila walichoghafilika ndugu zetu hao, ni kuwa mafuhumu
hiyo, ni mafuhumu inayoonyesha kuwa katika miezi iliyobaki, hakuna
kinachowapasa wao kufanya hayo, hivyo, kumfanya Mwenyeezi Mungu
Mtukufu, kuwa Kuwepo Kwake na Uwezo Wake, Nguvu Zake na Amri Zake
hazina uzito wowote ila Ramadhaan tu. Nayo ni mafuhumu potofu na
dhana iliyo ovu.
Ni
wajibu wa jamii linapoonekana jambo lolote ovu, kulizuia, kulikemea
au kulikasirikia/kulisusia endapo tutakuwa tupo katika udhaifu wa
kutumia njia mbili za awali. Na hii ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta'ala) kama Anavyosema:
((Na
Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi.
Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Swalah, na hutoa
Zakaah, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Hao Mwenyezi Mungu
Atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye
hekima))
At-Tawbah: 71
Vile vile Hadiyth kutoka kwa Mtume wetu mpenzi (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abu
Sa'iyd
Al-Khudriy
(Radhiya Allahu 'anhu)
ambaye
amesema:
Nilimsikia Mtume
(Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam)
akisema:
"Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu basi akiondoe (akibadilishe)
kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au
kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani
kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani))
Muslim
UONGOFU NI ULE
WA MTUME NA UPOTOFU NI KUZUSHA NA KUFANYA MAASI
Muislamu
inampasa afuate mafunzo yaliyo sahihi na kujiepusha na yasiyo sahihi
kwani kufuata uzushi ni kumpotosha mtu na hatari yake ni kama
alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika
kila khutbah yake:
Akisema katika Khutbah za Ijumaa,
((Amma Ba'ad, hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu
cha Allaah, na uongofu ulio bora ni uongofu wa Muhammad
(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na
jambo la shari kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu))
[Muslim] na katika riwaaya nyingine
((na kila upotofu
ni katika moto))
Na pia alieleza katika Hadiyth nyingine:
((Atakayezusha
katika mambo yasiyokuwa (katika Dini) yetu basi itarudishwa [haitopokelewa]))
Al-Bukhaariy na Muslim
Uzushi huu wa Vunja Jungu ambao ni
mchafu na ovu, ni jambo linalopaswa kukemewa na Waislam wote wa hali
zote; Mashaykh, Maimaam, Maustaadh, walinganiaji na watu wa kawaida.
Katika kila mnasaba na kila khutbah kukemewe hayo hadi jamii ifahamu
ubaya wake na madhara yake na mwisho mbaya ambao unaoweza kumfika
mtendaji wa tendo hilo.
Kila mwenye kuvunja jungu angepaswa
ajiulize wakati anapofikiria kufanya uovu wake, kuwa kufanya hivyo
ni kufuata mafundisho ya nani? Ikiwa hayo hayapo katika Dini,
achilia mbali kumuudhi Muumba. Ajiulize pia, ana uhakika gani wa
kuwa ataishi hadi kuikuta hiyo Ramadhaan?
Je, akichukuliwa katikati ya tendo lake ovu kama hilo anafikiria
khatima yake ni nini? Kuna uhakika gani wa kuufika huo mwezi na
kuumaliza na hata kughufuriwa madhambi hayo aliyoyatenda? Nani
anayemiliki uhai mikononi mwake? Wangapi wenye siha wameondoka na
siha zao? Wangapi vijana wameondoka na ubarubaru wao? Je,
hawajiulizi yote hayo?
Na hao ndugu
zetu wanapofikiwa na mawaidha haya, au wakapata kujua ubaya wa
wayafanyayo, basi wasiwe wenye ukaidi wa kuyafuata na kuyafanyia
kazi. Wasiwe kama watu wa zamani walivyokuwa wakipelekewa Mitume
kuwatoa katika kiza cha kuabudu masanamu na kumshirikisha Allah na
kuwaingiza katika mwanga ya uongofu ulio na hoja za wazi, ikawa kila
wakipewa mawaidha, wao hutaka kubakia katika ujinga na ukaidi wao
{{Na
haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola wao Mlezi ila wao
huwa wenye kuipa nyongo}}
Al-An’aam:4
Na Ndiyo
maana pia wameambiwa baada yao na sisi pia kuwa tuende tukaone hizo
athari za kuangamizwa kwao ili iwe funzo kwetu:
{{Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa
wanaokanusha}}
Al-An’aam:11
Athari zao
hizi nyingi zimejulikana kwetu kutokana na mafunzo haya ya Qur-aan
lakini ni nani mwenye kutaka kutafakari na kujitoa katika upotofu na
kupata uongofu? Anasema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa hao
wasiotaka kupata uongofu ni vipofu wa moyo:
{{Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za
kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho
yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani}}
Al-Hajj:46
Naam ndugu
Waislamu, mwenye kupofoka macho anaweza kuwa na iymaan ya dini,
kwani wangapi waliokuwa vipofu lakini wamepata
hidaaya, wangapi wameweza kuhifadhi Qur-aan na hata kuwa ni
Maulamaa wakubwa wa Ummah na mifano ni mingi. Lakini wangapi
waliokuwa na macho kamili lakini wakawa ni vipofu wa nyoyo; wakiwa
wametawaliwa na upotofu na ufisadi?
KUACHA MAOVU NI
KUFANYA JIHAAD YA NAFSI AMBAYO NI JIHAAD BORA KABISA
Aliulizwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
na
Swahaaba, "Je, Hijrah gani iliyo bora?" Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu:
((Ni kuhama yale Anayochukia Mola wako Mtukufu
((Swahiyh
Al-Albaaniy kutoka kwa An-Nasaaiy
Hivyo mwenye kuacha maovu kama haya ya uzushi wa Vunja Jungu bila
shaka atakuwa amepata daraja ya kufanya Jihaad.
Na
thawabu hizo ambazo usawa wake pia ni wa Hijrah pamoja na Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kuzipata mtu atakapokuwa
katika twaa'a wakati wa fitnah, nao ni kama wakati wetu huu uliojaa
fitnah (mitihani, misukusuko, Uislam kukabiliwa na Uadui ndani na
nje n.k.) kila aina, khaswa kwa zama hizi ni mkorogo ulio katika
Dini wa yale yaliyo sahihi na yaliyo ya uzushi (Bid’aa). Kwa hiyo,
anapojikita mtu katika msimamo thabiti na kujiepusha na fitnah hizo,
bila shaka atakuwa amepata fadhila hizo za Hijrah iliyokusudiwa:
Kutoka kwa Ma'qil bin Yasaar (radhiya Allahu ‘anhu) ambaye amesema:
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Kufanya ibada
wakati wa fitnah, ni sawa na kufanya Hijrah kwangu))
Muslim
Basi na tujiepusha na yote Aliyokataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)
na kuzidisha ibada kwa wingi khaswa katika miezi mitukufu na mwezi
kama huu wa Sha’abaan ambao una fadhila na pia ni ni mwezi ambao
tunategema kughufuriwa madhambi yetu. Kwa nini tujiongezee madhambi
baada ya kughufuriwa? Tumekosa hata chembe cha shukurani kwa Mola
Muumba!
Nyakati hizi ndugu Waislamu tuzitumie katika ibada ili tujichumie
mema mengi, kwani ni nyakati ambazo kwa neema ya Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala) zinatumiminikia kila kukicha, angalau tuzingatie na
kushukuru kama Anavyosema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala):
{{Naye Ndiye Aliyefanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya
anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru}}
Al-Furqaan:62
Ndugu Waislam, kama wanataka kuvunja jungu kama waitavyo hao
wavunjaji, basi kwanini wasifanye kama Maswahaba (radhiya Allahu
‘anhum) ambao walikuwa kila ukikaribia kuingia kwa mwezi wa
Ramadhaan wakizidisha kusoma Qur-aan na wale wenye uwezo kimali
wakitoa mali kuwapa maskini ili kuwapa nguvu (Kujiandaa na mfungo wa
Ramadhaan).
Ni
muhimu kwa Waislamu kufanya maandalizi ya Ramadhaan kwa kujielimisha
juu ya namna ya kuukabili mwezi mtukufu hasa kuelewa maana na
makusudio ya funga, namna ya kufunga kwa kuzingatia masharti, mambo
yanayobatilisha Swawm, pamoja na Sunnah zilizokokotezwa na Mtume
(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha
namna iliyo bora ya kukaribisha funga ya Ramadhaan, hivyo tunapaswa
kufunga Sunnah za Jumatatu na Al-Khamiys pamoja na kuisoma Qur-aan
kwa wingi kama alivyotuagiza.
Vilevile Ramadhaan inapoingia Waislam wanatakiwa wajiepushe kabisa
na mambo yote ya laghwi ambayo hupoteza Swawm kama vile
kuangalia mpira, sinema za kipuuzi, misalsalaati, kucheza bao,
karata, usoro, dhumna, drafti, keramu n.k. Laghwi ni jambo
lolote la kipuuzi ambalo hupoteza muda na kumsahaulisha mja
kumkumbuka Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Katika zama hizi Sunnah zimetengwa
mbali na bid’aah ndizo zenye kufuatwa na kuwa ndio mwendo wa
Waislamu wengi, kwa sababu ya ujinga wa kuigiza tu watu bila ya
dalili, na kutopenda kujifunza mafunzo mema yaliyo sahihi ya
Kiislamu. Mafunzo ambayo yamekamilika na kumfaa kila binaadamu
popote na wakati wowote. Anasema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema yangu,
na Nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini}}
Al-Maaidah:3
Tumuombe Mwenyeezi Mungu Atuthibitishe mioyo yetu katika Iymaan, na
Atuongeze kwenye uongofu, na Atughufurie madhambi yetu makubwa na
madogo. Aamiyn
------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
*
Maelezo yote hayo yametolewa katika Hadiyth Sahihi za Mtume (Swalla
Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika vitabu vifuatavyo:
-
Swahiyhul-Bukhaariy
-
Swahiyhu
Muslim
-
Musnad Ahmad
-
Swahiyhut-Targhiyb
-
Sunnan
An-Nasaaiy
-
Al-Bayhaqiy
-
Silsilatus-Swahiyhah
-
Swahiyhul-Jaami’i
-
Fathul-Baariy