|
“Kwa kila jamii
ya watu kuna sikukuu, na hii ‘Iyd ndiyo sikukuu yetu”
alisema Mtume (s.a.w) kumwambia Abu Bakr (r.a). [Al
Bukhaariy na Muslim].
“Sikukuu yetu”
ina maana kubwa kwa Waislaam, kwa sababu inatujulisha
kwamba hii ni yetu na asili yake imetokea kwenye sharia zetu
tu peke yake. Kwa kuwa sherehe hizi zimeegemea kwenye
taratibu za kidini, ni muhimu sana kuzifafanua ili ziwe na
furaha kubwa na mikusanyiko yenye kuleta hisia ya kuwa hizi
sikukuu ni zetu (sisi Waislaam), na ni tofauti na zile
sikukuu za Mushrikina. Haturuhusiwi kusherehekea Christmas,
Hanuka, au sikukuu za Kipagani, na shukrani zetu zote
tuzielekeze kwa Allaah (s.w.t) peke yake.
Mtume
(s.a.w) ametuamrisha katika hutuba zake nyingi kuwa
tujitofautishe na Mushrikin (Wapagani), na hizi ‘Iyd mbili
ni miongoni mwa sikukuu zile ambazo Mtume (s.a.w) ametutaka
tuchukue tahadhari kubwa ya kujitofautisha sana nao
(Mushrikin). Ndiyo sababu akasema, baada ya kuona watu wa
Madinah walipokuwa na sherehe mbili wakizisherehekea kabla
ya kuja Uislaam, “Allaah (s.w.t)
ameshakupeni nyinyi kilicho bora kuliko vyote (sikukuu):
‘Iyd-l-Adh-haa (ya kuchinja) na ‘Iyd-l-Fitr”. [Ahmad,
Abu Dawuud na An Nasaa’iy].
‘Iyd-l-Adhaa huja baada ya kumalizika ibada ya Hijja na
‘Iyd-l-Fitr huja baada ya kumalizika saumu ya mwezi wa
Ramadhani. Kwa hivyo haishangazi hiyo, ni lazima tuzionyeshe
na tuzifafanue ‘Iyd zetu. Kutokana na bayana hizi zilizo
wazi, Wanavyuoni wa Kiislaam ni lazima watilie mkazo sana
juu ya kuzitofautisha sherehe zetu kutokana na zile za
Mushrikin.
Hii ni
kwa sababu sherehe zina taathira kubwa katika akili na tabia
ya mwanaadam. Kuwa tofauti katika Sherehe vile vile ina
maana kwamba ni lazima tusijishirikishe (tusihudhurie)
kabisa katika sherehe za Mushrikin. ‘Umar (r.a) amesema:
“Msijifundishe lugha ya Mushrikin
– bila ya kuwa kuna umuhimu ndani yake – wala Msiingie
makanisani wakati wa sherehe zao kwa sababu Hasira za Allaah
huteremka juu
yao.”
[Al Bayhaqiy].
Sisi,
Waislaam, huenda hata tufunge (saumu) katika siku za sikukuu
za Mushrikin. Umm Salamah (r.a)
amesema Mtume (s.a.w) alikuwa na kawaida ya kufunga siku za
Jumamosi na Jumapili, na alipoulizwa Alisema: Kuna siku
mbili katika siku za sherehe za Mushrikin kwa hivyo napenda
kwenda kinyume na wao katika sherehe zao”. [Ahmad na
An Nasaaiy].
Kulikadiria wazo hili la kuwa tofauti na Mushrikin, ni
muhimu sana kusema kwamba: Ili tuwe tofauti kwenye sherehe
zetu na katika mwenendo ambao Mtume (s.a.w) ametutaka tuwe
nao, ni lazima tufuate mwenendo wake (Sunnah) kikamilifu.
Kwa kufanya hivyo kutatupatia malipo mema (thawabu) ya kuwa
wafuasi wa kweli wa Mtume (s.a.w).
Kwa
hivyo tukitaka kuwa wafuasi wake ni lazima tuelewe ni yepi
Bid’ah (uzushi) katika sherehe zetu. Bid’ah inakuja pale
Sunnah hutumika mahali pasipo pake!
Ibn Taymiyyah amesema: “
Hakuna nafasi katika moyo wa binaadam kwa yote mawili;
Sunnah na Bid’ah.” [Al-Iqtidhaa]. Allaah (s.w.t)
amesema:
{Sema – Ewe
Muhammad – Ikiwa kweli mnampenda Allaah basi nifuateni mimi,
Allaah Atakupendeni}.
[Aali-Imraan, 3:31]
Ndugu
wapenzi, tunawasilisha kwenu baadhi ya matendo ya Sunnah
katika sikukuu ili muweze kujaribu kuyatekeleza. Vile vile
yanawasilishwa baadhi ya yaliyokuwa Bid’ah ili katika
sikukuu muweze kuyaepuka. Kuna umuhimu mkubwa sana katika
kufuata mwenendo wa Mtume (s.a.w) wa ‘Iyd ili kikweli kweli
tuweze kusema kwamba sikukuu zetu ni tofauti na zile sikukuu
za Mushrikin.
Yaliyokuwa
Sunnah Katika ‘Iyd
1)
Siku
ya ‘Iyd ni Sunnah kuvaa mavazi mazuri kabisa tuliyo nayo.
Imehadithiwa kwamba Ibn ‘Umar alikuwa akifanya hivyo pamoja
na Masahaba wa Mtume (s.a.w). [Fath al-Bariy]
2)
Ni
lazima (Waajib) kusali Salaa ya ‘Iyd-l-Fitr. Mtume (s.a.w)
na Masahaba zake hawakuacha kabisa kufanya hivyo, na vile
vile walikuwa wakiwakusanya watu kuitekeleza Salaa hiyo
wakiwemo wanawake wenye hedhi (hawaingii kwenye kusali
lakini wanashuhudia kheri na du’a kwa Waislamu), watoto na
vikongwe. [Al Bukhaary na Muslim].
3)
Ni
Sunnah kula tende kabla ya kuondoka kuelekea kusali Salaa ya
‘Iyd ili kuonyesha kwamba hatujafunga.
“Mtume (s.a.w) alikuwa hatoki
kwenda kusali Salaa ya ‘Iyd ila baada ya kula tende.”
[Al Bukhariy na Ahmad].
4) Ni
Sunnah kuleta Takbira kwa sauti tunapotoka majumbani mwetu
kuelekeya kwenye Salaa ya ‘Iyd. Mtume (s.a.w) alikuwa
akileta Takbira mpaka anamaliza Salaa.
[Silsilat Al Ahadiyth Swahiyhah -
Sheikh
Al Albaaniy]
5)
Hakuna
Hadiith inayohusiana na Rasuulullaah (s.a.w) kwamba nini
kisemwe wakati wa kuleta Takbira tunapoelekeya kusali,
lakini Ibn Mas’uud alikuwa akisema yafuatayo:
Allaahu Akbar
(mara mbili) (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa)
Laa Ilaha
Illallaaha (Hapana
Mola Ila Mwenyezi Mungu)
Allaahu Akbar
(mara mbili) (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa)
Wa Lillaahil
Hamdu (Na Shukrani
Zote ni za Mwenyezi Mungu)
[Imesimuliwa na Ibn Abi Shaybah].
6)
Ni
Sunnah kwa wenye kusali Salaa ya ‘Iyd kusali kwenye Musallah
(katika uwanja ulio wazi) na sio Misikitini. Mtume (s.a.w)
hakuwahi kusali Salaa ya ‘Iyd Msikitini. Abu Sa’iyd (r.a)
amesimulia: “Mtume (s.a.w) alikuwa
akienda kusali ‘Iyd-l-Fitr na ‘Iyd-l-Adh-haa kwenye
Muswallaa, na kitu cha awali alichokuwa akikifanya ni
kusali.” [Al Bukhaary na Muslim]
7)
Salaa ya ‘Iyd haina Adhana wala Iqaamah. [Muslim].
8)
Ibn
‘Abbaas amesimulia: “Mtume (s.a.w)
Alisali rakaa mbili kwa ajili ya ‘Iyd na hakusali tena baada
yake au kabla yake.” [Al Bukhaariy]
9)
Jabir (r.a) amehadithia: “ Mtume
(s.a.w) alikuwa akirudi kutoka kwenye Salaa ya ‘Iyd-l-Fitr
kupitia njia tofauti na ile aliyoendea.” [Al
Bukhaariy].
10) Siku
ya Sikukuu inaruhusiwa kusikiliza nyimbo za Kiislaamu
(Nashiyd, bila ya kutiwa ala za muziki) hususan kwa watoto.
[Al Bukhaariy na Muslim]
Yaliyokuwa
Bid’ah katika ‘Iyd
Ni
Bid’ah (uzushi katika dini):
1)
Kunyoa ndevu hasa kwa makusudi ya kukusudia ‘Iyd. Mtume
(s.a.w) ametukataza kunyoa ndevu zetu; ni aibu kufanya hivyo
katika siku kubwa ambayo ni ya kufafanua na kudhihirisha
tofauti ya sherehe zetu na zile za Mushrikin, Muislaam
hunyoa ndevu akajisafisha kabisa na kuonekana kuwa hana
tofauti (hufanana) na Mushrikin.
2) Kuwaiga
Mushrikin katika mienendo yao na mavazi yao, na kupeana
mikono na Wanawake. Mtume (s.a.w) amesema:
“Ni bora kwa mwanamme kupigwa
sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa
mwanamke ambaye si halali yake.”
[Silsilat Al Ahadiyth Swahiyhah -
Sheikh
Al Albaaniy]
3)
Kusikiliza
muziki siku ya ‘Iyd. Mtume (s.a.w) amesema:
"Kutakuja watu katika umma wangu
watakaozini, wanaume watakaovaa hariri, wengine watakunywa
ulevi, na muziki utahalalishwa.” [Al Bukhaariy, Abu
Dawuud na Al Bayhaqiy].
4)
Wanawake kutovaa vazi la stara (hijaab). Kufanya hivyo ni
kusherehekea ‘Iyd na ilhali kunatendwa dhambi kubwa.
5)
Kuzuru
makaburini hususan siku ya ‘Iyd. Inaruhusiwa kuzuru
makaburini siku yoyote kwenye mwaka lakini isiwekwe kuwa
siku ya ‘Iyd ni maalumu kufanya hivyo.
6)
Kuharibu
pesa na kufanya israfu ya chakula badala ya kuwapa maskini
(na mafakiri).
Tunamuomba
Allaah (s.w.t) Atusaidie tuepukane na Bid’ah, na Atuelekeze
kwenye kuzifuata Sunnah za Mtume Wake (s.a.w).
|